Kwa nini jeli hutumika kusukia nywele?

Muktasari:

  • Licha ya kuibuka mitindo mipya ya nywele zilizobamba na kufungia mwaka, lakini nywele aina ya yeboyebo haijawahi kupoteza mvuto wake.

Mwaka 2022 ulikuwa na mitindo mingi ya nywele, ikiwamo mipya na ya zamani.

Licha ya kuibuka mitindo mipya ya nywele zilizobamba na kufungia mwaka, lakini nywele aina ya yeboyebo haijawahi kupoteza mvuto wake.

Kumekuwa na mitindo mingi ya kuboresha usukaji wa yeboyebo, huku njia mpya ambayo imekuwa ikitumiwa sana na baadhi ya wasusi ni kusukia jeli.


Swali la kujiuliza jeli ni nini?

Kawaida jeli hujulikana zaidi kama kimiminika chenye asili ya gundi kwa sababu ya malighafi zinazotumika kutengenezea kuwa na asili ya kunata nata. Kuna aina nyingi za jeli ambazo ni jeli laini na jeli ngumu.

Katika ususi wa yeboyebo jeli inayotumika huwa ni jeli laini.

Kwa nini wanatumia jeli?

Wakati wa kusuka yeboyebo msusi huhitajika kukata mistari na ili ikae vizuri, hupaka jeli chini ya ngozi ambayo husaidia kunyoosha vizuri mstari na kuleta mng’ao katika nywele.

Pia, jeli humsaidia msusi kusuka nywele zote hata zile za mbele katika uso (malaika), hivyo huleta mng’ao katika uso na mvuto.

Mdau wa masuala ya ususi na urembo, Mwamvi Lyaunga akizungumza na Mwananchi anasema njia ya kusuka yeboyebo kwa kutumia jeli wakati wa kukata mistari ya nywele husaidia kusuka vizuri rasta na huleta mvuto katika nywele.

“Hapo awali wateja wangu nilikuwa nawasuka yeboyebo bila kutumia jeli, lakini baada ya kuzuka mitindo mingi ya nywele za rasta zinazochambuliwa na kusukia jeli nikaona kumbe naweza kutumia jeli katika yeboyebo na nilipoanza kusuka hivyo wateja wangu wamekuwa wakifurahia sana kwa sababu zinawapa mwonekano mzuri,” anasema Mwamvi.


Jinsi ya kutunza yeboyebo za jeli

Nywele ni kama mmea ambao ili uote na kukua vizuri unahitaji udongo mzuri na maji.

Hivyo, nywele za yeboyebo iliyosukwa kwa jeli ili iweze kuwa na mvuto na mng’ao lazima inyunyiziwe maji kidogo kwa mtindo wa kupulizia kama ‘spray’ kisha unapaka mafuta katika mistari na juu ya rasta.

Wakati wa kulala unapaswa uvae kofia ya nywele au kufunga kitambaa, njia hiyo husaidia kufanya nywele isifumuke, pia kutochafua mashuka kutokana na mafuta ya nywele yaliyopo kichwani.


Namna ya kufumua yeboyebo

Watu wengi hulalamika kuwa, nywele zao huwa zinakatika pindi wanaposuka yeboyebo kwa kutumia jeli, lakini tatizo huwa namna ya kuzifumua.

Sababu inayochangia nywele kukatika ni ukavu na kutokuwa na matunzo, hasa kwa kutozipa unyevunyevu pindi zinapokuwa zimesukwa.

Hata wale walioweka dawa nywele, wanapoacha kuziweka tena dawa pale zinapoota nywele za asili pia hukatika. Kwa hivyo, nywele yoyote isipokuwa na matunzo hukatika hata kama hujatumia jeli.

Mwamvi anasema wakati wa kufumua nywele ya yeboyebo iliyosukwa kwa jeli unapaswa kufuata hatua zitakazokuwezesha kutokukata nywele na kuiacha ikiwa na afya.

Anasema kwanza unapaswa kunyunyizia maji katika nywele ya yeboyebo kisha ukihakikisha nywele imepata unyevu anza kuifumua.

“Ukimaliza kufumua hupaswi kuichana, utapaka mafuta ya kimiminika kama nazi na conditioner ili kuwezesha kulainisha nywele.

“Baada ya hapo anza kuichambua nywele kwa kutumia vidole na sio chanuo au kitana. Ukishamaliza sasa unaweza kuiosha nywele yako kwa kutumia maji ya uvuguvugu na sabuni ya nywele (shampoo),” anasema Mwamvi.

Pia, anasema baada ya hapo zikaushe nywele kwa taulo au kitambaa safi kisha paka conditioner na mafuta laini na anza kuzichana kuanzia kwenye ncha ili kutoa nywele zilizokufa.

Mdau wa kusuka, Zainab Khatib anasema zamani alikuwa akiona yeboyebo zinasukwa kwa kutumia majivu ili nywele zishikike vizuri.

‘Lakini kuna siku nimekwenda kusuka nikaambiwa nunua jeli ndogo Sh1,000 nikauliza ya nini, nikaambiwa inatumika kushikia nywele za usoni (malaika) na inaleta mng’ao,” anasema Khatibu.

Kuhusu nywele kukatika, anasema huwa anajitahidi kuzifumua mapema, yaani anakaa nazo kabla ya wiki mbili kuisha ili kuepuka kujifunga.