Vijana kusaidia wazazi ni wajibu au fadhila?
Dar es Salaam. Ukipata mshahara wako wa kwanza utautumia kufanya nini? Ni swali ambalo majibu yake yanatafsiri mengi kuhusu mitazamo ya vijana juu ya maisha yao baada ya kipato cha uhakika.
Ukiachana na malengo mengine, mgawo kwa wazazi ni sehemu ya malengo ya kipato cha kwanza kwa vijana wengi nchini, kama wanavyosimulia wenyewe.
Ingawa kutoa kwa mzazi kunatafsiriwa kama kulipa fadhila ya malezi katika mtazamo wa kiuchumi, tabia hiyo ni ufunguo wa milango ya kutegemewa na hatimaye umasikini.
Mitazamo ya vijana
Habiba Swaleh anasema aliutumia mshahara wake wa kwanza kumshonea mama yake nguo na kumnunulia baba yake kanzu na mswala kama sehemu ya fadhila kwao.
Asingekuwa na namna nyingine zaidi ya kufanya hivyo, kwa kile alichoeleza hadi anafikia kuajiriwa na kulipwa mshahara wazazi wake ndio waliomwongoza.
Kilichofanywa na Habiba, kinafanana na alichokifanya Daudi Sondi, anayesema alitumia fedha kubwa aliyoipata kwa mara ya kwanza, kuwatumia wazazi wake.
“Nilipata Sh1 milioni, ilikuwa ndiyo fedha kubwa kwangu, nikawatumia wazazi Sh500,000 kama shukurani ya kunilea,” anasema.
Hatua ya Sondi kutuma fedha hiyo, anasema ililenga kuwaonyesha wazazi wake kwamba wamemlea vema, wamemkuza na sasa anamudu kujitegemea.
Kwa Khalfan Nyenzi, wazazi ndiyo kipaumbele chake, hivyo anatarajia kutumia mshahara au kipato chochote kikubwa atakachopata kuwafurahisha wazazi, ndugu na jamaa walioshiriki kumfikisha alipo sasa.
Nyenzi anaona kufanya hivyo ni kulipa fadhila kwa upande mmoja, lakini pia kujitengenezea baraka mbele ya Mungu kwa upande mwingine.
“Hata dini zinasema watunzeni wazazi wenu na wazazi ndiyo pepo zetu, nikipata fedha nitawatumia,” anasema.
Alikwenda mbali zaidi na kueleza badala ya kumpa mwanamke ‘kuhonga’ kwa ajili ya starehe ya mwili bila fadhila zozote, ni vema awape wazazi wake.
Mitazamo kama hiyo walikuwa nayo vijana wengine wanane waliohojiwa na gazeti hili, wakitaja sababu mbalimbali za kidini, kimila na shinikizo la jamii.
“Kuna wakati watu wakikuona umeanza kuingiza kipato, wanakwambia unapaswa kuwatumia wazazi wako,” anasema Dimoso Dimo, anayeishi Morogoro.
Wengine wanashinikizwa na wazazi wenyewe, kama kilichomtokea Happyness Ameni, aliyeambiwa na wazazi wake atakapopata ujira wa kwanza baada ya kuajiriwa awakumbuke wao kwanza ili wambariki.
Lakini wapo walio na mitazamo tofauti kuhusu hilo, akiwemo Richard Amani anayesema alitumia mshahara wake wa kwanza kununua vitu vitakavyomwezesha kuishi mwenyewe.
“Nilinunua kitanda na godoro ili nijipange kwa ajili ya kupanga chumba, maneno yalikuwa mengi, ndugu walipiga simu ulipofika mwisho wa mwezi, lakini niliwaweka wazi,” anasema.
Kwa mujibu wa Amani, kujijenga kiuchumi ndicho kipaumbele chake na baada ya hapo ndipo ataanza kurudisha fadhila kama atakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Anachokizungumza Amani, kinaelezwa pia na Adam Kisukari, anayesema wazazi wake wanapaswa kutambua kuwa ana mipango mingi anayopaswa kuitimiza kabla ya kusaidia wengine.
“Wazazi walinilea ni wajibu wao, waniache nami nitengeneze mazingira ili nije kulea watoto wangu kama wazazi wangu walivyonilea mimi. Sijalelewa nije kulea walionilea, sasa watakaozaliwa na mimi watalelewa na nani,” anasema.
Ingawa kauli hiyo iliwahi kusababisha alaaniwe na baba yake, Kisukari anasema kwake ni msimamo na hadi sasa hajapata matokeo ya laana ya mzazi.
Wazazi na fikra mseto
Jambo hilo, limeibua hoja tofauti za wazazi, wengine wakitaka wahudumiwe na watoto kama wajibu, lakini wapo wanaotaka watoto wao wajiimarishe binafsi kabla ya kuwaangalia wao.
“Ukiona mtoto anasema anataka kujiimarisha binafsi na hataki kukuhudumia kama mzazi wake, huyu ana tabia ya uchoyo na hata Mungu atamlaani,” anasema Nancy Shirima, mama wa watoto sita.
Grace Mtulia, mke na mama wa watoto wanne, anasema ni faraja yake kuona anahudumiwa na uzao wake na hilo ndilo linalomfanya ajivunie kuzaa. Anasema ni wajibu wa mtoto kumhudumia mzazi, kwa kuwa naye alimhudumia.
“Kama wanasema wanatakiwa kujijenga kwanza, mbona wakati tunamlea hatukusema tujijenge kwanza, ni wajibu wa mtoto kumtumia fedha mzazi wake,” anasisitiza.
Kwa Mbegu Ally, mtazamo wake ni tofauti, akisema mtoto anazaliwa anatunzwa na kusomeshwa ili ajitegemee na siyo kutegemewa.
“Tunawabebesha watoto majukumu makubwa ndiyo maana unajiuliza kwa nini mwanangu hajengi nyumba kama mtoto wa fulani, kumbe unamkandamiza.
“Umempa jukumu la kukuhudumia na wewe kama mzazi umeamua kubweteka unatarajia mwanao atakuwa na maendeleo,” anasema.
Katika watoto watano alionao, Ally anasema wanne ni watumishi wa umma na hakuwahi kuwaomba msaada, wala hatarajii chochote kutoka kwao.
Furaha yake, anasema ni kuwaona wakimiliki mali zao binafsi na wanavyojenga familia zao bila kuwaza urithi kutoka kwake.
Vivyo hivyo kwa Mama Nelson, anayesema angalau mtoto anapaswa kuachwa ajijenge kwa miaka kadhaa kabla ya kubebeshwa mzigo wa kutegemewa.
“Ukimtegemea mwanzoni utamuathiri, muache mtoto ajijenge, ukifikia umri wa kuhudumiwa ndiyo akuhudumie, vinginevyo ukoo wote mtakuwa masikini,” anasema Mama Nelson, mwenye watoto wawili.
Unajiweka karibu na umasikini
Mwanazuoni wa masuala ya uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sylvesta Rugaihyamu anasema msingi wa kujijenga ni kuanza kujitazama mwenyewe.
Anasema pamoja na wajibu wa upendo kwa mzazi, mtoto anapopata mshahara wa kwanza anapaswa kufungua pazia la maisha yake binafsi.
Kwa mujibu wa Dk Rugaihyamu, tabia ya mshahara wa kwanza nusu au wote kuutuma kwa mzazi unamjengea kijana kutegemewa na hivyo kujiweka karibu na umasikini.
“Ukituma inaonyesha kuwa sasa umefikia hatua ya kuhudumia na watu wanatarajia huduma kutoka kwako kila siku kama hiyo ukiyowatumia. Mwisho wa siku utashindwa kufanya maendeleo binafsi,” anasema.
Hata hivyo, mwanazuoni huyo anasema kuna umuhimu wa mtoto kuonyesha upendo kwa mzazi, lakini siyo lazima fedha, hata salamu.
“Kwa mfano kila siku ukiandika ujumbe au kumpigia simu mzazi kwa ajili ya kumsalimia unatengeneza mazingira mazuri. Kinachohitajika ni kwamba watoto wasiwasahau wazazi, ila siyo kuwalipa fadhila, kwa sababu nao wana maisha binafsi,” anasema.
Dk Rugaihyamu anasema kauli yake hiyo haimaanishi kwamba mtoto hapaswi kumtumia kiasi chochote mzazi wake, bali anapaswa kumpa kile ambacho hakitaathiri kujiimarisha kwake.
Lakini, msisitizo wake ni upendo wa mtoto kwa mzazi kama jambo muhimu zaidi kuliko kutuma mshahara wa kwanza.
Mwanazuoni mwingine katika chuo hicho, Respich Soka anasema suala hilo limesimama kiimani na kijamii. Kiimani, anasema wapo wanaoamini mshahara wa kwanza unapaswa kulipa fadhila kwa wazazi na hata kupeleka kwenye nyumba za ibada.
Lakini kijamii, anasema utaeleweka iwapo utakapopata mshahara wa kwanza utautuma kwa wazazi.
Anasema hakuna uhusiano wa kutegemewa na kutuma fedha kwa wazazi. “Kama wewe ni mtegemewa haijalishi umetuma mshahara wa kwanza au haujatuma utategemewa tu,” anasema.
Hata hivyo, anasema kutuma mshahara wa kwanza kwa wazazi hakuangalii hali ya uchumi wa mzazi, inafanywa kuonyesha shukrani na fadhila.