Maajabu ya shule za Mburahati na Mbagala

Ni kilomita 5.9 kufika Shule ya Sekondari Mbagala kutoka kituo cha mabasi Mbagala Rangi tatu.
Ukipanda bajaji utachangia Sh500, lakini ukipanda bodaboda utalipia Sh2,500 kufika shuleni hapo.
Shule hiyo yenye majengo mapya na mengine chakavu, inaelezwa kuwa ina wanafunzi zaidi ya 4,000 huku ikiwa na walimu 68 pekee.
Mazingira ya shule hiyo ni changamoto kwani ipo bondeni, baya zaidi hakuna uzio wa kuzuia wanafunzi kuchangamana na wananchi, hiyo inaelezwa kuwa mlango wa wanafunzi kukimbilia kuishi porini badala ya kuingia darasani kusoma.
Katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha pili yaliyotangazwa hivi karibuni, shule hiyo imeingia kwenye orodha ya shule zenye wanafunzi wengi waliofanya vibaya zaidi.Huwezi amini kama wanafunzi 204 wamepata daraja sifuri hivyo kulazimika kurudia mwaka.


Hali ilivyo Mbagala
Japo walimu wa shule zote wanasimangwa kwa matokeo hayo, Mwananchi limefuatilia undani wa anguko la wanafunzi hao kwa kuzungumza na wazazi, ‘wanafunzi, walimu pamoja na viongozi ambao wengine hawakutaka kutajwa majina yao.
“Tunapotoa mitihani ya darasani, wanafunzi 300 wanafeli sasa kwenye mtihani huu wa kidato cha pili hawa 204 waliofeli sisi tunaona kama maajabu kwa kuwa hatukutarajia haya… tulitegemea wengi wangefeli,” anasema mwalimu wa Mbagala ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Japo wananyooshewa vidole, mwalimu huyo anakiri kuwa walimu shuleni hapo hawana moyo wa kufundisha, kutokana na wanafunzi kuwa watukutu,
Tukio la kusisimua analosimulia mwalimu huyo lililotokea mwaka jana, ni mwalimu kuchomwa kisu cha tumbo na mwanafunzi wa kidato cha pili akiwa katika harakati za kuwafuatilia wanaotokomea porini.
“Yule mwalimu alikuwa akiwafuatilia wanafunzi ambao hawaingii darasani akachomwa kisu cha tumbo, Mungu alimsaidia tulimkimbiza Hospitali ya Temeke tukishikilia utumbo wake akanusurika kupoteza uhai huyo mwalimu hakurudi tena aliomba uhamisho akaondoka,” anasimulia mwalimu huyo.
Kuhusu uhaba wa walimu, mwalimu huyo anasema kwenye shule hiyo kuna jumla ya walimu watano wa sayansi.
Walimu hao, anasema wawili wa biolojia, wawili wa fizikia na mmoja wa kemia, huku wawili wengine wa somo hilo wakiwa wamestaafu.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kichechem Mussa Magenge anaeleza changamoto zinazoitafuna shule hiyo akiyaibua madudu mengine ya wanafunzi na wazazi huku akipaza sauti ya uhitaji wa uzio shuleni hapo.
Magenge anasisitiza kuwa hamahama ya wakurugenzi wilayani Temeke ndio inafifisha ndoto ya shule hiyo kupata uzio, hali ambayo inazorotesha ufaulu shuleni hapo.
“Kila mkurugenzi anapokuja akitaka kuanza majukumu yake anahamishwa, ndio jambo limesababisha uzio usijengwe hadi sasa, kungekuwa na uzio wanafunzi wangedhibitiwa,’ anasema na kuongeza: ‘’Walimu wachache waliopo wanajitahidi sana hata kuwafuatilia hao wanafunzi wanaotoroka mwishowe wanachomwa visu.’’
Magenge anasema, jambo alilolifanya ni kuunda polisi jamii kuwafuatilia wanafunzi hao na kuwaita wazazi wa wanafunzi hao kuwaonya kuhusu tabia ya watoto.
Naye mjumbe wa Serikali ya mtaa Kichemchem Halima Badi anasema: “Kiukweli shule ipo kwenye maeneo mabovu, hakuna uzio, kuna vichaka vya bangi, kamari watoto hawa wanawapiga walimu, uzio ungewekwa tatizo hili lisingekuwepo, tumeanza kulalamika enzi za Yusuf Makamba akiwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.’’
Anasema karibu na shule hiyo lipo eneo linaitwa miti mirefu, sehemu ambayo wanafunzi hushinda wakifanya ngono na kucheza kamari.


Akizungumzia matokeo hayo, Mbunge wa Mbagala Abdallah Chaurembo anasema, anguko la wanafunzi hao halina uhusiano wowote na shule kukosa uzio.
“Sidhani kukosekana kwa uzio ndiko kunawafanya wanafunzi kwenda kuvuta bangi, mwanafunzi aliyelelewa kwenye misingi mibaya atatoroka tu, kwa sababu shule hiyo sio bweni utaweka uzio lakini baada ya kipindi cha masomo watatoroka tu, jambo la msingi hapa ni suala la malezi kwa wazazi na walimu,” anaeleza.
Anasema mtatizo yanapotokea watu hukimbilia kutafuta visingizio, lakini ukweli ni kwamba wazazi hawatimizi wajibu wao. Anabainisha kuwa wazazi wana jukumu la kuwekeza kwenye elimu ya watoto
“Badala ya kuwekeza kwenye jambo lenye maana tunawekeza kulipa mgambo kuwakamata watoto wasioenda shuleni, wazazi wana jukumu kuwalea watoto wao, unakuta mtoto anashida kwenye banda la video, vigodoro kwa hiyo kuna shida kubwa,” anasema.

Wanachoeleza wanafunzi
Mmoja wa wanafunzi shuleni hapo, anasema, wanakabiliwa na upungufu wa walimu pamoja na matundu ya vyoo ambapo kwa sasa wana matundu matano pekee.
Anasema wapo wanafunzi zaidi ya 1,000 kidato cha tatu lakini walimu wa somo la hisabati ni wawili na biolojia ni wawili.
“Pia kuna suala la wanafunzi kutiana mimba wenyewe kwa wenyewe na wengine wanapata kutoka kwa wananchi waliopo jirani, kwenye darasa letu wapo wanafunzi kidato cha tatu wamepata mimba kutoka kwa wenzao na wananchi,’’ anasema.
Jambo lingine analosema mwanafunzi huyo, ni uhaba wa madarasa na wingi wa wanafunzi darasani unawaweka kwenye mtihani wa kuyaelewa kwa ufasaha yale wanayofundishwa.
Anasema kwa kidato cha tatu mwaka jana kuna mkondo A hadi N, akibainisha kwamba kwa kidato cha tatu pekee walikuwa wanafunzi zaidi ya 1,000.


Ufaulu wa kutia moyo
Wakati idadi hiyo kubwa ya wanafunzi kupata daraja sifuri ikizua gumzo, uongozi wa elimu Manispaa ya Temeke unasema bado shule hiyo ni kati ya shule zilizofanya vizuri.
Ofisa elimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Dk Janeth Barongo, anasema manispaa yake ina shule 32 zilizofanya mtihani wa kidato cha pili na Shule ya Sekondari Mbagala ipo nafasi ya 21 na hivyo kudai kuwa miongoni mwa zilizofanya vizuri katika wilaya hiyo.
“Ufaulu wa wilaya ni asilimia 84 mwaka huu, mwaka jana ulikuwa asilimia 80 maana yake ufaulu umepanda, ukiangalia kwa shule moja moja ndio unaona zipo zilizofanya vibaya sababu ya kwanza ni wingi wa wanafunzi ambao unachangia ugumu wa mwalimu kumfuatilia mwanafunzi,’’ anasema.
Kuhusu mkakati wa kuinua ubora wa elimu, anasema ni pamoja na kuhakikisha shule zinatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi ili wawe na ufuatiliaji mzuri wa masomo.
Dk Janeth anataja mkakati mwingine wa kunyanyua kiwango cha ufaulu wilayani hapo kuwa ni kuanzisha mitihani ya pamoja ndani ya wilaya hiyo kwa shule za sekondari hatua itakayoonyesha tatizo mapema na hatua kuchukuliwa.


Sekondari Mburahati
Si Mbagala pekee, kuna shule ya Sekondari Mburahati nayo imo kwenye mkondo huohuo kwani wanafunzi wake 229 walianguka katika mtihani huo.
Shule hiyo nayo walimu wake wananyooshewa kidole, lakini wazazi ni kama wamewatelekezea walimu watoto shuleni hapo.
“Fikiria mzazi nyumbani anashindwa kumuadhibu mtoto wake anamleta ananiambia mwalimu nisaidie kumchapa huyo mtoto nimemshindwa. Hii ina maana sisi walimu kazi zetu kuchapa, unakuwa na watoto karibu 1,000 wanakuzunguka wana tabia tofauti tofauti,”ni simulizi ya mwalimu jina linahifadhiwa akionyesha kasoro waliyonayo wazazi kwenye malezi hatua inayosababisha walimu kutupiwa mzigo.
Shule ya Sekondari Mburahati iliyopo Manispaa ya Ubungo ipo kwenye makazi ya watu. Hayo ni mazingira yanayotajwa na mwalimu huyo kuwa yanachangia ustawi mbovu wa wanafunzi hao.
Anasimulia kwamba, wakati mwingine wanafunzi huishia kwenye nyumba zilizo jirani kwenda kuvuta bangi na kufanya uchangudoa.
“Hata mwalimu anapowapa adhabu hutoroka kukimbia kwenye nyumba hizo na mwalimu anapowafuata, huambiwa mwanafunzi hajaonekana kwenye mazingira hayo,” anasema.
Jambo lingine analobainisha mwalimu huyo ni wanafunzi wengi wanaochaguliwa kuanza masomo shuleni hapo kutokuwa na uelewa, hali inayochangiwa na mfumo wa mitihani ya darasa la saba ambayo wanafunzi huchagua majibu pasipo kujieleza.
Kama haitoshi, shule hiyo anasema huchukua wale wanafunzi wenye ufaulu wa chini darasa la saba.
Anapendekeza wanafunzi wanaohitimu darasa la saba wachukuliwe wenye alama kuanzia 160 kuendelea na wale wenye alama pungufu waandaliwe shule za ufundi.
Anaibua hoja ya elimu bila malipo kuwa na mchango mkubwa kwa wanafunzi kuanguka, kwani wazazi wengi sasa hawana uchungu na elimu kwa kuwa hawagharamii kama ilivyokuwa zamani.
“Ukimuita mzazi aje tujadili maendeleo ya mwanawe haji, anapiga kona hata madaftari mzazi hamnunulii mtoto wake hadi mgombane, yaani tangu kuanza huu mfumo wa elimu bila ada, mzazi huwezi kumshirikisha kwenye jambo lolote, anaweza kuja mkakabaliana watoto wataanza kula mchana akitoka hapo ukimkumbusha anapiga kelele tunachangishwa, wanasiasa nao wanalipokea juu juu moto unakuwakia,” anasema.
Sintofahamu iliyopo kichwani kwa mwalimu huyo, ni kutojua nini wafanye, kwani wakati mwingine wanafunzi hufika darasani bila madaftari na wanaporudishwa kwenda kuzifuata au kupewa adhabu wazazi huwafokea walimu.


Wanachosema viongozi
Nao viongozi ambao majina yao wameomba kuhifadhiwa, wanasema shule hiyo haina uzio unaoweza kuwazuia wanafunzi kutochangamana na wananchi na hatimaye kujiingiza kwenye makundi hayo ya watumiaji wa bangi, wacheza kamari na biashara ya ngono, huku wengine wakipanga chumba mtaani na kwenda kuishi wakiwa wengi chumba kimoja.
Anasema miongoni mwa hao waliofeli wamo ambao ni kama walikuwa wameacha shule siku nyingi na baadhi ilibidi wakamatwe ili wakafanye mtihani huo.
“Tulitumia askari kwenda kuwakamata huko wanakokaa (nyumba waliyopanga) wakaletwa na magari ya polisi kufanya mtihani huku wakisimamiwa kwa mtutu…. mwanafunzi wa namna hii hawezi kufaulu hata kwa dawa,” anaeleza.
Jambo la kustaajabisha analotaja kiongozi huyo ni tukio la mwalimu kuporwa simu akitoa adhabu kwa wanafunzi waliochelewa na mwanafunzi aliyetenda tukio hilo kutokomea kwenye nyumba za majirani karibu na shule hiyo.
Anasema kibaya zaidi mwanafunzi anapokimbilia kwenye nyumba za majirani karibu na shule hiyo, walimu hawapewi ushirikiano.
Ukiachana na tukio hilo, yapo matukio ya wanafunzi wa kike kujiuza kwa kima cha Sh1,000 tena wakifanya hivyo kinyume na maumbile jambo ambalo linaipoteza shule hiyo kwenye ramani ya taaluma.
‘’Darasa moja lina wanafunzi 500 hapo mwalimu hana vifaa vya kufundishia madaftari atasahihisha muda gani, muda huo huo mwanafunzi anapanga kukupora kwa hiyo mazingira ya kufundishia ni magumu sana,’’ anaeleza kiongozi huyo.
Wingi wa wanafunzi na uchache wa walimu bado unaendelea kuwa mwiba kwani kiongozi huyo anasema, wakati mwingine watoto hulawitiana chooni na hata wanapobainika na kufukuzwa wakawalete wazazi, wazazi wenyewe wanapofika na kuelezwa hukana wana wao kuhusika na tabia hiyo.
“Mwalimu huyu huyu hatakiwi kuchapa, mwalimu huyu anakaa mbali, mshahara mdogo, anatishiwa na wazazi na wao inafika wakati wanakata tamaa anabaki kuangaliia tu anashindwa afanye nini kila kitu wakifanya yapo makatazo mengi,’’ anasema.


Maadili ya shule
Mmoja wa viongozi wa usalama anayeshughulika na kubadili tabia kwa wanafunzi jina limehifadhiwa, anasema wakati akianza programu hiyo kwa watoto watukutu, alipofika Serikali ya mtaa Mburahati alielezwa changamoto nyingi zinazoikabili shule hiyo.
Kiongozi huyo anasema aliomba miadi ya kufika shuleni hapo na kuzungumza na wanafunzi wa shule nzima pamoja na kukagua miundombinu ya shule hiyo na alichobaini ni kukosekana kwa uzio, jambo ambalo huwafanya wanafunzi kuwatoroka walimu.
Jambo lingine alilobaini kiongozi huyo ni mfumo wa utawala shuleni hapo kutokuwa imara hali inayowafanya wanafunzi kupewa adhabu ndogo tofauti na makosa wanayoyatenda.
“Kuna wakati nilishuhudia mwalimu alikuwa anatoa adhabu kwa wanafunzi waliochelewa, mmoja kati ya wanafunzi wale alipita nyuma ya mwalimu na kumpokonya simu na kutokomea nayo, baada ya wiki moja alirudi darasani, lile kosa lilipaswa kumfukuzisha shule lakini alitandikwa viboko tu akarudi darasani.
Kiongozi huyo amekiri kwamba yeye ndiye aliyesimamia wanafunzi hao kukamatwa na kupelekwa kwenye chumba cha mitihani kupitia askari waliovalia kiraia.


Hatua inayochukuliwa
Mmoja wa viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo naye hakutaka jina litajwe anasema wapo kwenye maandalizi ya kufanya vikao na wadau kubaini wapi palikuwa na changamoto hadi kusababisha anguko hilo kubwa la wanafunzi.
“Tayari tumeanza kuhoji wanafunzi na endapo tutabaini kuna uzembe wowote ulifanyika kuna watu watawajibika,” anaeleza.