Kwa dalili hizi, unakaribia kupata shambulio la moyo

Friday October 16 2020
moyo pic

Wiki iliyopita nilizungumizia dalili kuu zinazojitokeza kwa takribani mwezi mmoja kabla ya kupata matatizo ya moyo hasa shambulio la moyo.

Kuna matatizo yanayojitokeza kwenye upumuaji, sambamba na kuashiria matatizo ya moyo, pia yanaweza kuashiria matatizo mengine makubwa kama vile pumu na hata magonjwa ya mapafu.

Tafadhali uonapo dalili hizi ni vyema kuwaona wahudumu wa afya mara moja.

Mapigo ya moyo kutokwenda sawa; hii ni dalili ya wazi ambayo wengi wameizoea.

Kiafya moyo unatakiwa kuwa na mapigo takribani 70 kwa dakika kwa mtu ambaye kiafya hana tatizo lolote, hali hii huwa inatokea mara chache kwa muda na kutoweka kutokana na sababu chache kama vile uoga na hasira.

Kwa wakati ambao mtu anakuwa kwenye hali ya uoga au hasira ni rahisi sana mapigo yake ya moyo kwenda mbio, lakini hata hivyo hali hii hutoweka mara tu hasira na uoga vinapokoma.

Advertisement

Kuyumba kwa mapigo ya moyo pia ni kawaida kuwapata watu wenye shinikizo la damu au hata wenye uzito mkubwa uliopitiliza.

Pia, ikitokea hali hii hutokea mara kwa mara hata kwa wakati ambao mtu hayupo kwenye hali ya hasira au uoga na hana shinikizo la damu ni vyema kupata msaada wa daktari haraka kwa kuwa hii ni dalili ya wazi kabisa kuonyesha kuwa mtu yupo hatarini zaidi kupatwa na shambulio la moyo.

Maumivu ya kifua; wanawake na wanaume wanapitia hali hizi za maumivu ya kifua kwa sababu tofauti za kibaiolojia. Mara nyingi wenye dalili hii huashiria hatari ya kupatwa na shambulio la moyo na hawapaswi kufumbia macho.

Pia, inaripotiwa ni wanawake watatu tu kati ya 10 wanaopatwa na maumivu ya vifua wanapatwa na tatizo la shambulio la moyo. Hivyo, wanaume wapo hatarini zaidi kuliko wanawake kupatwa na shambulio la moyo kupitia dalili hii ya maumivu ya kifua.

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu

Advertisement