Wazazi wanavyofifisha jitihada za kuinua elimu Korogwe

Akiwa madarakani mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere alianzisha vita dhidi ya maadui watatu; ujinga, maradhi na umaskini.

Kiongozi huyu aliamini kama Tanganyika na baadaye Tanzania itaweza kupigana na maadui hao watatu kwa mafanikio, ingekuwa kisiwa cha maendeleo.

Ni miaka zaidi ya miaka 60 tangu vita hii ianze kupiganwa lakini mapambano yanaonekana kuwa magumu, pengine yakikwamishwa na ‘askari’ wenyewe.

Hili lithibitishwa na Mwananchi lilipotembelea Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Septemba 2023 na kubaini baadhi ya watu wanaoendelea kuwapa nguvu maadui hawa, hasa ujinga; adui anayewabeba wenzake; maradhi na umaskini.

Katika safari hiyo yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa mpango wa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali, ilibainika kuwa baadhi ya wazazi wanachangia watoto wao kuacha shule kwa kuwashawishi kufanya vibaya kwenye mitihani ya elimu ya msingi ili wasiendelee na sekondari.

Kimsingi, kinachofanywa na wazazi hawa ni kinyume cha maelekezo ya mwongozo wa Serikali uliotolewa Februari 2022, ambao unampa mzazi jukumu la kuhakikisha mtoto mwenye umri wa kuwa shule anapata haki ya kusoma pamoja na kumpatia mahitaji muhimu ya kumwezesha kuendelea vyema na masomo.
 

Wazazi tatizo

Katika kijiji cha Madumu tunakutana na mmoja wa wazee wa kijijini hapo Zuberi Makunya, ambaye anasema licha ya kutambua umuhimu wa elimu lakini matokeo hasi yanawafanya kupoteza matumaini.

“Tumeshaelimishwa vya kutosha tunaelewa umuhimu wa elimu lakini changamoto tuliyonayo hao watoto tuliowasomesha hatuoni matunda yake. Tumetumia fedha kuhakikisha wanapata elimu lakini wengi wao hawana ajira, hivyo hawana msaada hii inafanya tukate tamaa ya kuendelea kusomesha watoto wengine.

“Unauza ng’ombe wako ili mtoto aende shule, anamaliza masomo anarudi tena kukaa kijijini na kuwa mzigo kwenye familia hajapata ajira anakutegemea tena wewe umlishe, sasa kwa mwenendo huu hata wadogo zao wanaona na sie wazazi tunakata tamaa unaona heri umuache ajikite kwenye kilimo,”anasema Makunya.

Huo ni mfano mmoja wa wazazi walioamua kuipa kisogo elimu, katika halmashauri ya wilaya ya Korogwe, lakini wapo wazazi waliokwenda mbele zaidi na kuwazuia watoto wao wasifaulu kwenye mtihani wa elimu ya msingi kwa kukwepa jukumu la kubeba gharama za usafiri na mahitaji ya shuleni watakapoingia sekondari.

Anayetufungua masikio ni Mwalimu wa shule ya Msingi Chekelei, Mariam Kawambwa. Kwa mujibu wa mwalimu huyu, kukosa mwamko wa elimu kunachangia wanafunzi kukatisha masomo na hata kujifelisha kwa makusudi baada ya kupewa maelekezo za wazazi.

Kawambwa anasema katika kipindi hiki ambacho Serikali inaweka msisitizo kwenye elimu, bado kuna wazazi wanawazuia watoto wao kusoma na hilo linafanyika zaidi katika ngazi ya sekondari kwa kuwa wanawashawishi watoto kufanya vibaya kwenye mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.

Anaeleza kuwa kinachofanyika ni mzazi kumtishia mtoto kuwa akifaulu hatahusika kwa namna yoyote ile kugharamia kumsomesha, huku kukiwa na ahadi ya kupelekwa mjini kwa ajili ya kufanya kazi itakayomwezesha kupata fedha kwa haraka.

Mwalimu huyo anasema kazi za ndani ndiyo zinaonekena kupewa kipaumbele na wazazi, hivyo kwao ni heri kumtoa mtoto shuleni na kumpeleka mjini akafanye kazi.

“Wazazi wanakwepa kusomesha watoto, hivyo wanawaambia watoto wasifaulu. Wakati mwingine hili linasababishwa na umbali, utakuta ilipo shule ya sekondari ya kata ni mbali na kijiji anachoishi mtoto hivyo mzazi akiwaza gharama ya kuhakikisha mtoto anafika shuleni na kula mchana anaona ni heri asiende.

“Sasa ili asiende anamuandaa pale anapofanya mtihani darasa la saba kwa kumwambia usifaulu, hapa inategemea na mtoto mwenyewe lakini kama tunavyojua watoto mara nyingi wanawasikiliza wazazi wao labda itokee awe na mawazo tofauti aje kutoa taarifa,”anasema.

Hali hiyo inawasababisha walimu wa shule za msingi kutenga muda wa kuzungumza na wanafunzi kuwasihi wasisikilize maelekezo hayo ya wazazi huku wakilazimika kuwapa ahadi za kuwasomesha.

Anasema:, “Wakati mwingine inabidi utumie njia za ushawishi hata kumwambia mtoto kwamba utamsomesha, unajikuta ukilazimika kufanya hivi kwa sababu mtoto ashawishike kufanya vizuri kwenye mtihani. Unamwambia wewe faulu kama wazazi wako hawatakusomesha mimi nitakusomesha. Najua fika mtoto akishafaulu mzazi wake atawajibika tu kumsomesha.’’

Anaongeza: “Pia shuleni kwetu kila Ijumaa tuna utaratibu wa kuzungumza na watoto, mwalimu anazungumza na wanafunzi wa darasa lake kujua changamoto walizonazo kupitia hili tunabaini kama kuna wanaopata changamoto hata nyumbani ndipo hapo unakuta mtoto anakwambia nimeambiwa nifeli.’’
 

Uongozi

Ofisa elimu wa kata ya Chekelei, Zuwena Mshana anasema: “Wazazi wa aina hii wapo na hata mwaka huu tulipata taarifa za watoto watatu wameambiwa na wazazi wao wafeli. Tuliwaita wazazi tukazungumza nao watoto pia tukawapa hamasa na bahati nzuri wakafanya vizuri tu kwenye mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.’’

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Halfan Magani anakiri tatizo hilo lipo kwa wanafunzi wa shule za msingi kushawishiwa kufeli, lakini kupitia maofisa elimu kata, ufuatiliaji wa kina umekuwa ukifanyika.
“Ni kweli kabisa changamoto hii ipo sana huko vijijini, kama unavyofahamu elimu kwa sasa ni bure lakini mzazi anaona hawezi kuwajibika hata kumnunulia mtoto wake sare za shule na madaftari, hivyo anaona ni heri aachane na hayo mambo ya kusoma afanye vitu vingine.

“Tumekuwa tukifanya ufuatiliaji kuanzia kwa maofisa elimu kata na hata walimu kwa kuwa hawa ndiyo wapo karibu na wanafunzi wanaweza kuzungumza nao na kujua kama mazingira ya aina hiyo yapo.Kama mtoto anaeleza ameambiwa na mzazi wake afeli, basi tunashughulika na huyo mzazi hivyo tumekuwa tukilitatua kwa njia hiyo.
 

Hali ilivyo shuleni

Katika shule kadhaa zilizotembelewa, ilibainika kuwapo kwa wanafunzi wanaoacha shule. Kwa mfano, katika Shule ya Sekondari ya Mlungui, wanafunzi 27 walioripoti kidato cha kwanza mwaka huu wameacha shule.

Mkuu wa shule hiyo Halila Mkanda anasema mwaka huu wa masomo kidato cha kwanza waliochaguliwa kujiunga na sekondari hiyo ni 119, walioripoti 117 ila hadi Mwananchi lilipofika hapo, kulikuwa na wanafunzi 90.

“Tuna wanafunzi wengi wa kidato cha kwanza wanaoacha shule ukifuatilia hupati sababu zinazoeleweka kwa hiyo tunachofanya ni kuwasilisha taarifa kwa uongozi wa kata na vijiji ndiyo wanashughulika kuwafuatilia wazazi wa watoto husika lakini wengi huwa wanaondoka kwenda kutafuta ajira katika maeneo mengine,” anasema Halila.

Mtendaji wa kijiji cha Nguru kilichopo kata ya Mlungui, Swahib Magembe naye anatupa lawama zake kwa wazazi kuchangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kuacha shule kwa kuvumilia vitendo vya utoro.

“Sisi kama Serikali ya kijiji tunafanya ufuatiliaji baada ya kupokea taarifa kutoka shuleni, mwalimu akitueleza kwamba kuna watoto watoro ndiyo tunafuatlia kwenye nyumba zao lakini hata hivyo sisi nao ni binadamu. Unaweza kumfuatilia akakufanyia mambo ya Kiswahili na hilo limeshatukuta tulimfuatilia baba mmoja kuhusu mtoto wake kutoka pale macho yanatoa machozi kutwa nzima kwa hiyo tunafanya ufuatiliaji ila taratibu,” anasema Magembe.

Mwenyekiti wa kijiji cha Madumu Cassian Joseph anasema kuna baadhi ya wazazi wanafurahia watoto wao kufeli kwa kile alichoeleza kushindwa kugharamia mahitaji ya kwenda sekondari.
 

Wadau wanasemaje?

Meneja uhusiano, mawasiliano na uchechemuzi wa shirika la Uwezo Tanzania, Greyson Mgoi anasema wazazi ndiyo wanapaswa kuwa kipaumbele kuhakikisha watoto wanapata elimu, hivyo inapotokea wanafanya kinyume na hilo ni ngumu kutengeneza kizazi kinachofahamu umuhimu wa elimu.

Mgoi anasema inapotokea hali hiyo ni wazi kuwa hata wazazi wenyewe hawafahamu umuhimu wa elimu hivyo kuna haja ya kuanza kufundishwa umuhimu wake ili wajione wana wajibu wa kuhakikisha watoto wao wanasoma.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) Ochola, Wayoga anasema inawezekana elimu inayotolewa haikidhi matarajio ya wengi, lakini hilo halibadili ukweli kwamba elimu hiyo ni muhimu na ina thamani kubwa katika kupunguza mnyororo wa umaskini.

“Inawezekana elimu inayotolewa haikidhi matarajio ya watu kwa maana ya kuwa na matokeo ya haraka, yaani mtu anafikiria mtoto wake akimaliza shule apate ajira, ikitokea mambo yakawa kinyume basi haoni umuhimu wa elimu. Ukweli ni kwamba hata hiyo inayoonekana kuwa haina thamani ni muhimu kuipata kwa kuwa ina msaada mkubwa katika maisha ya kila siku,’’ anasema.