Wanawake ni watoto wenye umri mkubwa

Muktasari:

  • Mtu mmoja alikwaruzana na mkewe kwa sababu alikuwa anahitajika akitoka ofisini kwake ampitie mkewe ofisini pia, kisha waondoke kwenda nyumbani, na hii ndiyo ratiba yao ya kila siku.

Mtu mmoja alikwaruzana na mkewe kwa sababu alikuwa anahitajika akitoka ofisini kwake ampitie mkewe ofisini pia, kisha waondoke kwenda nyumbani, na hii ndiyo ratiba yao ya kila siku.

Sasa siku hiyo, kama kawaida, muda ulivyofika jamaa alitoka ofisini, akawasha gari, safari ya kuelekea ofisini kwa mke wake ikaanza.

Lakini akiwa njiani, akakutana na mama mmoja, jirani yao.

“Unaelekea nyumbani?” Jirani akamuuliza jamaa.

“Ndiyo mama.” Jamaa akajibu.

“Naomba unipe lift.” Jirani akasema na akapewa jibu la hakuna tatizo, ingia.

Basi jirani akapanda na kukaa kiti cha mbele. Jamaa akaendesha mpaka ofisini kwa mke wake, akamjulisha kuwa amefika na akaegesha gari nje akimsubiri. Baada ya dakika chache mke alikuja; alipofika akagundua kuwa kiti cha mbele kuna mtu amekaa hivyo yeye akaenda kukaa kiti cha nyuma na safari ikaanza.

Huwezi kuamini, safari nzima mke wa jamaa alikuwa kimya, hakuzungumza neno hata moja ukiachana na salamu. Na sio kwamba walikuwa hawazungumzi humo ndani, hapana, walikuwa wanaongea yeye na jirani lakini hata jamaa alipojaribu kumjumuisha mkewe kwenye stori zao, mke wake alikuwa anajitoa, hachangii.

Jamaa anakwambia kuanzia pale akafahamu kuna jambo atakuwa ameharibu, lakini hakujua linaweza kuwa jambo gani hilo.

Anakwambia kila alipojaribu kujipima alijiona ni msafi, sasa shida ilikuwa wapi? Hakuelewa kabisa.

Lakini safari haikuwa mbali, hivyo walipofika anapoishi jirani wakamshusha, kisha wao wakaendelea na safari. Jamaa anakwambia kitendo cha jirani kushuka tu, mke wake akalipuka na lawama. Anamuuliza jamaa kwa nini anapenda kuwapa upendeleo na kipaumbele wanawake wengine.

“Kwa nini,” jamaa akauliza. Akajibiwa kwa nini umemruhusu jirani akae kiti cha mbele wakati unajua na mimi nipo kwenye safari moja.

“Kwa hiyo ningefanyaje?” Jamaa akauliza. Akajibiwa kwa nini hukumwambia akae kiti cha nyuma.

“Kwani ni mimi niliyemwambia akae kiti cha mbele, kaona hakuna mtu kaamua kukaa, kwa nini nimzuie? Kwani wewe ukikaa nyuma kuna tatizo gani?” Jamaa akauliza, na hapo akawa ameharibu kila kitu.

Mwanamke akalipuka zaidi, anadai jamaa hamjali na ndiyo maana haoni tatizo kumuweka kiti cha nyuma wakati kiti cha mbele kuna mwanamke mwingine.

Na mwisho wakaishia kwamba kuanzia siku hiyo kila mtu aende kazini kwa gari yake, hakuna kufuatana.

Umeona akili za wanawake zinavyofanya kazi? Nadhani hakuna kitu wanawake wanatamani kama kuwa mwanamke wako kipaumbele chako zaidi ya mwanamke yeyote yule. Yaani anataka hata ukimlinganisha yeye na mama yako mzazi, jibu liwe yeye ndiyo bora zaidi. Hivyo kama ni jambo ambalo liko ndani ya uwezo wako au halikuharibii chochote unaweza kumdanganya nalo tu.

Ni kama mtoto, ndege ikipita juu akililia, humfokei, unamwambia ikishuka nitakununulia mwanangu.