NIKKI WA PILI : Zaidi ya mwanamuziki

Mwanamuziki kutoka kundi la weusi ,Nikki wa Pili .

Muktasari:

Wengi wa wasanii wa Tanzania hawajaenda shule, huku baadhi yao wameishia elimu za sekondari. Hali hii ni tofauti na msanii Nickson Simon au Niki wa pili ambaye yeye kwa upande wake amesoma elimu ya juu na kuwa na shahada ya pili na sasa anaendelea na masomo yake ya shahada ya tatu ya PhD katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mara nyingi tumezoea kuona wasanii wakijishughulisha na kazi za sanaa pekee na ni wachache ambao wanafanya kazi za sanaa na wakati huohuo wakajishughulisha na shughuli nyingine za kitaalamu.

Wengi wa wasanii wa Tanzania hawajaenda shule, huku baadhi yao wameishia elimu za sekondari. Hali hii ni tofauti na msanii Nickson Simon au Niki wa pili ambaye yeye kwa upande wake amesoma elimu ya juu na kuwa na shahada ya pili na sasa anaendelea na masomo yake ya shahada ya tatu ya PhD katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Tofauti na usanii msanii huyu pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa nchini lakini pia ni mtangazaji mshiriki katika kipindi cha Cloud 360.

Kwa mujibu wa Niki wa Pili, aliingia katika uchambuzi wa masuala ya kisiasa bila kutarajia baada ya kualikwa siku moja na kuonekana kwamba alifaa, hivyo waandaaji waliomwomba ili awe mchambuzi ndani ya kipindi hicho cha runinga.

Anasema kwa kuwa shahada zake amesomea masuala ya maendeleo, imemuwia rahisi kwake kuchambua masuala ya kisiasa ingawa yeye si mwanasisasa na hatarajii kuingia huko.

“Haukuwa mpango wangu ni kitu ambacho kimetokea ghafla, sijawahi kujiona kama mchambuzi lakini kumbe vile unavyotoa mawazo yako kuna mapokeo ambayo wengi wanayapokea inakuwa tofauti,” anasema.

Hata hivyo, Nikki wa Pili anasema anapenda vijana wenye uthubutu, hata alivyosikia idadi kubwa ya wasanii wanajiunga katika siasa aliwaunga mkono.

Anasema ni kitu kizuri kwani inaonyesha kwamba vijana wapo tayari kwa mawazo mapya, lakini jambo la msingi ni lazima watu wawe makini wachunguze na watambue au wafanye utafiti kujua historia zao zikoje na je? Kilichowavutia ni kwenda kuitumikia jamii au kwa ajili ya masilahi yao binafsi.

“Nafikiri kwa wabunge vijana wameonekana wakichapa kazi, ukiangalia mfano kina January Makamba, David Kafulila, Zito Kabwe, Halima Mdee na hata John Mnyika wamefanya vizuri, kwa hiyo unajua vijana wana mwamko wapo tayari kupokea mambo mengi kufanya mabadiliko,” anasema Nikki na kuongeza kwamba ni vizuri kuwa na rais kijana kwa sababu asilimia kubwa ya taifa ni vijana hivyo kiongozi anatakiwa kufanana na wale anaowaongoza.

Mchango alioutua kuendeleza muziki

“Nimejaribu kufanya kwa kiwango fulani katika ushawishi. Kwanza, nimeshiriki harakati za kuishawishi Serikali itambue kikatiba umuhimu wa sekta ya sanaa.”

Anasema pia kuwa ameshiriki mstari wa mbele kama mfano kupinga unyonyaji unaofanywa kupitia milio ya simu na alitangaza kujiondoa Kampuni ya Spice VAS Africa na Push Mobile mwaka jana na baadhi wakafuata baada ya kuelimisha kuhusu unyonyaji huo.

Kwa mujinu wa Niki wa Pili, wasanii wengi bado hawafahamu hata makadirio ya faida au mapato yanayoingia kupitia milio ya nyimbo zao jambo ambalo ni hatari sana kwani kampuni za simu zinachukua asilimia 60, mzalishaji anachukua 31 na mpaka hatua ya mwisho msanii anapata asilimia mbili hadi sita pekee.

“Harakati za kujiondoa huko zinaathiriwa na mfumo, inahitaji safari ndefu ya ushiriki wa Serikali na uamuzi wa wasanii wenyewe. Kwa hivyo, akimaliza PhD nitakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuendeleza harakati hizo, ili siku moja tuone muziki wetu unaondolewa mizizi ya unyonyaji.

“Ansema mbali na harakati hizo, amekuwa muelimishaji wa fursa za ajira kupitia semina iliyoandaliwa na Clouds Media Group.

Semina hiyo iliitwa Fursa, pia ni balozi wa kupinga rushwa, mtetezi wa haki za binadamu na mwanaharakati wa ulinzi wa mtoto dhidi ya unyanyasaji.

Harakati alizowahi kuzifanya

“Baada ya kumaliza Shahada yangu ya Uzamili, nilipata nafasi ya kufanya kazi katika shirika la kimataifa linalojihusisha na Ulinzi wa Mtoto Dhidi ya Unyanyasaji na Utelekezwaji barani Afrika (African Networking for Prevention and Protection Against Childrens).

Muziki

Niki wa Pili anasema ili muziki wa Tanzania usonge mbele na kuchuana na ule wa kimataifa unahitaji kufanyiwa utafiti wa kina.

Anasema iwapo taasisi zilziowekwa kusimamia sanaa hapa nchini zitaifanyia kazi mikakati hiyo, sekta hiyo itaingiza pato kubwa la taifa na kuongeza ajira kwa vijana walio wengi.

Nikki anasmea licha ya wasanii mbalimbali kujitangaza kimataifa, wanatumia nguvu kubwa sana ambayo iwapo utafiti ungefanyika nguvu hizo ingekuwa ni ziada kwa kuvuka mipaka zaidi.

“Hakuna utafiti, ukitaka kuongelea muziki wa Tanzania ni ngumu kwa sababu hakuna takwimu, huwezi kujua baadhi ya mambo yahusuyo sanaa kwa kuwa kuna vitu vya msingi vya kuweza kufanyiwa kazi lakini vimeachwa tu,” anaanza kwa kusema Nikki.

Nyota huyo anasema wasanii nchini wana malengo ya kuwa namba moja Afrika ndiyo maana wanahangaika kwa fedha ndogo wanazozipata kupitia shoo za kila siku.

Anasema hiyo ndiyo sababu ambayo hata kundi la Weusi wameamua kusaidia, huku wasanii wengine wakiangalia namna ya kutoka kwa kutafuta kolabo na wasanii wa kimataifa ili kuzifikia ndoto zao kwani wanahitaji kufika mbali zaidi ili muziki upanuke, hivyo nguvu za ziada kutoka kwa taasisi hiyo zikiongezwa lengo litafikiwa.

Hata hivyo, Nikki anasema changamoto za mitandao kuzikabili ni mtihani, lakini pia imefungua kitu kipya kwao ambapo sasa wanaweza kuuza muziki wao online, “zamani ilichukua wiki moja muziki kufika vijijini lakini kwa sasa ndani ya sekunde kadhaa unaweza kuwauzia mamilioni ya watu muziki wako.

“Kinachotakiwa kufanya ni namna tunavyotumia faida katika teknolojia hizi lakini pia vilevile kuangalia namna ya kupunguza madhara ya teknolojia.”

Nikki anasema ili kufikia katika viwango vinavyofaa kuna mambo ambayo yanatakiwa kufanywa na taasisi zilizopewa dhamana ikiwamo kuangalia namna soko linakoelekea wapi na namna ya kuweza kuingia huko, mfano soko la muziki wa Afrika lakini ili uweze kuingia huko msanii anatakiwa awe na video nzuri, nchi ina maprodyuza lakini bado hawana viwango.

“Mfano Diamond au Weusi wakienda kutengeneza video Afrika Kusini wanalipa mamilioni ya fedha, lakini bado hatupati kitu wala nchi haipati kitu fedha ya ndani inatoka nje ya nchi, kuna kila sababu sasa Tanzania isomeshe maprodyuza wakubwa wawasomeshe wakafikia viwango fulani ili na sisi tupate watu wanaoweza kufanya kazi kubwa zaidi ili hata wasanii wa nje nao pia watamani kufanya kazi na sisi wakaja kufuata ule ubora wa video kwa hiyo nchi itaingiza kipato kikubwa,” anasema Nikki.

Licha ya hayo aliyoyaongea, Nikki anasema Rais atakayepewa ridhaa na Watanzania, anatakiwa kuzingatia kwamba robo ya Watanzania wamejiajiri kupitia sekta ya sanaa.

“Rais ajaye nataka nimwambie kwamba kuna zaidi ya wasanii milioni moja Tanzania, ambayo ni asilimia kubwa ya nchi sanaa inaweza kuajiri watu wengi, ninapopiga muziki wangu Dj anapata kipato, prodyuza na wengineo kwa hiyo kuna mzunguko mkubwa, hivyo ana uwezo wa kuutumia muziki ili kutatua tatizo la ajira nchini.”