Hii ndiyo elimu itakayokomesha ajira zinazodhalilisha Watanzania nje

Muktasari:

Mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ongezeko la watu lisiloakisi fursa za kazi, vimechangia baadhi wa wahitimu kuingia kwenye mtego wa ajira zinazodhalilisha nje ya nchi.

Dar es Salaam. Kila mzazi anayesomesha mtoto huwa na matumaini ya kuhakikisha anapata ajira stahiki kulingana na ujuzi alioupata.

Hata hivyo, hali si shwari siku hizi kwani mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ongezeko la watu lisiloakisi fursa za kazi, vimechangia baadhi wa wahitimu kuingia kwenye mtego wa ajira zinazodhalilisha nje ya nchi.

Shirika lisilo la Kiserikali la kuzuia ongezeko la wahamiaji haramu (PRIF), likishirikiana na shirika linalojihusisha na afya ya jamii na ustawi Afrika (Comheswa), yamebaini ukubwa wa tatizo la ajira nchini linalochangia ongezeko la usafirishaji haramu wa binadamu.

PRIF na Comheswa katika utafiti wenye kichwa; Uwepo wa ajira za kulazimishwa miongoni mwa wafanyakazi wa ndani nchini Tanzania," umeweka wazi ukweli wa kutisha juu ya wafanyakazi hawa katika jitihada za kukabiliana na ukosefu wa ajira nchini Tanzania.

Utafiti huo unabainisha kwamba huenda elimu ya Tanzania haiwaandai wahitimu kukabiliana na changamoto za kimaisha, huku ukosefu wa stadi stahiki ukishika kasi kubwa suala linaloongeza chachu kwa Serikali kuboresha mitalaa, inayolenga kuwaandaa wahitimu kujiajiri.

Kupitia uchunguzi wa kina uliotumia njia mbili tofauti za utafiti; utafiti wa ubora na kiasi (Quantitative and Qualitive Approach), imebainika kuwa idadi kubwa ya wafanyakazi wa ndani, mara wanapokuwa nje ya nchi hukabiliwa na tatizo la unyonyaji na kulazimishwa kufanya kazi kinyume na makubaliano na pengine hupokonywa uhuru wao.

Utafiti huo uliotumia mbinu za hali ya juu za sampuli; 1,052 na 788, unaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya wafanyakazi wa ndani wa Kitanzania nje ya nchi wamebadilishwa kuwa watumwa wa ndani.

Dk Angela Mbilinyi, mtafiti mkuu wa mashirika yasiyo ya kiserikali; PRIF na Comheswa alisisitiza umuhimu wa matokeo haya, akisema: "Utafiti wetu unatoa mwanga kuhusu unyonyaji uliokithiri unaokabiliwa na wafanyakazi wa ndani wa Kitanzania nje ya nchi. Utafiti wetu unapendekeza umuhimu wa Serikali kuweka hatua za haraka kukabiliana na janga hili ili kulinda haki na ustawi wa watu hawa walio katika hatari."

Miongoni mwa mambo yanayotofautisha nchi tajiri na zile masikini ni ajira. Katika nchi mfano zile za Ulaya, watu ni wachache na ajira ni nyingi. Kwa lugha nyingine, kuna kazi zinazokosa watu wa kuzifanya.

Kwa sababu hiyo nchi hizo kuanzisha programu za kuchukua wahamiaji kutoka mataifa masikini, ama wakimbizi na watafuta hifadhi kutoka maeneo yenye migogoro na vita, kwenda kuziba hilo pengo la uhaba wa rasilimali watu.

Lakini katika mataifa masikini hasa barani Afrika, watu ni wengi na kazi ama ajira ni chache. Afrika ndilo bara lenye vijana wengi kuliko bara lolote. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, asilimia 70 ya wakazi wa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara wako chini ya umri wa miaka 30.

Ajira tatizo

Akibainisha uwepo wa tatizo la ajira, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba Januari 07, 2022 alisema: “Serikali yenu, tunajua ukubwa wa tatizo la ajira na tutajitahidi kutengeneza fursa mbalimbali ili vijana wapate ajira.”

Kuna namna mbili ya kuangalia ukubwa wa tatizo la uhaba wa ajira. Mosi, kuangalia matukio yanayoashiria moja kwa moja uwepo wa tatizo hilo.

Pili, kuziangalia takwimu kwa mujibu wa Serikali au mashirika yanashughulika na tafiti za aina hiyo. Aliyekuwa, Waziri Wa Tamisemi, Angellah Kairuki, alizungumza na vyombo vya habari na kueleza kuwa, waomba ajira 419 walidanganya ni walemavu kati ya waombaji 171,916 walioomba katika kada ya ualimu na afya kupitia wizara hiyo.

 Katika kada hizo mbili, waliopata ajira ya ualimu ni waombaji 13,130. Upande wa afya ni 5,319. Kwa hesabu za jumlisha na toa; jumla ya waliopata ajira katika kada zote mbili ni watu 18,449, na walioachwa kwa sababu mbalimbali ni 153,512.

Hii inatoa picha pana ya ukubwa wa tatizo la ajira. Licha ya kundi kubwa la waombaji wa nafasi ya ualimu kuachwa, kelele juu ya uhaba wa walimu katika shule za Serikali bado zitaendelea kusikika.

Kufuatia mkanganyiko huu ndipo mjadala wa ajira unatupeleka katika kauli chechefu; Serikali haina pesa za kuajiri walimu wote na shule za Serikali zina uhaba wa walimu.

Juni 2014 zaidi ya watu 10,000 walijitokeza katika uwanja wa taifa, Dar es Salaam kufanya usaili wa maombi ya kazi katika Idara ya Uhamiaji iliyohitaji watu 70 pekee..

Ukosefu huu mkubwa wa ajira husababisha vijana wa Kitanzania kukubali kutoroshwa kwa njia haramu, wakiamini kuwa nje ya nchi kuna neema na kujikuta wakiwa kwenye lindi la ufukara na unyonyaji wa kutisha.Wahitimu kama hawa wanapaswa kuwa na maarifa ya kutosha yanayowawezesha kujiajiri wenyewe wakiwa nchini.

Mkurugenzi mkuu wa Comheswa, Furaha Dimitrios, anashauri kuwa kufuatia ongezeko la idadi la Watanzania wanaoafirishwa kufanya kazi nje ya nchi kutoweza kudhibitiwa na idara husika, ni bora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikaweka idara inayoshughulika na ustawi wa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi katika kila balozi husika.

Kwa mujibu wa Furaha, uwepo wa idara hii katika balozi utasaidia sana kujua idadi ya Watanzania waliotoroka ama kusafirishwa kwa mbinu zinazokiuka sheria na kuwarudisha nyumbani.

Anasema wakirudi kuwe na mbinu za kuhakikisha wanapata mitaji na mbinu stahiki za kumudu maisha.

Hayo anasema yanapaswa kufanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali na wizara yenye dhamana na vijana.

Kwa mujibu wa Furaha, uwepo wa idara hii katika balozi utasaidia sana kujua idadi ya Watanzania waliotoroka ama kusafirishwa kwa mbinu zinazokiuka sheria na kuwarudisha nyumbani, huku mbinu za kuhakikisha wanapata mitaji na mbinu stahiki za kumudu maisha nchini mwao zikifanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali na wizara yenye dhamana na vijana.

Kwa mujibu wa mtafiti mkuu, Dk. Angela Mbilinyi, baadhi ya Watanzania waliosafirishwa nje ya nchi pasipo kufuatia taratibu walibainika kuwa wamebadilisha majina, huku wakiogopa kutoa taarifa sahihi katika balozi husika kufuatia tuhuma za kugushi nyaraka.

Dk Angela anasema endapo taratibu na miongozo itafuatwa Watanzania wanaweza kupata fursa nyingi za ajira nje ya nchi pasipo kuingia migogoro na idara ya Uhamiaji, kwani zipo nchi nyingi kama Australia, Suadi Arabia na Ujerumani zinazohitaji nguvu kazi ya kutosha ambayo pengine ingepatikana kutoka Barani Afrika.

Ndio maana April 16 mwaka jana, vijana waliofuata taratibu za kupata ajira nje ya nchi  waliipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuwezesha na kulinda haki zao baada ya kupata fursa za ajira nje ya nchi.

Pongezi hizo zilitolewa wakati wa hafla ya kuwaaga vijana 50 waliopata fursa za ajira nchini Saudi Arabia kupitia ushirikiano kati ya Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA) na kampuni ya wakala wa ajira, Bravo Job Center Agency.

Exaver Jauri, mmoja wa wanufaika, alisisitiza umuhimu wa kuacha dhana potofu kuhusu ajira nje ya nchi, akieleza kuwa Serikali imekuwa ikiratibu na kusimamia vyema ajira za Watanzania hao.

Mkurugenzi wa Huduma za Ajira,  Joseph Nganga, alisema juhudi za TaESA ni bayana katika kuunganisha watafuta kazi na waajiri pamoja na kusimamia taratibu zote za ajira za Watanzania nje ya nchi. Alisisitiza ushirikiano wa karibu na balozi zetu ili kuhakikisha kuwa ajira zinazotolewa ni halali na za heshima.

Kwa mujibu wa Nganga Serikali imeingia makubaliano na nchi mbalimbali ili kujenga misingi imara ya ajira na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, huku akiwasihi vijana kufanya kazi kwa bidii, uaminifu, na kuzingatia misingi ya maadili ya Kitanzania.

Mwenyekiti wa kampuni ya Bravo Job Center Agency, Abbas Mtemvu aliwapa hamasa vijana kujitokeza kwa wingi kujisajili na TaESA ili kunufaika na fursa za ajira zinazopatikana nje ya nchi.

(Makala haya yameandaliwa na Adonis Byemelwa, mwalimu na mtafiti wa masuala ya elimu. Anapatikana kwa namba 0758 884 436)