Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kukosa kazi kulivyomkosesha mke James Lembeli Ujerumani

Mbunge wa zamani wa Kahama (CCM), James Lembeli katika mahojiano aliyofanya hivi karibuni na waandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi

Akiwa mfanyakazi wa Redio Berlin Internation nchini Ujerumani, James Lembeli alikutana na binti wa Kijerumani, Birgit Lifka, wawili hawa wakaanzisha urafiki uliowapeleka kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Kwa Lembeli uhusiano huo haukuwa wa kupoteza muda, aliamini kuwa mwanamke huyo ndiye atakayekuja kuwa mke wake na mama wa watoto wake kwa kuwa alishamridhia kwa shida na raha.

Wakati yeye akiwaza hivyo, mambo yalikuwa tofauti kwa Birgit, yeye alitaka uhakika wa maisha yake, hilo lilimfanya akatae kuja Tanzania kuishi na mwanamume huyo kwa kuwa hakuona hatima yake siku za usoni.

 Katika mahojiano aliyofanya na gazeti hili, Lembeli anasimulia kisa hicho akikumbuka namna umaskini ulivyomfanya amkose mrembo huyo wa Kijerumani.

Mwanasiasa huyo mkongwe, mbunge wa zamani wa jimbo la Kahama mjini, anasema kutokuwa na kazi kuliharibu ndoto hiyo, ingawa baadaye alikuja kumpata mke wa maisha yake, Hawa Mchinja.

"Ni 'binti' mrembo wa Kimasai kutoka Arusha, alibadilisha maisha yangu kabisa, nilipomchumbia ikabidi nimwambie yule wa Ujerumani kwamba sasa nataka kuoa.

"Aliniandikia barua ya kurasa tisa, kilichoandikwa mule ni siri yangu," anasimulia Lembeli, katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika Julai Mosi, jijini Dar es Salaam yakiangazia masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii.




Kisa chenyewe kilivyokuwa

Lembeli, aliyekwenda Ujerumani mwaka 1987 kufanya kazi kwenye radio Berlin International, ndipo alikutana na 'binti' huyo aliyekuwa 'girlfriend' wake.

"Tulipanga kufunga ndoa, lakini tulikubaliana iwe kwa sheria za Tanzania, yule binti alikubali, ingawa kabla hatujafanya hivyo, mkataba wangu kule Ujerumani ulikwisha na kurudi nyumbani mwaka 1992," anasema.

 Anasema, akiwa Tanzania, alirudi kufanya kazi Washirika, lakini wakiendelea kuwasiliana na yule binti, japo baada ya mwaka mmoja Washirika ikavunjwa na yeye kutokuwa na kazi.

 "Kipindi kile nilidhalilika haijawahi kutokea, ilifikia hatua nilishindwa hata kuweka mafuta ya Sh500 kwenye gari, nikaongea na yule binti wa Kijerumani akaniambia nirudi Ujerumani.

 Anasema, kulingana na maisha yalivyompiga alikubali, ikabidi aombe kurudi Radio Deutsche Welle, japo shida ilikuwa ni mtoto, alitaka aende na binti yake aliyekuwa naye hapa nchini.

 "Walikubali nirudi, nikiwa katika maandalizi ya kuondoka Tanzania, nikapata barua ya kazi Tanapa (Shirika la Hifadhi za Taifa) ambako mshahara tu ilikuwa ni Shilingi elfu 95, napewa nyumba, gari na matibabu, wakati Ujerumani mshahara ilikuwa ni Shilingi elfu 14.

 Donge nono hilo likamfanya afikirie mara mbili kuhusu kurudi kwenye nchi hiyo ambayo wakati huo ilikuwa ni kama jehanamu kwa watu weusi kutokana na ubaguzi.

 Kwa kuwa tayari alishakuwa na uhakika wa maisha baada ya kupata kazi, akamwambia Birgit aje kuishi nchini Tanzania, tofauti na alivyotarajia ombi hilo lilikataliwa.

 "Nilimuomba yeye ndiyo aje Tanzania, baada ya kupata barua ya Tanapa, alinikatalia, akaniambia hawezi kwa kuwa maisha ya Afrika hayatabiriki na mimi bado sina kazi, hivyo nikitaka mimi ndiyo nirudi Ujerumani. Niliona upuuzi, nikaachana naye.

Si kwamba ilikuwa rahisi kuachana na mwanamke huyo, lakini ilibidi afanye hivyo ili maisha yake yaendelee, kwa kuwa aliamini huenda ndoa hiyo haikupangwa na anapaswa kukubaliana na hilo.

 Miaka mitatu baadaye Lembeli alikutana na Hawa, wakaanzisha uhusiano na mwaka uliofuata wakafunga ndoa.

“Hawa nilikutana naye AICC ambako alikuwa akifanya kazi kama secretary wa bosi wa kampuni moja kubwa ya utalii hapo Arusha na mimi nikiwa Tanapa. Tangu nimekutana naye maisha yalibadilika mno kutokana na ucheshi na ukarimu alionao mwanamke huyu.

“Amekuwa mvumilivu sana kwangu, hasa katika masuala yangu ya kisiasa, amekuwa ni mtu anayenitia moyo,”

Ni takribani miaka 28 sasa tangu wawili hao wafunge ndoa iliyowawezesha kupata watoto ambao kwa pamoja waliwezesha kutengeneza familia iliyomfanya asahau kabisa kuhusu binti wa kijerumani Birgit.


Azungumzia ongezeko la talaka

Lembeli anasema kwa kiasi kikubwa tatizo hilo linachangiwa na wengi kuingia kwenye ndoa katika umri ambao hawana uzoefu.

Anasema, ndoa inahitaji ustahimilivu na uvumilivu, kama huna hivyo vitu ukatengana na mwezako unachanganyikiwa.

“Ukiingia kwenye ndoa kama akili yako haijakomaa, unabaki kuwa na tamaa, huko kwenye ndoa bado unataka michepuko, hicho ndicho kilinifanya niingie kwenye ndoa nikiwa na umri mkubwa.

“Mara nyingi chanzo ni kutovumiliana, vijana wengi sasa hawana uvumilivu na kuchukuliana kwenye shida na raha, katika maisha ya ndoa bila kuvumiliana ni ngumu kuwa na ndoa yenye furaha, amani na upendo.”


Alifikaje Ujerumani

Safari ya Lembeli kwenda Ujerumani ilikuwa ni kama bahati, japo katika maisha yake kuzaliwa, elimu hadi kuanza kazi nayo ni kama yalikuwa na bahati.

Mwanasiasa huyo aliyezaliwa Desemba 26, 1956 akiwa ni mtoto wa nane kati ya watoto 15 kwenye familia ya chief Daudi Lembeli na mkewe Maria, anasema alisoma elimu ya msingi kwa shida kutokana na mazingira ya kijijini kwao wakati ule.

“Nilikwenda kuishi kwa watu, ambako ni mbali na nyumbani, nilirudia darasa la saba mara tatu, huwa nasema kama vyeti feki vingeanzia darasa la saba basi na mimi ningekuwa kwenye kundi hilo.”

Anasema alitumia jina la mtu aliyeahirisha kujiunga sekondari kuanza kidato cha kwanza, hivyo kuitwa Mathias, hadi alipofika kidato cha pili ndipo alibadilisha jina na kutumia jina lake halisi la James.

Anasema, pamoja na pasi zake kuwa nzuri, hakuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano, kwa kuwa wakati ule ilikuwa ukihitimu kidato cha nne unajaza unataka kazi gani, yeye alijikuta tu amepangiwa Benki Kuu ya Tanzania kama Karani.