HEKAYA ZA MLEVI: Kweli dunia tambara gumu!
Kuna ajuza mmoja aliishangaza jamii baada ya kugoma kufa. Hakuna mtu aliyekuwa na kumbukumbu ya msimu (acha mwaka) wa kuzaliwa kwake. Walianza kufa wakubwa wake, wakaja shoga zake, watoto, wajukuu mpaka vitukuu lakini kibibi kikawa kinadunda tu.
Maneno yakazagaa kuwa kibibi ni ajuza. Lakini walioathirika na maneno hayo walikuwa ni vitukuu, vilembwe na vining’ina vilivyomhusu. Kenyewe kaliposikia kalijibu “Semeni, mkichoka mtalala” na “Jishembendueni tu, maneno hamyanunulii bando”.
Halafu kalikuwa kanajipenda kwelikweli. Pamoja na kuondokewa na zaidi ya dazani ya meno, mswaki haukumtoka kinywani. Kalikuwa kanakula mboga saba tena za nyodo; kuku wa kupaka, mlenda wa Mahenge (si wa bamia), mchicha bwaksi, tembele kiuno, ngogwe za Korogwe na mbilimbi za Kilwa.
Alasiri baada ya mlo kalioga na kuvalia moja ya magauni yake ya vitenge, kakajipodoa swadakta na kujipulizia uturi wa mvita. Kalitandika jamvi chini ya mwembe mbele ya nyumba na kufungulia nyimbo za mwambao kwenye redio kaseti. Hapo utawasikia Sitti binti Saad, Malika, Juma Bhalo na wengineo.
Ilifikia wakati hata vilembwe nao walimchoka maana waliona maisha yaleyale kila kukicha. Japo kabibi kalipokea kodi ya mashamba na majumba kaliyorithi kwa waume zake, kenyewe kaliishi uswazi kwenye nyumba nadhifu ya udongo. Humo ndimo kalimowalea na kulelewa na vilembwe na vining’ina.
Kalibebeshwa majina yasiyo na idadi. Wengi walimwita “Kibibi Gula” kwa jinsi alivyokuwa mkavu na mwenye nguvu kama binti wa miaka ishirini. Lakini pia walimhusisha na nguvu za giza, wakasema ati uhai wake kauchimbia kwenye mti fulani (nimeusahau) ambao hata ukikauka unaendelea kuishi.
Wakiwa na lengo la kugawana mali zake ili waende kuishi maisha ya kisasa, walikaletea wafukuza mapepo na mizimu lakini hawakufua dafu. Wakawaleta walozi wanaosemekana kuweza kumfisha binadamu kwa kupuliza ujani hata hivyo baada ya kupuliziwa bibi akaagiza soda baridi ya kushushia ugali wake. Wakajiuliza: “Au huyu ndiye shetani mwenyewe?”
Sijui hivi sasa kama yu hai au la maana mara ya mwisho nilipata habari zake miaka kadhaa iliyopita.
Kama kuna kilichoumbwa halafu kikapigania maisha na kuahirisha mauti yake, kitu hicho ni dunia. Iliumbwa tangu enzi na enzi ikiwa na kila aina ya uzuri, urembo, utanashati na uchangamfu. Wahenga waliikuta na kutuachia, nasi tutawaachia wajao watakaowaachia watakaofuata. Yenyewe inaendelea kudunda.
Inaendelea kudunda katikati ya misukosuko kutoka kwa watu wake zaidi ya ilivyokuwa kwa “Kibibi Gula”. Binadamu anahusika na karibu kila aina ya majanga duniani.
Tunasema magharika na matetemeko ya ardhi ni sehemu ya maisha ya dunia. Lakini pamoja na ajali kutokuwa na kinga, usalama barabarani ni namna moja ya kupunguza ajali. Unategemea nini kwa dunia unayoilipua kwa nyuklia, kutoboa hewa ya ozone na kuitia mashimo kwa kasi ya ajabu kila kukicha?
Watu hudhani kuwa uharibifu wa mazingira huathiri rutuba tu. Kumbe madhara yake ni uuaji wa dunia na vyote inavyovibeba vikiwemo viumbe hai. Miti kama kinga ya ardhi huzuia maafa yanayoanza na upepo mkali, mmomonyoko wa udongo, mafuriko, ongezeko la chumvi na hewa chafu duniani na mengi mengineyo.
Likitokea janga moja tu kati ya mengi yaliyoandaliwa, watu wanakesha kwenye nyumba za ibada kumlalamikia Mungu. Kesho mwendo ni ule ule. Na matangazo meeeengi ya “kujifunza mabadiliko ya hali ya nchi”! Ama kweli ndio maana ilinenwa “Watu wangu huangamia kwa kukosa maarifa”.
Haikutegemewa kama binadamu wa sasa anaweza kuifikisha dunia ilipofika kwa muda mfupi kama ilivyotokea. Miti huko California imethibitika kuwa na umri wa zaidi ya miaka 4,800. Na watafiti wameugundua mti wenye umri wa miaka 9,000 huko Canada.
Mimi nadhani utafiti huo ungefika Afrika ungevumbua miti yenye umri mkubwa zaidi. Lakini pamoja na hayo mtu bila hata chembe ya woga wa umri wala umuhimu wake, anakwenda kuudondosha kwa tamaa ya gunia chache tu za mkaa. Kweli watu hawaogopi laana.
Ebu fikiria hapa Tanzania pekee tunakata karibu eka laki moja na sitini elfu za miti kila mwaka kwa ajili ya mkaa (achana na mbao, nyumba na kuni na bakora)! Tupo bega kwa bega kukamilisha idadi ya zaidi ya miti bilioni 15 na nusu inayokatwa kila mwaka duniani. Kwani tunashindana au tunakomoana?
Wenyewe tulizoea kuona wanyama wadogo, ndege na wadudu wakicheza mpaka kando kando ya majiji, lakini hivi sasa wameshatoweka. Hamna cha tongwa wala kisiesie. Tetere, shorwe bwenzi, shorwe wanda na mbayuwayu wamebakiza hadithi zao tu.
Zamani ndege hawa walijenga kwenye miti. Lakini kwa jinsi miti ilivyokatwa hovyo, wakaona wasingeweza kuendelea kuhatarisha uhai wao, watoto na mayai yao, wakajenga kwenye nyumba za watu. Lakini walipoiona dunia jinsi inavyoangamia wamekimbia jumla!
Hivi sasa tuna nishati mbadala za kutosha, iliyo karibu na rahisi zaidi ni gesi. Inasemekana gharama ya matumizi ya mkaa inazidi ile ya gesi. Hata gharama ya mirunda na miti ya kujengea ipo juu zaidi ya sementi. Ni kitu gani kinachozuia mabadiliko?