TUONGEE KIUME: Kukosa kazi kunachangia kuharibu mahusiano

Tunaposema mahusiano tunamaanisha mahusiano ya kila namna. Ndoa, urafiki, uchumba, mzazi na mwana, ukwe, ushemeji na kila namna ya mahusiano.

Na tunaposema kazi tunazungumzia kitu kama ajira au biashara au labda tuseme shughuli yoyote ambayo inakuingizia pesa kihalali kwa lugha rahisi tungeweza kuweka kichwa cha makala hii kuwa, ‘kukosa ajira au biashara inayokupa chochote mfukoni kunaongoza kuvunja mahusiano’.

Usipokuwa na kazi ndoa yako itayumba tu, hata kuwe na upendo wa kiasi gani kati yako na mkeo. Atakupenda leo, kesho na keshokutwa baadaye atagundua kuwa yeye na watoto wana mahitaji muhimu ambayo hayawezi kutimia bila pesa, na pesa huwezi kuipata bila kazi au biashara.

Mkeo naye ni mtu sio mbao, ana akili kichwani sio barafu, hivyo ataamua kutafuta namna ya kukusaidia bila kupunguza upendo wake kwako kwa sababu anajua utakuwa nayo kesho. Hapo ndio utaanza kuwaza vitu vingine katoa wapi pesa au ananichukuliaje hivi ambavyo mahitaji ndani anatimiza yeye kwa kiasi kikubwa na taratibu upendo utaanza kupungua kutoka kwako kwenda kwake, na usipokuwa makini uhusiano au ndoa itaharibika.

Kuhusu marafiki nao, Waswahili wanakwambia akufaae kwa dhiki ndiye rafiki kwa enzi hizi, kutokuwa na pesa ni dhiki kubwa zaidi, kwa hiyo marafiki zako wa kweli hii ndiyo itakuwa tiketi yao ya kukuonyesha upendo wa dhati walionao juu yako.

Watakusaidia watakutumia pesa kwenye simu, watakununulia pombe mtalewa na mtafurahia tu.

Lakini zikipita wiki mbili tatu wataanza kukuchoka, wataanza kukuona kama kupe au kunguni, unawanyonya tu kwa sababu zamani walikuwa wanakupa na wewe unawapa sasa hivi huna.

Matokeo yake ni kwamba urafiki utaharibika kwa sababu utakuwa ni urafiki wa upande mmoja na tangu dunia imeanza urafiki wa namna hiyo haujawahi kudumu. Kwa ndugu unaambiwa ukiwa huna hela, kwenye vikao vya familia hata hawakuulizi unatumia kinywaji gani, utashangaa tu umeletewa ‘mirinda nyeusi’. Na ukitaka kuchangia hoja kuwa makini na sauti yako, ukiipandisha kidogo tu wanaweza kukwambia unafanya fujo.

Ukweli ambao unaweza kuamua kuukataa ukipenda ni kwamba usipokuwa na pesa ya kutatua matatizo angalau madogo madogo ya familia, unakosa kuheshimika kwa sababu kwa dunia ya sasa watu wanathamini vitu kuliko utu.

Mwisho wa siku tusikubali kukaa bure, pia tuwakumbushe na watoto wetu umuhimu wa kutokukaa bure. Wanapotoka vyuoni, waache kukaa nyumbani kusubiri ajira ziwafuate. Itafikia mahali kinamama wataanza kuwatuma vitunguu magengeni bila kujali ni wavulana au wasichana.

Ukifanya shughuli yoyote atakuagiza uje na vitu kama mkate, maziwa, sukari, badala ya kukuita kwa jina lako atakuita baba au mama.