Jafarai yuko zake bize kuosha ndinga

Wimbo wa ‘Niko Busy’ ndio ulimtambulisha Jafarai kwenye ramani ya muziki, ilikuwa ngoma yake ya kwanza kuifanya nje ya kundi la Wateule, Jafar Ally, miongoni mwa mastaa wa zamani wa Hiphop aliyejikita kuosha magari.
"Naosha mwenyewe, ukinikuta niko bize hapa kazini kwangu huwezi amini, napiga kazi kwelikweli," anaanza kueleza staa huyo wa muziki ambaye kwa muda mrefu amekuwa nje ya jukwaa.

Alianza hivi kuosha magari

"Huwa nafanya kazi mwenyewe, kuna muda nakuwa bize hadi kuosha magari mwenyewe, ingawa wakati mwingine nawaelekeza vijana wangu mimi nakuwa nasimamia," anasema.

Jafarai ambaye pia ana uzoefu kwenye ufundi magari anasema mbali na kuosha, pia wanatengeneza magari.

"Hata kama sitoshika spana, lakini nitaelekeza fanya hiki, fungua hiki hata na kile, nafanya vitu vingi nimebobea pia kwenye usafi wa majumbani, ukinikuta kazini, sio Jafarai yule wa studio.

"Na utaalamu wa kuchanganya dawa za usafi, mfano tunaposafisha makochi, yana utaratibu wake na dawa zake za kusafishia hivyo tukipata kazi, lazima niwepo kuwaelekeza vijana," anasema.
Anasema aliingia kwenye kazi hiyo baada ya kupata changamoto kuosha na kulifanyia matengenezo gari lake.

"Mimi ni mmoja wasanii wa mwanzo kuwa na gari, wakati ule wasanii wachache sana wana magari, nilikuwa napata taabu kusafisha na kulifanyia service, ilikuwa ni kazi ya siku nzima, nikasema kwa nini nisiwe nafanya mwenyewe? hapo ndipo safari yangu ya magari ilipoanzia.
Anasema, hakuwa na pesa nyingi wakati anajikita kwenye kazi hiyo, lakini kelele nyingi ndizo zilimbeba.

"Hata mashine moja sikuwa nayo, watu walihisi nimewekeza kwelikweli, lakini siri nilikuwa naifahamu mwenyewe, nilianza kwa kukodi mashine, hii ikanifunza kwamba katika biashara sio lazima uwe na kila kitu ndipo uanze,"anasema.
Kuosha magari kulivyomlipa

Jafarai anasema kwenye kukodi mashine kulikuwa lazima ulipe kwa siku, haijalishi umefanya biashara au vinginevyo yeye anachokitaka ni pesa mliyokubaliana.

"Kuna muda pia akiona umefanya sana kazi anachukia akiamini umetumia kupita kiasi mashine zake, hiyo ndiyo ilikuwa changamoto, lakini nilikodisha kwa mwezi mmoja nikanunua zangu, mbili moja ikiuzwa Sh 2 milioni na nyingine Sh1 milioni,"anasema.

Anasema tangu kuanza kwa kibarua hicho, vijana zaidi ya 50 wamepitia na wengine kufanikiwa kimaisha kwa kuosha magari.

"Nilikuwa nawaambia wadogo zangu hili ni daraja sitaki mkae hapa, kwamba ndiyo mmemaliza, hapana tumieni hapa kujitafutia riziki na kutafuta fursa nyingine.

"Kutokana na kufahamika kwangu kwenye muziki, wengi niliwakutanisha na watu wengine na wamefanikiwa, wapo ambao leo hii ni madereva kwenye kampuni kubwa, wameoa, wana familia zao na maisha mazuri, lakini tulikuwa tukiosha nao magari hapa. "Nimewasaidia kuwaunganisha watu wengi, wapo wanaorudi kushukuru na huko walipokwenda wananipa heshima ya hali ya juu, sikuwasaidia pesa lakini nimewaonyesha njia za maisha," anasema.
 

Changamoto ya kuosha magari hiko hivi
 

Jafarai ambaye sasa anewaajiri vijana watano akishirikiana kwenye kazi hiyi anasema kila kazi ina changamoto zake, ikiwamo yao ambayo wakati mwingine analazimika kulipa kitu ili kumridhisha mteja.

"Unaweza kumuoshea gari mtu, kumbe hajapenda au mkorofi tu hata kama yeye ndiye amekosea, lakini inabidi mimi kujishusha na kujifanya mjinga na kuomba samahani, watu hawapendi ujitete.

"Kuna mwingine atadai kaibiwa perfume yake ya Sh2 milioni kwenye gari, kumbe hakuja nayo alipoleta gari kuoshwa, hivyo tunajishusha na kumshauri ajaribu kuangalia nyumbani wakati huo na sisi tunamuangalizia, baadaye anapiga simu anakiri kuiacha nyumbani, kuna vitu vingi ambavyo usipokubali kujishusha kazi haziendi,"anasema Jafarai.
Anasema kuna muda inatokea ajali, gari inaharibika analazimika kulipa.

"Siku hazifanani, kuna kijana wangu mmoja siku moja alikuwa tu na mawenge, akagonga nguzo na kupasua kioo cha gari ya watu, ikabidi nilipe,".
Kwenye muziki iko hivi
Licha ya kutosikika muda mrefu, Jafarai anasema hawezi kuacha muziki maisha yake yote.

"Muziki ni kazi ambayo haina kustaafu, pia kila mwanamuziki ana wivu, ukisikia mwenzako katoa ngoma kali unaitamani iwe yako, hiki ndicho kinasababisha tusiache, lakini ni bora ukae kimya muda mrefu ili ukirudi unakuja na kitu kikubwa

"Kuandika nyimbo hakuhitaji mawazo, eti uwe na njaa hauna hela ya kula, halafu ukae uandike nyimbo, huwezi," anasema.
Anasema wakati anaanza kuimba, wanamuziki wengi waliingia kwenye fani kwa mapenzi.

"Kipindi kile hatukuwa tunawaza muziki utupe pesa wala utufanye kuwa mastaa, tulifanya sababu tu tulipenda. "Nimeanza wakati niko sekondari Al-Haramain, kulikuwa na ushindani wa shule kwa shule kama Jitegemee, Jangwani na Azania .
 

Amkimbia Mdosi, asepa na pesa za shoo
 

Akiwa mwanafunzi wa kidato cha tano, Jafarai anasema alijiandalia shoo mwenyewe shuleni.

"Wakati ule kuna ushindani kwelikweli, nakumbuka tiketi zote ziliuzwa wiki mbili kabla ya shoo, mashabiki walikuwa wanafunzi, walimu na hawakuwa wakiufahamu huo mchongo. "Wanafunzi walipania, wanatambiana wakisubiri siku ifike tukiwashe, ilikuwa ni mimi na kundi langu, Jay Mo na mshikaji mwingine yeye hakuwa anasoma, lakini mtaani marapa tulikuwa tunajuana na kualikana kuja kuonyeshana uwezo wa kuchana.

"Tulikuwa tunafurahia michano, hatukuhitaji pesa kabisa, lakini ile shoo baada ya tiketi kuuzwa na kuisha wiki mbili kabla, nikapata Sh700,000.

"Ilikuwa ni pesa nyingi sana wakati ule, nimekaa nayo ndani bila kuigusa hadi siku shoo, ilifanyika Las Vegas, tulikubaliana na Mdosi anipe ukumbi kisha tutagawana mapato nusu kwa nusu.

Anasema shoo iliisha saa 8 mchana, lakini alifanya tukio la ajabu ambalo huwa analijutia hadi leo.

"Nilijiuliza kweli nimpe Sh350,000! Nikajiambia hata haiwezekani, nikakimbia nazo, huku nikijidanganya Mdosi atakuwa kazisahau maana nilikaa nazo nyumbani wiki mbili baada ya tiketi kuisha.

"Nilivyotokomea nazo, ile kufika tu nyumbani nasikilizia nini kitatokea, nikasikia mabaunsa wanagonga geti, nikaona huu msala, nikawaambia ndugu zangu wasilifungue hadi asubuhi.
Anasema wakati huo alikuwa na miaka 17, hakuwa amewahi kupata pesa nyingi namna ile.

"Ilienda yule Mdosi akanipotezea, hata hivyo kwa akili ya shule ile pesa niliitumia kula chipsi kuku sana hadi ikaisha, lakini hili ni tukio langu baya ambalo nililifanya bila kutegemea na huwa nalijutia hadi leo,"anasema.
Anasema shuleni kufanya muziki haikumletea shida kwani hata walimu waliwasapoti na kuna vipindi walishindana kurap darasa kwa darasa au shule kwa shule.

"Wakati ule kuna makundi, walimu waliruhusu na binafsi ukiacha kwenye shule niliyosoma, nimewahi pia kufanya kwenye bwalo la shule za Azania na Jitegemee na walimu walisapoti,".
Naziz amrahisishia njia
Licha ya kwamba wakati ule familia nyingi ziliamini muziki ni uhuni, Jafarai anasema walifanya kazi ya ziada kuzishawishi familia zao kuondoa fikra hizo.
 

"Tulitunga mashairi ya kuelimisha, ambayo hata walipotusikiliza waliona tunafundisha zaidi ya kuburudisha, watu wazima walisikiliza hata wazazi waliona tunaongea vitu vikubwa, kiasi fulani ikatusaidia.

"Ilibidi tuwashawishi ili watuelewe, ingawa upande wangu ilinipa unafuu kupitia dada yangu Naziz, ambaye tayari alikuwa ameingia kwenye muziki,".

Naziz alikuwa Kenya, ambako Jafarai anasema baba yake alikwenda huko kitambo, hivyo dada yake huyo alikulia na kulelewa nchini humo.

"Naziz ni mtoto wa mjomba wangu, familia yao ilihamia kule japo kila mmoja alianza muziki kivyake, nilikuwa nikienda Nairobi namkuta anachana.

"Tukawa tunashindana kinyumbani, ndugu wengine wanatushangilia, naye akawa akija Dar es Salaam tunaenda studio wazazi wetu wanatusapoti pesa za kurekodi," anasema.


Alivyokutana na Mox, Jay Mo

Jafarai ni mmoja wa nyota waliounda kundi la Wateile sanjari na Mchizi Mox na Jay Mo ambao anasema walikuwa mtaani pamoja wakichana.

"Iliandaliwa talent shoo, tukaenda kushiriki kama kundi, tukashinda na kupata fursa ya kurekodi bure, hapo ndipo tulianza kujulikana kote nchini,"anasema.
Tofauti na wasanii wengi kupita njia ngumu hadi kutoboa, Jafarai anasema kundi lao haliku-haso.

"Tumepita njia rahisi sana kutoka, tuliposhinda talent shoo, tukapata nafasi ya kurekodi kwa Master Jay, lakini pia tulikuwa watoto wa mjini, tulijulikana hadi makondakta, hivyo hata daladala tulipanda bure.

"Mtaani tulionekana tofauti tangu wadogo, wakati huo tukiishi Makumbusho, masikani yetu ilikuwa Brevia, Kijitonyama, miaka ya 2001, tulii-brand, tulipoondoka ndio ikapoa," anasema Jafarai ambaye wimbo wake wa kwanza kufanya nje ya kundi la Wateule ilikuwa ni ‘Niko busy’.

Anasema katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru, wimbo wake huo ulichukuliwa kuwa ni miongoni mwa nyimbo 10 bora, ambao ulimpa heshima. "Hili ni miongoni mwa matukio mengi mazuri niliyokutana nayo kwenye muziki," anasema mwanamuziki huyo na baba wa binti wa miaka sita.
"Sitaki binti yangu apite njia zangu, yeye atakwenda na zake atakazotaka lakini nitamsapoti,".


Soka ndiyo ilikuwa mpango mzima

Jafarai licha ya kufahamika kupitia muziki anasema ndoto yake kubwa ilikuwa kwenye soka.

"Sikuwahi kuwaza muziki, nilipenda mpira wa miguu, lakini pia kwetu tuna asili ya Kihindi, na Wahindi wengi ni wafanyabiashara, nilijua nitakuwa huko.

"Kwenye soka ndoto hazikutimia, lakini kwenye biashara sitaishia hapa, pia kabla mwaka haujakwisha lazima nifanye kitu kwenye muziki. "Nitakuwa natimiza miaka 20 ya ‘Niko busy’, kuna kitu nakiandaa ili nirudi kivingine kwenye muziki," anasema.