Prime
Loveness: Mimi ni mwanamke, nitaolewa na nitazaa

“Sijawahi kusumbuliwa na namna watu wanavyoniangalia au kunizungumzia wakisema kwamba ni mwanamume, hayo nilishazoea kuyasikia tangu nikiwa mtoto, hayaniumizi kichwa kwa sababu najitambua ni mwanamke tena niliyekamilika”.
Hayo ni maneno ya mtunisha misuli, Loveness Tarimo ambaye amejijengea umaarufu kutokana na mwonekano wa mwili wake kuwa kama wa mwanamume, ilhali yeye anasisitiza kuwa ni mwanamke.
Mwananchi ilifunga safari hadi katika hoteli anayofanyia kazi Loveness na kumkuta akiendelea na majukumu yake ya kila siku ya kufundisha kufanya mazoezi kwa watu wanaotaka kuweka sawa miili yao.
Uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu, Loveness (37) alimkaribisha mwandishi na kwa haraka akaanza kuonyesha misuli aliyonayo, akifahamu fika shauku ya wengi ni kujua uhalisia wa mwili wake.
Kama wafanyavyo watunisha misuli, akaanza kuchezesha kifua chake kwa mtindo wa kupandisha na kushusha upande mmoja mmoja, kitendo hiki kilionekana vyema, licha ya kuwa alikuwa amevalia fulana nyeupe ambayo ni sare ya kazini kwake.
Jicho la mwandishi lilipotua kifuani lilibaini kwamba Loveness hana matiti, lakini hii haiwezi kuwa sababu ya kubishania uanamke wake kwa kuwa wapo wanawake wengine ambao hawana matiti makubwa.
Kitendo hicho ndicho kilianzisha mahojiano kati ya mwandishi na Loveness, bila hiyana akaeleza ameamua kujiweka hivyo kwa sababu anapenda mazoezi na hana mpango wa kubadilika kwa sababu maisha yake yameshakuwa upande huo, si pesa wala mapenzi vinaweza kumbadilisha.
“Najipenda mno jinsi nilivyo, kila ninavyojitazama nafurahi Mungu kuniumba wa aina yake, kwa hiyo hata nikisikia watu wananizungumzia au kunishangaa, furaha yangu inaongezeka maradufu kwa kuwa niko tofauti na wanawake wengine.
“Katika maisha yangu yote hapa duniani, hakuna siku nimewahi kujutia wala kujiuliza kuhusu mwonekano wangu, ndiyo maana nasema sijaona cha kunibadilisha. Hata mpenzi wangu amenipenda jinsi nilivyo, na tunafurahia uhusiano wetu nikiwa hivi,” anasema Loveness.
Kauli hii ya Loveness ilimpa shauku mwandishi kutaka kujua kwa kina kuhusu uhusiano na mpenzi anayemzungumzia, bila hiyana alijibu swali hilo na kueleza matarajio ya penzi hilo ambalo lina mwaka wa nne sasa.
Uhusiano wake na mwanaume huyo ulianza kwa urafiki baina yao baada ya kuwa wanakutana mara kwa mara kwenye eneo la kufanyia mazoezi, hiyo ikiwa ni baada ya kukaa miaka minne akiwa hana mwenza.
“Nina mpenzi tunapendana kweli kweli, tuko kwenye uhusiano mwaka wa nne sasa, tumeshaanza kuzungumzia suala la ndoa, huenda huyu ndiye akawa mwanamume wa maisha yangu.
“Ni mtu ambaye tunaendana na yeye anapenda mazoezi, ingawa mimi ni zaidi yake ila amenipenda jinsi nilivyo. Vitu anavyovipata kwangu nina kila sababu ya kusema amefika,” anasema na kuongeza;
“Nasema tunaendana kwa sababu ni mtu ambaye hapendi kunyenyekewa, anataka usawa kwenye uhusiano na hivyo ndivyo mimi napenda. Huwa sipendi dharau au kuniletea mfumo dume. Huyu anatoa nafasi linapotokea tatizo tunakaa chini tunazungumza na kuweka sawa maisha yanaendelea, sio kuleta ubabe,” anasema Loveness.
Anaeleza kuwa huyu ni mpenzi wake wa nne tangu aanze kujihusisha na masuala ya mapenzi na ilimchukua mwaka mzima kukubali kuanzisha uhusiano naye kutokana na kadhia alizopitia huko nyuma katika maisha yake ya kimapenzi.
“Wakati nyie mnaniona mwanaume, kuna mwanamume amefika hapa na ananiona mtoto mlaini kabisa, tofauti yangu na hao wengine mimi sivai magauni wala kuhangaika na vipodozi. Niko natural, ngozi yangu haipakwi mafuta wala kipodozi chochote na iko vizuri kuliko hao wanaohangaika kujiremba,” anasema.

Mtunisha misuli na mshindi wa shindano la Miss Fitness 2019, Loveness Tarimo akizungumza na mwandishi wa makala hii katika mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni.
Mbali na kutojiremba, mwanadada huyu anasema hajawahi kutamani kuwa na matiti makubwa kama ilivyo kwa wanawake wengine na msimamo wake ni kuukubali na kuupenda mwonekano alionao.
Kama ilivyo kwa wanawake wengine wanavyokuwa na shauku na itakavyokuwa siku ya harusi, hivi ndivyo ilivyo kwa Loveness, lakini yeye amekwenda mbali na kueleza kuwa harusi yake itakuwa tofauti, hivyo amewataka Watanzania kusubiri kwa hamu siku hiyo ifike.
Si hivyo pekee, Loveness pia anakusudia kuanzisha familia pindi atakapoingia rasmi kwenye ndoa na idadi ya watoto anaowahitaji ni wawili bila kujali jinsia zao kwa kuwa kwake mtoto yeyote ni sawa.
Kazi za nyumbani
Loveness anakiri kuwa licha ya kumudu kufanya kazi zote za nyumbani kama ilivyo desturi ya wanawake, hafanyi kazi hizo kutokana na kubanwa na majukumu ya kazi zake za kumwingizia kipato.
“Kazi za nyumbani naweza kufanya zote ila kwa bahati mbaya sina muda, kwa kuwa mara nyingi nabanwa na kazi za gym. Asubuhi naamka alfajiri kuwahi hotelini kwa ajili ya kuwafanyisha mazoezi wageni, ninavyotoka jioni naenda kwenye gym ya mtaani. Huko nafanya mazoezi yangu binafsi. Pia kuna watu nawafundisha mazoezi, mimi ni mwalimu wa mazoezi.
“Ratiba hiyo inanifanya nisipate muda wa kujihusisha na shughuli za nyumbani, naishi na wadogo zangu wanafanya haya mambo, mimi natafuta, kazi pekee ambayo naifanya mwenyewe ni kupika chakula na hiki ni cha kwangu, sisi watu wa mazoezi tuna namna ya kuandaa vyakula vyetu mtu mwingine anaweza asifahamu,” anasema.
Kwa Loveness, chakula ni kitu muhimu zaidi, ili awe na mwendelezo mzuri kwenye mazoezi yake ya kuuweka mwili sawa, mpangilio mzuri wa chakula ni kitu anachokizingatia.
“Asubuhi nakula mayai 15, mchana nakula wali wa brown na vidari viwili au vinne, jioni naweza kula mkate wa brown, ila hapo katikati ni lazima niwe nakula iwe matunda au mboga za majani. Kutengeneza mwili wa aina hii si kitu rahisi, ni gharama kubwa inatumika. Binafsi imenichukua miaka 10 kutengeneza misuli hii inayoonekana sasa,” anasema.
Historia kwa ufupi
Loveness alizaliwa Aprili 29, 1986 akiwa mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto wanne, wadogo zake wawili wa kike na mmoja wa kiume.
Baba na mama yake walikuwa watu wa michezo, hivyo na yeye akajikuta akianza kupenda mpira wa miguu tangu akiwa mdogo, hata ndoto yake ilikuwa kuwa siku moja awe mchezaji maarufu wa mpira wa miguu.
Hilo lilimfanya kuwa karibu zaidi na watoto wa kiume na akajikuta anapendelea mavazi ya kiume, ili kumpa nafasi nzuri ya kucheza mpira.
Hali hiyo pia imemfanya hadi sasa kabatini kwake kusiwe na mavazi yoyote ya kike, kwani nguo zake ni suruali, kaptura, fulana na raba kama ambavyo huvaa wanamichezo.
Tangu akiwa mdogo alianza kuhusishwa na uvulana, kitu ambacho kilikuwa kinamshangaza hadi pale alipolalamika kwa wazazi wake na kumwambia asiwajali wanaomwambia hivyo.
Maneno hayo yaliingia vyema masikioni mwa Loveness, hivyo tangu wakati huo hajawahi kuumizwa kichwa na anayemuona yeye ni mwanamume kwa kuwa ukweli anaufahamu na hana sababu ya kupoteza muda kuuthibitisha.
Mwanadada huyu amecheza mpira wa miguu katika timu kadhaa za wanawake jijijini Dar es Salaam, kabla ya kuupa kisogo mchezo huo na kuhamia kwenye mazoezi ya viungo na hatimaye kuwa mtunisha misuli.
Mwaka 2019 alitwaa taji la Miss Fitness, akiwa mtunisha misuli bora mwanamke na kuingia kwenye kinyang’anyiro cha aina hiyo Afrika Mashariki, ambako aliibuka mshindi wa pili. Tangu wakati huo, shindano hilo halijafanyika tena nchini, hivyo hadi sasa Loveness ndiye anashikilia taji hilo.