Hoja za Kishimba zaja na kozi ya udalali CBE

Muktasari:

  • Chuo cha CBE kikianzisha mtalaa wa madalali mtakosa kweli wanafunzi, maana madalali ndio wamechukua ajira zaidi.” Ni kauli ya mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba alipotoa mada kwenye kongamano la Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).


Chuo cha CBE kikianzisha mtalaa wa madalali mtakosa kweli wanafunzi, maana madalali ndio wamechukua ajira zaidi.” Ni kauli ya mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba alipotoa mada kwenye kongamano la Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

Kishimba ambaye ameshawahi kusema bungeni kuwa aliishia darasa la nne, amekuwa maarufu bungeni kutokana na hoja za kipekee ambazo licha ya kuonekana kuwa ni hoja nyepesi, lakini mara nyingi huibua mijadala hasa kuhusu elimu, biashara na malezi.

Mwaka jana Chuo cha Elimu ya Biashara ( CBE), walimkaribisha Kishimba kuwa mmoja wa watoa mada kwenye kongamano lililokuwa na lengo la kuonyesha fursa za kibiashara, kuziweka wazi tafiti za kibiashara zilizofanyika na kupata uzoefu kwa wafanyabiashara waliofanikiwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa chuo hicho, Profesa Emanuel Mjema, Kishimba alialikwa kama mmoja wa watoa mada na kuelezea mafanikio yake na hoja zake kuhusu elimu anazozitoa bungeni.

Katika kongamano hilo, Kishimba alizungumzia kuhusu umuhimu wa elimu kwa madalali.

Kwa mujibu wa Profesa Mjema, Kishimba aliwaeleza kuwa udalali ni eneo linalotoa ajira kubwa, hivyo ni muhimu wakaanzisha mitalaa ya udalali ili kuwapa uelewa namna ya kufanya kazi zao kwa namna bora.Alisema walichukua wazo la mbunge Kishimba na sasa wameanzisha kozi ya madalali.

Dk William Gomera ambaye ni mmoja wa walimu wa CBE, alisema wataanza na kozi za muda mfupi ya awali ya siku tano (foundation course), baadaye watakuwa na kozi ya kati (intermediate course) ya siku 10 na kozi ya mwisho.

Alisema watatathmini maendeleo ya kozi hiyo na baadaye wataanzisha kozi za muda mrefu za ngazi ya cheti, diploma na shahada.


Watakachofundisha

Dk Gomera alisema watafundisha namna ya kutumia teknolojia kuungana wao kwa wao (networking) kati ya madalali. Itasaidia kupeana taarifa na kuwatoa sokoni madalali feki.

Alisema pia kozi itahusu sheria za nchi, jinsi ya kumtafuta mteja na jinsi ya kumpatia huduma, huduma baada ya kumpangisha au kumuuzia nyumba au kiwanja mteja.

Dk Gomera alisema huduma hiyo inahusu dalali kuwa na kanzidata ya wateja na wenye mali ili kama kuna changamoto yeyote waweze kuwasiliana na pia kama mpangaji amemaliza mkataba wake anaweza kuwasiliana naye kumtafutia huduma nyingine.

“Siyo ukishawapangisha umeachana nao, huduma baada ya huduma ni muhimu ili kutengeneza ‘network’ na wapangaji na wenye nyumba kwa kuwa nyumba ni bidhaa ambayo ipo siku zote,” alisema.

Dk Gomera alisema kuna migogoro mingi sana kwenye ardhi na mingi inasababishwa na madalali.

“Dalali anajua nyuma ya pazia kuhusu kiwanja au kuhusu nyumba. Kwa hiyo tukiwapa elimu kwanza itatusaidia sana kupunguza migogoro kwenye ardhi na nyumba kati ya mpangaji na mpangishaji. Lakini, pia itawasaidia kuwainua kiuchumi na kuwafanya wawe na sauti moja,” alisema Dk Gomera.


Mada ya Kishimba

Kwenye kongamano la CBE, Kishimba alisema eneo la udalali lina ajira kubwa, lakini haimo kwenye mital aa na watu wa Necta (Baraza la Mitihani la Taifa Tanzania) haoni kama wataikubali.

“Na madalali ndio wanaofanya kazi nzuri sana, nafikiri hata kuwaletea wanafunzi, baadhi ya vyuo mnaletewa na madalali. Kama dalali anakuletea wewe wanafunzi, wewe kwa nini hutaki chuo cha madalali kiwe kwenye mitalaa yako?

Kishimba alisema kumfundisha dalali ni rahisi kwa sababu yeye haitaji cheti, maana haendi kufanya kazi kwa mtu.

“Yeye akiona ameelewa mwache aende. Halafu wewe utapata wanafunzi wazuri, mtu analipa anasema nimeelewa niache niende si bora, wala hatakulalamikia nafasi ya ajira.

“Maana yeye amekuja umfundishe kwamba unaanza udalali inabidi uwe na ‘diary’ (daftari la kumbukumbu), uwe unaandika, unafanya ‘photocopy’ (durufu) ya ‘documents’ (nyaraka), unaelewa ‘location’ (eneo), unasema- nyumba hii imelipiwa mpaka tarehe fulani, yaani unamsaidia dalali kuwa uptodate (wa kisasa). Maana najua malalamiko ni mengi sana ya ajira.Samia ampa tano

Rais Samia Suluhu Hassan naye aliwahi kueleza namna anavyofuatilia hoja za mbunge Kishimba anazozitoa bungeni na aliiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuangalia upya mfumo wa elimu ambao utakuwa na manufaa kwa wanafunzi tofuati na uliopo sasa ambao umeshindwa kumwandaa mwanafunzi kujitegemea na kwamba hiyo ni dalili mbaya kwa Taifa la Tanzania.

“Kuna mbunge mmoja anaitwa kishimba, (Jumanne- Mbunge wa Kahama Mjini), huwa akisimama bungeni kuongea wabunge wanacheka sana.

“Lakini, mimi huwa namsikiliza kwa makini, ana hoja nzuri sana, kuna siku alizungumzia kuhusu suala la elimu, hivi ni nani aliyesema mtu asome darasa la kwanza, darasa la pili, la tatu, …sita, anaanza na miaka sita, akirudi ana miaka 27 hajui kulima, anarudi na karatasi yake ya ‘degree’ alafu mnataka ajiajiri... alisema Rais.


Hoja zake bungeni

Miongoni mwa hoja alizowahi kutoa Kishimba bungeni ni pamoja na kuitaka Serikali ipeleke muswada bungeni utakaomwezesha mzazi kumshtaki mtoto ambaye anakataa kumpatia fedha wala kupokea simu ya mzazi wake.

Kishimba alisema kuwa mzazi au mlezi ambaye hamsomeshi mtoto wake iko sheria ya kushitakiwa kwa kutotimiza wajibu wake wa kusomesha mtoto, lakini hakuna sheria ambayo inaweza kutumika kumshtaki mtoto ambaye ameshindwa kumsaidia fedha mzazi wake au hata kupokea simu.

Kishimba pia aliwahi kuzungumza bungeni kuhusu utoro wa wanafunzi shuleni, akisema utafiti na uzoefu walionao, watoro ndiyo watu waliofanikiwa katika maisha. Hivyo alihoji kwa nini Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, isianzishe mtaalaa wa watoto watoro na watu wazuri (wasiokuwa watoro).


Wasifu wake

Jumanne Kibera Kishimba, alishinda ubunge kwa tiketi ya chama hicho kwa miaka 2015 – 2020.

Kwa mujibu wa tovuti ya Bunge inaonyesha Kishimba kuanzia mwaka 1966 hadi mwaka 1969 alisoma Shule ya Msingi Isagehe, kuanzia mwaka 1970 hadi mwaka 1972 alisoma Shule ya Msinhi Mpera na kuanzia mwaka 1975 hadi mwaka 1976 alisoma Shule ya Msingi Isagehe na kupata chetti cha CPEE. Alizaliwa mwaka 1953.

Ni Mkurugenzi wa ‘Imalaseko Supermarket’ kuanzia 1977 hadi mwaka 2015.

Ni mjumbe wa Kamati Viwanda, Biashara na Mazingira kuanzia mwaka 2021 hadi sasa.