Mwasi Mboya alivyoikwaa PhD akiwa na miaka 27

Muktasari:

  • Baada ya wazazi wake kumlipia kuanzia Shule ya msingi Mount Kibo jijini Dar es Salaam kisha Sekondari ya Pangahill mkoani Mbeya na Sekondari ya Wasichana Mariani iliyopo Bagamoyo, ilikuwa imetosha kwa Mwasi Mboya, kufungua macho yake kuangalia fursa za ufadhili wa elimu ya juu.

Baada ya wazazi wake kumlipia kuanzia Shule ya msingi Mount Kibo jijini Dar es Salaam kisha Sekondari ya Pangahill mkoani Mbeya na Sekondari ya Wasichana Mariani iliyopo Bagamoyo, ilikuwa imetosha kwa Mwasi Mboya, kufungua macho yake kuangalia fursa za ufadhili wa elimu ya juu.

Akiwa amefaulu vizuri masomo yake ya kidato cha sita ya fizikia, kemia na hisabati, elimu yote ya juu kuanzia shahada ya kwanza, shahada mbili za uzamili mpaka shahada ya uzamivu, amesoma kwa ufadhili alioupata kutoka kampuni tofauti katika vyuo vikuu vya Tanzania, Rwanda, Finland na Ujerumani.

Akiwa na umri wa miaka 28 tu, Mwasi Mboya ni daktari wa falsafa katika fedha na takwimu (PhD in Financial Econometrics and Statistics) kutoka Chuo Kikuu cha Leibniz Hanover cha Ujerumani, ambako anafundisha kwa sasa.

Mwandishi wetu Julius Mnganga amezungumza mambo na msomi huyu kijana anayesimulia mengi kuhusu safari ya maisha yake.

Swali: Katika umri mdogo umefanikiwa kupata shahada ya juu kabisa ya elimu. Nini siri ya mafanikio?

Jibu: Nianze kwa kujitambulisha. Mwasi ni mtoto wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto watatu wa Oscar Mboya wa Mbeya na Deva Urio wa Kilimanjaro.

Wote ni wajasiriamali wadogo. Siri kubwa ya kufika hatua hii, kwanza ni kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila ninachofanya. Pili, huwa napangilia malengo yangu mapema na kupanga mikakati ya kuyafanikisha kwa juhudi nyingi bila kuruhusu vikwazo na changamoto kunirudisha nyuma.

Mwisho ni ushirikiano wa upendo, mawazo na ushauri ninaopata kutoka kwa familia yangu, inanipa moyo na nguvu ya kusonga mbele bila kurudi nyuma. Wao ndio wanaonifanya nisikate tamaa kila nikikumbuka kuwa nina jukumu la kuwaweka mahala pazuri, na kuwa mfano mzuri kwa wadogo zangu.

Swali: Familia ilikusaidiaje kufanikisha ndoto ya elimu yako?

Jibu: Familia imenisaidia kwa kiasi kikubwa. Ukiacha ushauri na mawazo, baba yangu ndiye aliyenihamasisha kutambua kuwa naweza kutimiza ndoto zangu bila kujali hali yetu ya kiuchumi. Yeye ndiye alinitafutia ufadhili wangu wa kwanza wa masomo pale Karimjee Jivanjee Foundation akiwa kwenye harakati zake za kusoma magazeti.

Mama naye yaani sijui nianzie wapi maana ushauri na mawazo yake yalinijenga niamini kuwa ninaweza kutimiza chochote nitakacho. Nilikuwa namwambia nataka niwe daktari kabla ya kutimiza miaka 28 hata kabla sijaanza chuo na yeye alinipa moyo ingawa hatukuelewa tutafanikishaje malengo hayo.

Mara nyingi aliniasa nisiyumbishwe na mambo ya dunia.

Swali: Unao uzoefu wa mfumo wa elimu nchini na nje, kuna maeneo unaona yanapaswa kuboreshwa ili wahitimu wa nchini washindane vyema kimataifa?

 Jibu: Kwa uzoefu wangu, naamini elimu yetu ni nzuri na tuna nafasi kubwa ya kushindana kimataifa tukirekebisha maeneo machache tu mfano tupate walimu wa nje (visiting lecturers) mara kwa mara, pia tuwe na programu za kubadilishana wanafunzi ambayo huwapa fursa ya kwenda vyuo vya nchi nyingine kuja kujifunza kutoka kwa wenzao wanaosoma programu zinazoendana na walimu wetu vyuoni wapate maarifa mapya kwa kusoma kozi fupi.

Mwisho niseme tupo kwenye nafasi nzuri ila tuzidi kuwa na kiu ya kutaka kupata maarifa zaidi na kujifunza kutoka kwa nchi zilizoendelea.

Swali: Wanawake wengi hukimbia masomo ya sayansi ambayo wewe umeyasoma kuanzia sekondari, umemudu vipi hata ukafanya shahada tofauti za eneo hilo?

Jibu: Kwanza niwaondoe fikra potofu kuwa masomo ya sayansi ni magumu, wanawake hawawezi kuyamudu. Naamini mtu akiwa na malengo ya kuyafanikisha hatakiwi kuwaza ugumu maana haitamsaidia.

Kama una kitu unachokipenda basi utatafuta mbinu ya kuumudu ugumu utakaokutana nao kwa hiyo usikubali kukatishwa tamaa kwamba hutaweza. Kwa upande wangu huwa napenda sana kuongea na watu kusikia wanasema nini kuhusu jambo ninalotaka kulifanya na baadaye huwa nachuja ushauri huo na kuchukua ule wenye tija katika malengo yangu.

Kwa hiyo siku zote fuata ndoto zako na usiache kuongea na watu waliokutangulia kujua walipitaje ili ukikutana na vikwazo viwe ndani ya uwezo wako.

Swali: Kwa zaidi ya miaka 22 uliyoishi duniani umeitumia shuleni. Umepata uzoefu gani tofauti?

Jibu: Ni kweli nimetumia miaka mingi shuleni mpaka kuna muda huwa nachoka ila huwa naamini ni hali ya kupita hasa nikipata changamoto. Baada ya kuzoea kuwa shuleni muda mrefu naona ni hali ya kawaida na maisha mengine yanaendelea.

Kwa kusoma fani mbalimbali na nchi tofauti nimejifunza mambo mengi yaliyofungua upeo wangu wa kufikiria na kukabili changamoto hata kunipa fursa zaidi kielimu.

Swali: Elimu yako yote ya juu umesoma kwa ufadhili ambao vijana wengi nchini huukosa. Uhangaikaji wako ulikuwaje hata ukafanikiwa kirahisi?

Jibu: Elimu yangu yote ya juu nimesoma kwa ufadhili, natambua si rahisi kupata ufadhili lakini kwa upande wangu sikupata ugumu sana kwa sababu ufaulu wangu ulikuwa mzuri. Nilipohitimu shahada ya kwanza niliomba kusoma shahada ya pili Rwanda na nilipomaliza hapo nilipata ufadhili mwingine nchini Finland, kote huko ni kutokana na ufaulu mzuri.

Changamoto kidogo ilikuwa kutafuta PhD. Niliomba vyuo vitatu nikapata viwili, nikachagua Ujerumani nilikomaliza hivi karibuni. Kwa uzoefu wangu naamini inawezekana kupata ufadhili ukifuatilia vigezo na ukiweka juhudi kuandaa viambatanisho muhimu.

Inatakiwa kufuatilia katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu fursa za ufadhili wa masomo zinazotangazwa.

Swali: Unatamani kurudi nyumbani kulijenga Taifa?

Jibu: Hapa Ujerumani nilipata nafasi ya kufanya kazi huku nasoma PhD nikifund sha madarasa ya masters (shahada ya pili). Ukiachana na ndoto yangu ya kutaka kuwa professional actuary (mtaalamu wa bima), ndoto nyingine ilikuwa kufundisha elimu ya juu.

Nilipenda siku moja nifundishe chuo na nimeitimiza ndoto hiyo kwa miaka mitatu ya kusoma hapa Ujerumani. Ni matamanio yangu kuwa siku moja nirudi Tanzania kuitumikia nchi yangu na kutoa elimu kwa vijana katika fani na yale niliyojifunza katika nchi za wenzetu pamoja na kuhudumu katika nafasi za kazi itakayonifaa kwa fani yangu ili kutatua matatizo ya umma au sekta binafsi.

Swali: Ndoto yako katika elimu ilikuwa kuwa mtaalamu wa masuala ya bima na majanga. Kwa nini eneo hilo? Dk Mwasi: Nilipenda kubobea kwenye utaalamu wa takwimu bima sababu ni muunganiko wa fani ambazo kwa pamoja hutumika kutatua changamoto ngumu zinazozikabili kampuni na biashara. Pia, kutokana na mazingira ya changamano hizo nitapata nafasi ya kujipima na kutumia ujuzi wangu kuzitatua.

Jingine ni ukweli kwamba wataalamu wa takwimu bima ni wachache mno na wanahitajika kwa ukubwa na wanalipwa fedha nzuri hivyo sipaswi kuhofia kuhusu ajira. Faida nyingine ya mtaalamu wa takwimu bima ni kuwa na nafasi kubwa ya kujiajiri na kufanya kazi kwa ufanisi baada ya miaka kadhaa ya uzoefu.

 Swali: Sekta ya bima ni changa nchini na watumiaji wa huduma zake ni wachache. Unadhani nini kifanyike kuikuza?

Jibu: Ni kweli sekta ya bima ni changa nchini na mwitikio wake bado ni mdogo. Nadhani tunahitaji kutoa elimu zaidi kwa wananchi na kufikia maeneo mbalimbali nchini. Vilevile tunapaswa kuboresha na kuongeza huduma zetu ili kuendana na mahitaji ya Watanzania. itie mkazo kwenye sekta ya bima kwa kutunga sera rafiki.

 Swali: Tanzania kama yalivyo mataifa mengine duniani inatekeleza miradi mingi ya maendeleo ikitumia kampuni za nje za bima. Kuna cha kufanya kubadili hali hiyo? Jibu: Natambua kuna baadhi ya huduma za bima ambazo hatuna ujuzi nazo nchini na tunahitaji kampuni za nje kuzitoa jambo linalotugharimu pesa nyingi.

Ni wakati sasa wa kuwekeza katika elimu hii na kuhamasisha vijana kujiendeleza kielimu ili kupata nguvukazi yenye maarifa kama waliyonayo kwenye kampuni za nje. Juhudi hizi zihusishe kufanya mitihani ya kitaaluma ambayo inatolewa na jumuiya za kimataifa kama vile Australia, India, Uingereza, Canada na Marekani ambazo humchukua mhusika miaka kadhaa kuikamilisha.

Nchini tuna changamoto kwamba mitihani hii kwanza ni ghali kidogo na hatuna prometric centres (vituo vinayotambulika kimataifa) kufanyia mtihani hii mpaka twende Kenya. Kwa hiyo ningezishauri kampuni zetu pamoja na Serikali kuweka nguvu nyingi katika eneo hili ama kwa kutafuta vibali vya kujenga prometric centres au kuwalipia wafanyakazi kwenda kufanya mitihani hii ili kujiendeleza kielimu.

Swali: Kwa Watanzania wengi, baada ya masomo, hatua muhimu kwa msichana ni ndoa. Umejiandaa lini kuingia kwenye maisha hayo?

Jibu: Nafahamu kuwa ndoa ni suala muhimu na ni jambo linalotegemewa kwa msichana wa umri wangu. Nitaingia kwenye ndoa na kuwa na familia kwa wakati sahihi. Ushauri wangu kwa msichana yeyote, ndoa isikufanye uache kukimbizana na ndoto zako.

Kwa sisi ambao bado hatujaingia kwenye ndoa, tumwombe Mwenyezi Mungu atukutanishe na mtu atakayeunga mkono na kuheshimu ndoto zetu.

Nyongeza na Abeid Poyo