Hii ndio faida ya kunywa mtindi

Friday January 01 2021
mtindi pic
By Mwandishi Wetu

Unywaji wa maziwa mtindi husaidia kuboresha afya ya mwili na kupandisha kiwango cha lehemu nzuri mwilini.

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Sayansi ya Chakula ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk Elifatio Towo anavitaja virutubishi vilivyomo kwenye maziwa kuwa ni utomwili, kabohaidreti, mafuta , madini na vitamini.

Dk Towo anasema maziwa ni mojawapo ya vyakula vichache ambavyo ni mlo kamili na hiyo ni kwa sababu ya ubora wake wa virutubishi vilivyomo.

Anasema maziwa yaliyochachushwa (mtindi) yanakuwa yameongezewa bakteria wazuri.

“Bakteria hawa wanasaidia kubadilisha sukari iliyoko kwenye maziwa halisi kuwa kwenye hali ya uchachu (asidi),” anasema Dk Towo.

Mtaalamu huyo anasema maziwa yaliyochachushwa ni miongoni mwa vyakula bora na muhimu katika afya ya binadamu kwa sababu ya kuwa na virutubishi vingi ambavyo vina faida katika mwili wa binadamu.

Advertisement

Anasema mtindi pia una vitamini ‘Riboflavin (vitamin B2), na ‘vitamin B12.

Dk Towo anasema wakati wa uchachushaji kuna vichocheo vingine vinavyojulikana kama antioksidants, hivi vinavyokinga mwili dhidi ya magonjwa ya kuharisha na aina mbalimbali za saratani.

Maziwa hawa yana faidia nyingi kama kuimarisha kinga mwili kwa kuwa tafiti zinaonyesha utumiaji wa mtindi mara kwa mara unaongeza uwezo wa mwili kupambana na magonjwa ya saratani, vidonda vya tumbo na vidonda katika sehemu mbalimbali za mwili.

Pia, husaidia ukuaji wa misuli na kurudisha ute ulipotea kwenye maungo ya magoti na viwiko kutokana na kiasi cha protini kinachopatikana katika maziwa yaliyochachushwa.

Hata hivyo, anasisitiza mtindi uliobora ni ule ulioandaliwa katika mazingira safi na salama.

Advertisement