Chanzo, hatari ya wanafamilia kuchukiana
Katika jamii zetu, familia imeendelea kuwa nguzo muhimu ya malezi, upendo, na mshikamano. Hata hivyo, kumekuwa na ongezeko la visa vya familia kuvunjika kutokana na kutokuelewana, chuki zilizokomaa, na ukosefu wa mawasiliano kati ya wazazi na watoto au kati ya ndugu wa tumbo moja.
Migogoro hii ina athari kubwa na imeendelea kuleta kwa baadhi ya familia kiasi cha kufikia hatua ya kushindwa hata kuzikana.
Hali hii inazua maswali mengi na wengine hujiuliza chanzo cha mfarakano huo ni nini na je! kuna mbinu ya kurejesha umoja na upendo ndani ya familia?
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, watu walio kwenye mitafaruku na ndugu zao wanasema migogoro ya familia hutokana na mambo mbalimbali, lakini mingi chanzo chake ni masuala ya urithi, chuki za zamani, kipato, kashfa za uchawi na tofauti za kimtazamo. Kwa maana hiyo, kila mmoja anapoanza kuona ana haki kuliko mwingine, mfarakano unaanza kuchipuka.
Masuala ya urithi ni miongoni mwa chanzo kikubwa cha migogoro mingi. Wazazi wanapofariki dunia, watoto huanza kugombania mali, na kama hakuna maandishi yaliyoachwa na wazazi, hapo ndipo uhasama husimama kati.
Mwandishi alitembelea maeneo kadhaa na kukutana na watu waliothirika moja kwa moja na migogoro ya kifamilia na hizi ni baadhi yasimulizi za kweli zinazoakisi hali halisi ya familia nyingi nchini.
Mzee Hamisi (siyo jina lake halisi) ni mkazi wa kijiji kimoja mkoani Morogoro, anasema aliacha kuzungumza na watoto wake baada ya kutofautiana kuhusu ugawaji wa ardhi ya urithi.
“Nilipoamua kugawa ardhi yangu, watoto wangu wa kiume walipinga sana, wakisema si haki mimi kugawa mali nilizopata kwa jasho langu. Hapo ndipo tulipokosana na hadi leo hawazungumzi na mimi,” anasema Hamisi kwa huzuni.
Anasema tangu wakati huo, hakuwahi kusemeshana nao wala kusalimiana nao. “Wanapokuja kijijini wanaingia moja kwa moja kwenye nyumba zao bila hata kupita kwangu. Inaniumiza sana kuona tumefikia hali hii,” anasema.
Naye msanii wa maigizo nchini, Chausiku Salum maarufu ‘Bi Chau’ anasema ana miaka 20 hazungumzi na mtoto wake wa kumzaa licha ya kuwatuma watu kujua sababu ya mtoto huyo kutokuwa na ukaribu na mama yake.
“Katika kutafuta suluhisho la tatizo, nilijaribu kuita wazee wamkanye mwanangu ajirekebishe ili awe karibu na mimi lakini hataki, nikajaribu kutoa hadi sadaka msikitini hata kushirikisha mashehe na masharifu, maana nimemtumia hadi jirani yangu kwa kumpa sadaka ya Sh10,000 ili wamuombee lakini imeshindikana,” anasema Bi Chau.
Anasema amejaribu kutumia njia zote ili kumuangukia mwanawe huku akimsihi kama kuna mahali alimkosea bila kujua, bado hajafanikiwa.
Mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam, Mariam Juma ambaye ni mama wa watoto wanne na dada yake wa tumbo moja, hawazungumza kwa zaidi ya miaka 15 sasa baada ya kuuza nyumba waliyoachiwa na wazazi wao.
“Tuligombana kwa sababu shemeji yangu aliyemshawishi mdogo wangu tuuze nyumba tuliyoachiwa na wazazi wetu, hata nilipomsihi asifanye hivyo hakunielewa,” anasema Mariam.
Anasema sababu hiyo ilileta mtafaruku mkubwa katika familia yao na ukizingatia katika tumbo lao walizaliwa wawili tu na sasa hakuna mtu anayeshiriki katika jambo lolote la mwenzie, liwe la huzuni au furaha, kwa sababu walishapelekana mpaka mahakamani kwa sababu ya mali.
Mariam anasema kuna wakati anaona mahali walipofikia si pazuri, lakini hana la kufanya kwa sababu kila mmoja ana mambo aliyoyapitia na hakuna aliyeshiriki si msiba wala furaha huku mmoja akifiwa na mume na mwingine na mjukuu.
"Ndugu ni nguzo muhimu katika maisha, lakini sasa najiona mpweke. Ni ngumu sana kuishi bila mawasiliano na mdogo wangu wa tumbo moja, sina la kufanya kwa sababu bado kuna watu wanaendelea kuchochea ugomvi wetu," anasema huku machozi yakimtoka.
Simulizi ya John Muro mkazi wa Arusha inafanana na ya Mariam ambaye hana mawasiliano kabisa na ndugu zake wa tumbo moja huku yeye akisema wanatuhumiana hata mambo ya ushirikina.
"Tuligombana kwa sababu ya mirathi baada ya wazazi wetu kufariki dunia, kila mmoja alikuwa akivutia upande wake, tulishindwa kuelewana na kuanzisha utaratibu wa kwenda kwa waganga wa kienyeji ili kumaliza mzizi wa mifarakano kwa yeyote anayesumbua, kwa sasa kila mmoja anaishi maisha yake, hatuzungumzi na hata hatuzikani," anasema John.
Lakini anakiri kuwa hali hiyo imesababisha maumivu mengi. "Nilipofiwa na mke wangu, hakuna ndugu hata mmoja aliyejitokeza kumzika. Ilikuwa ni aibu kubwa kwa familia yetu," anasema John.
Wakilizungumzia hilo, baadhi ya viongozi wa dini wanasisitiza umuhimu wa amani na upendo ndani ya familia, wakionya juu ya athari mbaya za mifarakano kati ya wazazi na watoto.
Wanasema migogoro ya kifamilia inaweza kusababisha majeraha ya kihisia kwa watoto, ambayo yanaweza kuathiri maendeleo yao ya kijamii na kiroho.
Viongozi hao wanakemea tabia za ukosefu wa heshima na uvumilivu kati ya wazazi na watoto, wakisisitiza kwamba familia inapaswa kuwa ngome ya kwanza ya maadili na uadilifu.
Wanaonya kwamba mifarakano inaharibu umoja wa familia na inaweza kusababisha watoto kukosa mwelekeo katika maisha yao na hata kupoteza imani.
Mchungaji wa Kanisa la Wokovu lililoko Mbagala, jijini Dar es Salaam, Daniel Zephania anasema, familia ni zawadi kutoka kwa Mungu.
Hivyo, anasema ni jukumu la wazazi kuhakikisha wanadumisha upendo na amani ndani ya familia. “Hatuwezi kuhubiri amani na upatanisho kwa jamii ilhali sisi wenyewe ndani ya familia zetu tunatofautiana na kukosana,” anasema mchungaji huyo.
Anasema wazazi wanatakiwa kuwasikiliza watoto wao kwa upendo na kuelewa changamoto wanazokabiliana nazo.
Kwa upande mwingine, anasema watoto wanahimizwa kuwa na heshima na utii kwa wazazi wao, kama ilivyoamriwa katika maandiko matakatifu.
Anasema kwa sababu hiyo, viongozi wa dini wanaamini kuwa suluhu ya migogoro ndani ya familia inaweza kupatikana kwa njia ya mazungumzo, sala na kujitolea kwa ajili ya ustawi wa kila mmoja ili kudumisha upendo, amani na umoja ndani ya familia.
Naye, Shehe wa Msikiti wa Manzese, Abdulrahman Rashid anasema; "Uislamu unatufundisha umuhimu wa kusameheana na kuishi kwa amani. Kutoongea na ndugu ni dhambi na ni wajibu wa kila Muislamu kutengeneza mahusiano mazuri na familia yake. Tunapaswa kuacha ubinafsi na chuki, na kuwekeza katika upendo na uhusiano wa familia."
Mwanasaikolojia afunguka
Akilizungumzia hilo, Mwanasaikolojia Ramadhani Massenga anasema chanzo cha yote hayo kimetokana na kukosekana kwa neno upendo.
Anasema na huo mara zote huanzia kwenye malezi tangu mtoto akiwa mdogo kwa sababu anajifunza kutoka katika familia.
“Kuna vitu vinaanzishwa na familia na vinajengwa katika akili ya mtoto na anakuwa nayo, kama hakuna upendo katika nyumba ni ngumu kwa mtoto huyo kukuwa na kuendelea nao,” anasema Massenga.
Anasema watu wengi wana manung’uniko, hivyo, inapotokea jambo lolote linalojitokeza wazi, mtu huyo hutoa hisia zake zote, na hivyo kusababisha chuki ya wazi kutoka kwa wazazi au ndugu wanaoishi nao.
“Kabla ya kukimbilia suluhisho, ni muhimu kujua chanzo cha tatizo kwani unaweza kuponya jeraha kwa juu, lakini ndani bado kuna ubichi. Ili kuweka usawa, wale wanaoitwa kwenye mabaraza au vikao wanapaswa kufahamu kiini cha tatizo ndipo watoe suluhisho,” anasema
Tofauti za kimtazamo, kama vile kuhusu ndoa, elimu, au jinsi ya kuendesha familia, zimechangia pia kuvunjika kwa mahusiano ya kifamilia.
Athari kwa jamii
Samwel Maliki (75) anasema migogoro ya kifamilia ina athari kubwa kwa jamii nzima na husababisha upweke na huzuni kwa wahusika, ambao mara nyingi huathirika kisaikolojia.
“Watu wanaweza kukosa msaada wa kijamii wakati wa shida kutokana na kuvunjika kwa mahusiano. Pia, inapunguza mshikamano wa kijamii kwani familia zilizovunjika haziwezi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii kama kawaida,” anasema Maliki.
Anasema migogoro hiyo pia inaathiri malezi ya watoto, kwa sababu wanaweza kukosa mfano mzuri wa kuiga kutoka kwa wazazi wao na kuna hatari ya kurithi tabia hiyo na kuja kuieneza kwa vizazi vijavyo.
Je! suluhisho ni lipi
Ili kukabiliana na tatizo hilo, Maliki anasema viongozi wa dini, wanasaikolojia na wazee wa mila wanapaswa kushirikiana kuanzisha programu za upatanisho wa kifamilia.
“Kwa mfano, vikao vya familia vinaweza kufanywa mara kwa mara ili kujadili masuala yanayoweza kuzua migogoro na kutafuta njia za kuyatatua kabla hayajawa sugu,” anasema.
Elimu pia ni muhimu
Anasema familia zinapaswa kufundishwa kuhusu umuhimu wa mawasiliano, kusameheana na kushughulikia tofauti za kimtazamo bila kuleta mgogoro.
Pia, wazazi wanapaswa kuandika urithi wao mapema na kwa uwazi ili kuepuka migogoro ya baadaye.
Maliki anahitimisha kuwa migogoro ya kifamilia ni changamoto kubwa inayoathiri jamii nzima, na ni muhimu kutambua kuwa familia ni nguzo kuu katika maisha.
Kuna haja ya kujenga familia zenye upendo, mshikamano, na amani ili vizazi vijavyo viishi katika jamii yenye mshikamano na upendo wa kweli.