Kinyongo kinavyopoteza upendo ndani ya familia

Limekuwa jambo la kawaida kusikia habari mbaya za kikatili kama mauaji, vipigo, ubakaji na ulawiti kutoka ndani ya familia.

Kama sio mke, mume au watoto wameuana basi utasikia matukio kama baba amembaka binti yake au amemlawiti mwanaye, utasikia mama amechoma viganja vya mtoto wake.

Kwa tafsiri, familia ni muungano baina ya baba, mama na watoto wanaopaswa kuishi pamoja huku upendo, utu na mshikamano vikiwa nguzo kuu katika maisha ya kila siku.

Viongozi wa dini, wanasaikolojia, wataalamu wa masuala ya ustawi wa jamii na watetezi wa haki za binadamu wanasema mmomonyoko wa maadili, wazazi kusahau wajibu wao na kukosekana kwa utu vimekaribisha ukatili kwenye familia.

Mchungaji Richard Hananja anasema siku hizi hakuna mafundisho ya asili, badala yake yanatumika ya mitandaoni na kusababisha balaa ndani ya familia.

Anasema kitendo cha watu kuwekeza uchungu moyoni na kushindwa kupata suluhisho la matatizo yao kimeongeza ukatili ndani ya familia.


Matukio ya kikatili ndani ya familia

Agosti 12, mwaka jana Mzee Florence Komba (70), mkazi wa Kijiji cha Mahanje katika Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma, alifariki dunia baada ya kuzikwa akiwa hai kwa tuhuma za kumuua mwanaye, Severine Komba (34) kishirikina.

Ilidaiwa kuwa watoto wake wawili walishirikiana na baadhi ya vijana wa kijijini hapo kumzika baba yao kwenye kaburi lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya maziko ya Severine.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mahanje, Jabiri Fussi anasema alipata taarifa za tukio hilo Agosti 11 mwaka jana na baadaye kuthibitisha baba huyo kuzikwa na wanaye akiwa hai.

Tukio lingine linawahusu watoto wawili waliofariki dunia baada ya mama yao mzazi, Veronica Gabriel (30), mkazi wa Kijiji cha Mwabagaru, Kata ya Buseresere, Wilaya ya Chato, mkoani Geita kuwanywesha sumu kisha na yeye kunywa kwa madai ya ugumu wa maisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe alisema mama huyo mwenye watoto watano aliwanywesha watoto wote sumu ya kuua wadudu kwenye nyanya na wawili kati yao kufariki.

Sio hivyo tu, Mkazi wa Iringa, Imani Mfilinge (46) alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na kosa la kumbaka bintiye wa kumzaa mwenye umri wa miaka 13. Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 24, 2023 baada ya Mahakama ya Wilaya ya Iringa kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Kifo cha Naomi Marijani (36), mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam miaka kadhaa iliyopita ni kati ya matukio yaliyotikisa nchini yakitokea ndani ya familia.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaa, Camillius Wambura, Mumewe Khamis Luwoga maarufu kama ‘Meshack’ alikiri kumuua mkewe kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.


Nini chanzo cha ukatili kwenye familia?

Akizungumzia kuweka uchungu moyoni, Mchungaji Hananja anasema, “uchungu ule unapokomaa mtu anachukua maamuzi yasiyo sahihi, hapo ndio anaamua kuua. Kwa hiyo kuua ni matokeo ya kile kilicho ndani yake kwa muda mrefu,” anasema Hananja.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatolikicha Ruaha (RUCU), Lupyana Kilimuhana anasema ukifanya uchunguzi utagundua wanandoa wengi hawaanzi na upendo isipokuwa mapenzi.

“Wanafamilia wengi wameanzia kwenye mapenzi ambayo kimsingi ni Individual setup kwanza, hayo mapenzi yakifaulu kujibu maswali mengi huweza kugeuka kuwa upendo, lakini yakishindwa kujibu maswali mengi, huwa ni kitu hatari. Utasikia watu wameuana,” anasema.

Anasema kubaka mtu, kuua, kudhuru mwanafamilia au hata kama si mwanafamilia ni kutafuta majibu ya maswali ambayo yamekosa majibu.

“Hata wanaojiua nao ujue walikuwa wanatafuta majibu mahala wakakosa na wakabakiwa na jibu moja tu, kujiua,” anasema.

Mchungaji wa Kanisa la Elgibo, Paul John anasema chanzo kikubwa ni mmomonyoko wa maadili.

“Ilivyokuwa zamani na sasa ni vitu viwili tofauti, hakuna maadili na jamii inaishi inavyotaka, ndio maana baba anambaka au kumlawiti mtoto wake bila huruma,” anasema Mchungaji John.

Hananja anasema wapo baadhi ya watu wanaoingia kwenye ndoa na kuanza kutengeneza familia, sio sahihi.

“Hawajapata mafundisho ya mambo ya familia, watu wanaingia kwenye ndoa kama familia ya nyau au mbuzi tu, leo wanachumbiana, hawafahamiani wanaenda kupewa mafunzo ya siku moja kisha ndoa. Kuna ndoa hapo,” anasema Mchungaji Hananja.

“Mafundisho yanayopatikana ni ya hovyo hovyo, tena kwenye mitandao na kibaya zaidi kila mmoja hatimizi wajibu wake na hivyo anasababisha hasira.”

Mkurugenzi wa Shirika la Kisaikolojia The Regional Psychosocial Support Initiative (REPPSI), Edwick Mapalala anasema watu wengi wameweka nguvu kwenye pesa kuliko utu na ubinadamu.

“Tunathamini vitu kuliko utu, hii inafanya watu wapokee mawazo potofu, yaani mganga akisema ua mwanao upate utajiri, anaenda kuua bila hofu kabisa, akiambia kuwa akifanya mapenzi na mwanaye utapata hela basi hasiti kufanya hivyo, ni hatari sana,” anasema Mapalala.

Anasema imani za kishirikina na kukosekana kwa malezi bora ya watoto kumesababisha matukio hayo kuongezeka kwa kasi.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Joshua Lyandala anasema sababu ya kuongezeka kwa ukatili kwenye familia ni kukosekana kwa uwajibikaji wa wanafamilia, ikiwamo wanaume kutotunza familia na wanawake kutokulea watoto wao.

“Lakini pia kunyimana haki ya tendo la ndoa kumekuwa shida kubwa, wanawake na wanaume kwenye baadhi ya familia hawapeani haki hiyo, jambo ambalo linachochea vitendo hivyo,” anasema.

Mchambuzi mwingine, Atuokoe Tweve anasema historia itabaki mwalimu anayepaswa kufuatwa katika kuokoa hali ya familia kwa sasa.

“Miaka ya 1970 kurudi nyuma suala la mke au mume halikuwa suala la kukutana sokoni, kanisani, njiani, shuleni na maeneo mengine, enzi hizo kijana akitaka mke hata awe anaishi Dar es Salaam au Ulaya alisafiri mpaka kwao ili wazazi au wajomba wao wamsaidie kupata mchumba,” anasema Tweve.

Anasema wazazi na familia yake walikaa chini kuchunguza mienendo ya mabinti pale kijijini kwao au vijiji vya jirani huku vigezo vikiwa familia isiwe ya watu wavivu, wenye magonjwa ya kurithi, wachawi na wengine.

“Wakikaa wanapata msichana anayewafaa na taratibu za kwenda kuomba kuoa zitafikishwa kwa wazazi wa binti,” anasema Tweve.

Anasema ulipokuja utaratibu mpya wa kizazi kipya ndio sasa umekutana na binti sokoni au kanisani anajiliza, unamchumbia.

“Tamaduni hizo ndizo zimechangia mmomonyoko wa maadili, mtoto kuwa wa mtu binafsi, sio jamii tena na matatizo yakitokea kwenye familia fulani, yanabaki hukohuko bila mtu nje kusaidia,” anasema Mgimwa.

“Mtazamo wangu sio kila mila na desturi zetu zilikuwa mbaya, nyingine zilikuwa ni msingi wa familia.”


Upatikanaji wachumba nalo tatizo

Shekhe Abdulkadir Khamis wa Msikiti wa Mkimbizi Iringa, anasema matukio ya kikatili ndani ya ndoa yanachangiwa na namna vijana wanavyopata wenza wao kabla ya kuoana.

Anasema vijana wengi wamepuuza misingi ya awali ya kidini, badala yake wametafuta njia zao za kuchumbiana huku wengi wakisukumwa na mihemko, kutamaniana badala ya kupendana.

“Watu wanaoana kwa matamanio sio kupendana, we fikiria wamekutana facebook au kwenye daladala, mara wameoana, kuna ndoa hapo? Itadumu kweli? Hawa watu wakipata shida watakimbilia kwa nani?” alisema Shekh Abdulkadir.

Anasema familia iliyoanzishwa kwa kutamaniana, matamanio yanapoisha huwa inajijenga chuki na kutosameheana na matokeo yake ni ukatili.

Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Christosiler Kalata anasema wingi wa matukio hayo unaonyesha kuna mahali pameachwa bila msaada wowote.

“Unapoona hali hii ujue kuna eneo limeachwa wazi, kuna sehemu tumeacha upenyo, matukio yanatisha, tujiulize tunakosea wapi? Kama ni kwenye eneo la kuunda familia basi tuanze kurekebisha hapo,” anasema Kalata.

Mtaalamu wa Saikolojia, Matrida Erick anasema kubadilika kwa mifumo ya maisha, hasa utamaduni kumesababisha ukatili kuongezeka kwa sababu tamaduni za kigeni zimekumbatiwa bila kufanyiwa tafiti.

 Anawakumbusha vijana kutokubali kuingia kwenye ndoa na watu wasiowajua wanaoweza kuja kuletea madhara baadaye.

“Unaolewa kumbe kijana anayekuoa ni jambazi, umekutana naye facebook, mnaanza maisha, siku mbili tatu anakutuhumu unamsaliti, anakupiga na kukuua. Mtu huyu anakosa moyo wa msamaha kwa sababu makuzi yake hayakuwa na msamaha,” anasema Matrida.

Anasema matukio hayo yanaonyesha msingi wa familia wa upendo, utu na kuthaminiana haupo tena, jambo linalopaswa kufanyiwa kazi.

Akitoa mfano, anasema watoto waliolelewa kwenye misingi mibovu hujulikana kwenye jamii, hivyo ikiwa kijana au msichana atafanya utafiti atapata uhakika wa nani anahitaji kuolewa naye.

Matrida anasema kuna matukio ya mauaji kwa watoto yaliyoripotiwa mwaka huu, yalihusisha wazazi kufanya hivyo kwa lengo la kutafuta utajiri kupitia ushirikina, jambo lisilowezekana.

“Kwa sababu ya pesa, mtu anaamua kumuua mtoto wake, kwa kweli tulipofikia tunawaathiri hata watoto wetu kisaikolojia, unadhani kila siku wanaposikia habari mbaya wanaonaje?” anasema Matrida.


Nini kifanyike?

Mhadhiri Kilimuhana anasema ni lazima kuwe na mfumo wa kuwafundisha vijana wanaotaka kuingia kwenye uhusiano kwa sasa.

“Kabla ya uamuzi, wanahitaji mafunzo ya kisaikolojia, ili wawe na uwezo wa kufanya uamuzi,” anasema Kilimuhana.

“Wapewe mafunzo ya kuudhibiti mwili, ashki zilizozidi ni tatizo la kibaiolojia na haiwezekani kwamba hakuna jawabu la kitabibu, ashki hizi zikizidi husababisha kufanya kila unaloweza kupata cha kukutoa hapo, ndio maana wanabaka,” anasema.

Mchungaji Hananja anashauri kuwa jambo pekee ni kurejea kwenye mafundisho ili kupata vitu sahihi.

“Zamani ilikuwa huwezi kuolewa au kuoa hovyo hovyo na watu walikuwa na tahadhari.

“Tunahitaji kuwa na taarifa za kutosha kabla ya kuingia kwenye familia badala ya kumpenda mtu bila kumfahamu vizuri, tukiacha sisi watafundishwa na mitandao na wakifundishwa huko watapata mafundisho feki. Mtoto afundishwe na wazazi wake sio kwa shangazi. Mafundisho na maadili yataokoa familia,” anasema.