Mjengwa: Vyuo vya maendeleo ya wananchi suluhisho la ajira

Mkurugenzi wa Karibu Tanzania Organization (KTO), Majid Mjengwa, katika mahojiano na Mwananchi Digital kuhusu mustakabali wa vyuo vya maendeleo ya wananchi.

Muktasari:

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi hivi karibuni, Mkurugenzi wa Karibu Tanzania Organization (KTO), Majid Mjengwa ambaye pia ni mdau wa vyuo hivyo, anasema pamoja na mengineyo vyuo hivyo vinaweza kubadili maendeleo ya Taifa na wananchi hususan upande wa ajira.

Dar es Salaam. Mwaka 1969 Rais mstaafu wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere alitembelea nchini Denmark,  na miongoni mwa mambo yaliyomvutia akiwa huko ni vyuo vya maendeleo ya wananchi.

Aliporudi nchini alianzisha maandalizi ya kuwepo kwa vyuo hivyo na hatimaye mwaka 1975 vikaanza.

Vyuo hivyo  ni falsafa yenye kuhusiana na watu wazima na maendeleo endelevu katika nchi za Nordic (Norway, Denmark na Sweden) vyenye historia ya kuwa na vyuo hivi tangu miaka ya 1800.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi hivi karibuni, Mkurugenzi wa Karibu Tanzania Organization (KTO), Majid Mjengwa ambaye pia ni mdau wa vyuo hivyo, anasema pamoja na mengineyo vyuo hivyo vinaweza kubadili maendeleo ya Taifa na wananchi hususan upande wa ajira.

Swali: Tuna vyuo vingapi vya wananchi na pengine msomaji angependa kujua maana na majukumu ya vyuo hivyo?

Jibu: Sisi Tanzania  tuna vyuo 55, kimoja kipo chini ya Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi) na kipo wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani na vingine 54 viko chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Lengo lake ni kupeleka maarifa na ujuzi kwa Watanzania walioko maeneo ya vijijini, kwa sababu idadi kubwa ya wananchi iko huko.

Vyuo hivi vinasimama katika mihimili mitatu, kwanza ni elimu endelevu ambayo hata kama mtu mzima akitaka kujifunza ujuzi pale, pili ni elimu ya ujuzi au ufundi na tatu ni elimu ya maendeleo ya jamii.

Kuna kozi fupi zinazoweza kuwa kati ya wiki moja mpaka miezi mitatu na ndefu inaweza kwenda miezi sita mpaka miaka miwili.

Huu mhimili wa pili ambao ni wa ufundi kuna fani mbalimbali kama useremala, umeme, ufundi bomba, umakenika.

Wanajifunza kwa lugha ya Kiswahili na hiyo inawarahisishia zaidi kupata mafunzo kwa lugha anayoielewa. Kwa sababu kama mtu yuko Ilula Iringa, soko lake liko huko, ili aelewe msumari, mbao, tunaona lugha ya mama ni muhimu.

Lakini haimaanishi kwamba lugha ya Kiingereza haina maana. Kwa hiyo Kiingereza katika vyuo vya maendeleo ya wananchi kinafundishwa kama somo.

Katika vyuo hivyo kuna masomo ya sekondari kwa wale walioikosa, kwa lengo la kuwapa ujuzi wale vijana waliokatishwa masomo kwa sababu mbalimbali, inawezekana ukawa ujauzito, ufukara au kukimbia ukeketaji.

Hivyo wanapata fursa hiyo kuendelea na masomo ya sekondari na wanapata fursa ya kuchagua fani mojawapo. Kwa hiyo mtu anamaliza kidato cha nne akiwa na kitu cha ziada.

Swali: Tunajua Mwalimu Nyerere alikuwa akijenga misingi ya sera ya Ujamaa na Kujitegemea. Je, vyuo hivyo viliakisi vipi sera hiyo?

Jibu: Vyuo hivi vinatekeleza falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea na ndio lengo la Mwalimu Nyerere kwamba watu wapate uwezo wa kujitegemea kwa kupata ujuzi.

Katika maendeleo ya jamii, utaona vyuo hivi viko kwenye jamii. Kwa mfano ukienda Namtumbo, kuna chuo cha maendeleo ya jamii pale, wanaweza kuomba kupata mafunzo ya kupambana na magonjwa yanayoathiri korosho, kwa hiyo chuo kina wajibu wa kutafuta wataalamu kwa ajili ya kozi fupi, ili kujua wadudu walioingia sasa hivi watu wafanyeje kupambana nao.

Chochote kile kinaweza kwenda kwenye chuo cha maendeleo kikafanyiwa mafunzo kusaidia wanajamii.Wapo hata wanafunzi walioshindwa kumaliza vyuo vikuu, wapo kule wanapata ujuzi, kama ujenzi wanapata ujuzi.

Kuna changamoto kubwa inayotatuliwa na vyuo hivyo, kuna kundi la vijana ambao wako mitaani hawajamaliza darasa la saba, wengine wamemaliza la saba, lakini hawajaenda sekondari. Kundi la tatu ni lile lililomaliza kidato cha nne lakini hawakwenda elimu ya juu.

Kundi lingine ni lile wanaomaliza vyuo vikuu ambao ni asilimia moja tu ndio wanapata ajira Serikali na sekta binafsi, wengine wanaishia kujiajiri na kutafuta ajira.


Wataalamu katika chuo kimoja cha maendeleo ya wananchi, wakionyesha aina mojawapo ya mafunzo ya ufundi wanayotoa kwa wanafunzi wao. Picha kwa hisani ya malya college na Moe

Kwa hiyo vyuo hivi vya maendeleo,  vinaweza kuwa suluhisho la kuwapatia ajira vijana hawa kwa kuwapa ujuzi mbalimbali.

Vyuo hivi vinajibu Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo kwa mwaka 2020 hadi 2025 katika huduma kwa jamii (ibara ya 18) inazungumzia elimu, vinatajwa vyuo vya maendeleo ya wananchi na wanaahidi kuvikarabati na kuongeza udahili kutoka wanafunzi 9,000 hadi 17,000 kuelekea 2025.

Swali: Umesema katika vyuo hivi wanafundisha mafunzo ya ufundi, hayo mafunzo yanatofautianaje na yanayotolewa na Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta)?

Jibu: Ukumbuke kwamba vyuo vya maendeleo ya wananchi vilianzishwa kabla hata ya kuwepo Veta. Vyuo hivi sasa vinatimiza miaka 50 na vina falsafa yake ambayo ni ile mihimili mitatu niliyotaja awali.

Kikubwa ni kwamba jamii husika inahusishwa katika kutatua mahitaji yake kupitia vyuo hivyo.Kwenye muundo wa vyuo hivyo, mkurugenzi wa halmashauri ni mwenyekiti wa bodi na miongoni wajumbe ni madiwani, wazee maarufu na maofisa maendeleo ya jamii.

Ni tofauti na Veta ambayo wanajamii hawawezi kwenda kuomba kozi pale, isitoshe, vigezo vyao ni tofauti, ni lazima uwe umefika ngazi fulani ya elimu,  ufanyiwe usaili, wakati vyuo maendeleo ya wananchi havihitaji usaili, ilimradi uwe unajua kusoma na kuandika lugha ta Kiswahili.

Swali: Bado kuna umuhimu wa hivyo vyuo, kwani nyakati zimebadilika tofauti na wakati Mwalimu Nyerere alipovianzisha?

Jibu: Hakika bado vina umuhimu, kwa sababu kama lengo ni kutaka watu kujitegemea, sasa wewe umetoka chuo kikuu, lakini huwezi kushika spana. Au una shahada yako ya uofisa rasilimali watu, sheria na nyinginezo, unazunguka kutafuta kazi, ni tofauti na yule aliyetoka chuo cha maendeleo ya wananchi ana ujuzi  anaoweza kujiajiri.

Ukiwa na nyundo yako na vifaa vyako, ukaonekana mitaani, unaweza kuitwa. Au ukikuta ujenzi unaendelea, unasema mimi ni fundi naomba hizi siku tatu nifanye kibarua hapa.Ni tofauti na mwingine akitembea na bahasha yake yenye wasifu wa kutisha.

Kwa hiyo nadhani bado kuna umuhimu, tena nadhani vyuo hivyo viongezwe, tuna ujenzi wa reli ya kisasa, tuna ujenzi mwingi unaendelea, kuna wahandisi na pia tunawahitaji mafundi hawa wa chini.

Swali: Tangu vyuo hivi vimeanzishwa miaka 50 iliyopita, ni mafanikio gani makubwa yaliyopatikana?

Jibu: Makubwa sana. Mifano iko mingi, lakini mmoja ni wa kijana aliyetoka chuo cha maendeleo ya wananchi baada ya kumaliza kidato cha nne miaka ya nyuma, akasoma ufundi wa magari.

Aliporudi akaajiriwa kwenye gereji za Ilala, ambako magari yanayopelekwa pale ni ya Wajapan. Hao Wajapan baada ya kuona huyo kijana ni hodari sana, kuna chuo huko Japan, wakamwambia wanamchukua akapate mafunzo huko kwa mwaka mmoja, ili atakaporudi aendelee kuwafanyia kazi.

Huo ni mfano mmoja tu. Kuna kijana mwingine yuko Zanzibar anatembea kwenye hoteli za kitalii anafanya ufundi wa umeme wa majokofu na majenereta, yeye alisoma chuo cha maendeleo cha Rufiji Mkoa wa Pwani.

Alikwenda Zanzibar wakati ule Makamu wa Rais ni Dk Mahmoud Gharib Bilal, alipotafuta fundi wa vifaa vyake vya umeme, akaambiwa kuna fundi huko Rufiji, wakampeleka akafanya vizuri na sasa anaendelea na kazi zake huko.Kwa hiyo ni vyuo vinavyotoa vijana wanoweza kutenda.

Tuko kwenye utafiti kuhakiki mafanikio ya vyuo hivyo, ambapo tutaangalia wanafunzi hao waliomaliza wamekwenda wapi, ili tupate takwimu ili kuwe na usahihi. Lakini kwa ujumla hizo program zimeonyesha mafanikio.


Ufundi seremala ni miongoni mwa aina za mafunzo yaa ufundi yanayotolewa katika vyuo vya maendeleo ya wananchi. Picha kwa hisani ya malya college na Moe.

Swali: Vyuo hivi vinakabiliwa na changamoto gani?

Jibu: Watu wetu wengi hali zao ni duni, hivyo wanategemea wazazi kuwalipia ada kwa sababu vyuo hivi havitoi mikopo. Sasa kwa hali ya uchumi baadhi ya wazazi wanashindwa kulipa Sh2050,000 kwa mwaka

Ni kiasi kidogo ukilinganisha na ruzuku ambayo Serikali inatoa, kwa sababu unalala pale kwenye bweni, unakula pale asubuhi mchana na jioni.

Hivyo Serikali ilipaswa ione kwamba elimu bila ada ilitakiwa iwepo pia kwenye vyuo vya maendeleo ya wananchi, ili tulipe kundi la vijana nafasi wasije kuingia kwenye wizi, ulevi na uhalifu mwingine.

Pia kuna changamoto za mabweni, hivyo waongeze mabweni ili kutoa nafasi kwa wanafunzi wengi.