Maajabu ya mtoto mwenye mtindio wa ubongo shuleni

Mtoto Joan Minja (11) (kjatika baiskeli maalum ya walemavu) 

Mtoto Joan Minja (11), amedhihirisha kwamba watoto mwenye ulemavu wakijengewa mazingira mazuri ya kielimu anaweza kufanya vizuri kitaaluma kutokana na kufanya vizuri darasani tangu akiwa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Masia Mamba, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimajaro.

Joan ambaye alizaliwa na changamoto ya mtindio wa ubongo, afya yake imekuwa ikiimarika kutokana na kuendelea kupatiwa matibabu ya utengamao katika kituo cha CCBRT Moshi.

Mtoto huyo ambaye kwa sasa yupo darasa la sita katika shule hiyo, alipofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nne mwaka 2021 alipata ufaulu wa daraja A katika masomo yote aliyofanya.

Kutokana na changamoto yake ya kiafya, hawezi kushika kalamu na kuandika, hivyo wanafunzi wenzake humsaidia kuandika kile walichofundishwa darasani katika masomo yote.

Mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Upendo Ngowo anasema kutokana na changamoto hiyo hata kipindi cha mitihani shuleni hufanya kwa kuulizwa maswali papo hapo na mwalimu wa somo husika, kisha naye hujibu na kuwekewa alama alizopata kwa aliyojibu kwa usahihi.

“Kipindi cha mtihani wa Taifa wa darasa la nne pia alifanya kwa njia hiyo, baada ya Halmashauri ya Moshi kuridhia utaratibu huo baada ya kupata kibali kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

“Matokeo ya mtihani wa darasa la nne yalipotoka, Joan alipata ufaulu wa daraja A baada ya kupata alama A katika masomo yote aliyofanya," anasema mwalimu Ngowo.

Kutokana na changamoto hiyo, anasema hata mfadhili alipofika shuleni hapo, aliamua kumjengea choo pamoja na kujenga ngazi mtelezo eneo hilo la shule.

Matokeo ya kitaifa ya darasa la nne katika mtandao wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), yanaonyesha Joan amepata alama A katika masomo yote isipokuwa somo la hisabati alilowekewa X.


Ofisa elimu maalumu

Ofisa Elimu Maalumu katika Halamshauri ya Moshi, Innocent Kaoko aliulizwa na Mwananchi kuhusu uratatibu huo wa ufanyaji mitihani, anasema utaratibu huo hutumika kwa wanafunzi wenye uhitaji maalumu na ni wa kitaifa.

Anasema kwamba wakati wa usaili wa wanafunzi kwa ajili ya mitihani ya kitaifa kila mwaka (kati ya Februari na Machi) hubainisha wanafunzi wote wenye mahitaji maalumu.

Baada ya kuwabainisha, hufuata utaratibu wa kuainisha aina za changamoto kwa wahitimu na kisha kutumia taarifa Necta.

"Kwa wenye changamoto ya viungo kama Joan tunawapiga picha na kuzituma Necta...utaratibu huu pia hufanyika wakati wa kuwapangia shule wanafunzi waliohitimu darasa la saba," anasema.

Akizungumza somo la hesabu mwanafunzi kuwekewa alama ya X, anasema somo hilo hakulifanya kwa kuwa linahitaji kufanya mahesabu, ambayo hawezi kufanya kwa kuwa hawezi kushika kalamu.

"Watoto aina ya Joan wanaweza kufanya hesabu rahisi zinazohitaji majibu ya moja kwa moja, na sio za calculation nafikiri hiyo ndio sababu," anasema.

Hata hivyo, baadaye alipoulizwa Mwalimu Ngowo kuhusu suala hilo, alikiri Joan kutolifanya mtihani wa hisabati kutokana na kutokuwapo vifaa vilivyohitajika ambavyo angewefanya kufanya mtihani huo.

“Vifaa hivyo vilikuwa havijaandaliwa, kwa sababu ilikuwa ni mara ya kwanza ndio maana kulikuwa na changamoto hizo ila Necta wamesema akiwa darasa la saba wataviandaa mapema,” anasema.


Kauli ya Mwalimu wa darasa

Exaud Kimario, anasema Joan ni mwanafunzi msikivu na pia anaelewa haraka kile anachofundishwa darasani.

Mwalimu huyo anasema pia wanafunzi wenzake humsaidia kuandika kile walichofundishwa katika kila somo ili baadaye aweze kujisomea.

Anasema hata katika somo la hesabu akishafamu kanuni ya mada husika, inakuwa rahisi kwake kupata jibu kwa swali atakaloulizwa.

“Amekuwa akishika nafasi ya kwanza kwenye mitihani shuleni tangu akiwa darasa la kwanza,” anasema mwalimu huyo.

Mwalimu huyo anayefundisha somo la hisabati na maarifa ya jamii anasema Joan anapofahamu kanuni za hesabu, mfano PAI anaweza kujibu Kwa usahihi.

Kutokana na hilo, anashauri Serikali iwapatie vya kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Akizungumzia ushirikiano na wanafunzi wenzake, anasema humsaidia katika mambo mbalimbali ikiwamo kumwelewesha zaidi pale ambako hajaelewa masomo na pia kumsindikiza kwenda chooni na kumrudisha darasani.
Ndoto yake

Mwanafunzi huyo anayependa masomo ya hisabati, Kiingereza na sayansi anasema ndoto yake ni kuwa daktari wa watoto ili awasaidie watoto wenye changamoto mbalimbali.

Wanafunzi wenzake wanasemaje?

Colin Leole na Pendo Mangowe wanasema huwa wanamsaidia kuandika mada mbalimbali za masomo waliyofundishwa na inapotokea hajaelewa baadhi ya mambo katika masomo huwa wanamuelekeza.

"Anapozungumza tunaelewa (anazungumza kwa tabu) hivyo huwa tunamsaidia kwenda chooni na katika mambo mengine


Mzazi wa Joan

Mwalimu Ngowo ambaye pia ni mama mzazi wa Joan anasema alipozaliwa hawakugundua changamoto yake mpaka alipofikisha mwaka mmoja, kwani mikono na miguu yake haikuwa na nguvu na pia alikuwa hawezi kuzungumza, huku akiwa anatokwa na udenda wakati wote.

Anasema alimpeleka hospitali kadhaa bila mafanikio, ndipo baadaye anasema alielekezwa kwenda CCBRT Moshi ambako alianza kupatiwa matibabu kwa njia ya mazoezi.

Anasema wakati anaanza mazoezi alikuwa hawezi kuzungumza na mikono pamoja na miguu haikuwa na nguvu, hivyo alikuwa hawezi kukaa wala kutembea.

“Alikuwa akitoka udenda muda wote na alikuwa hawezi kushika kitu chochote, ila sasa nashukuru Mungu kidogo anaweza kushika vitu na pia anajitambua kwa kiasi fulani,” anasema.

Anasema baaada ya kufanya mazoezi kwa muda, Joan alianza kutembea akiwa na miaka sita na mpaka sasa anaendelea kumpeleka kwenye mazoezi.

"Isingekuwa CCBRT sijui ningekuwaje? Wamemtengenezea kiti mwendo kinamsaidia sana katika mizunguko ya hapa na pale. Nawashauri wazazi wengine wenye watoto wenye ulemavu wasiwafiche majumbani, kwani wanawakosesha haki zao za msingi,” anasema Mwalimu Ngowo ambaye ni mama wa watoto wanne, Joan akiwa mtoto wa kwanza.

Anasema kwa sasa Joan anaelewa kile anachofundishwa shule na hata anapoelekezwa nyumbani, ana kumbukumbu kwa vitu anavyoekelezwa.


Changamoto za malezi

Ingawa wanafamilia wanampa ushirikiano mzuri akiwamo mumewe, anasema baadhi ya watu huhusisha changamoto ya mtoto wake na suala la ufreemason.

“Watu wanadai tumemtoa mtoto freemason ili tupate mali. Nakwazika na maneno haya, maana nimepambana kwa muda mrefu kuhahakisha mwanangu anakuwa sawa,” anasema.

Changamoto nyingine, anasema ni gharama za kumhudumia kwani kila siku analazimika kutumia Sh4,000 za usafiri pikipiki wa kumpeleka shule na kumrudisha nyumbani na wakati mwingine anapompeleka CCBRT kufanya mazoezi analazimika kukodi gari kwa kuwa ni mbali na anapoishi.

“Kwa kweli kama huna kipato cha uhakika ni changamoto kuweza kumudu yote haya. Nashukuru mimi ni mwalimu napata mshahara, naweza kumhudumia mwanangu,” anasema.


Joan si wa kwanza

Baadhi ya watu wenye mtindio wa ubongo duniani, wamewahi kuwa waigizaji maarufu, wanariadha, wanamuziki, na hata washiriki wa mashindano ya urembo. Watu hao ni kama RJ Mitte, Keah Brown na Abbey Curran ambao ni uthibitisho kwamba hali hiyo haipaswi kuikatisha tamaa wanafamilia.