Mbosso aeleza kuhusu nyumba aliyowajengea wazazi wake

Muktasari:

  • Adai aliumizwa na hali hiyo na alipania akipata fedha, jambo la kwanza ni kuwajengea nyumba wazazi wake

Hivi karibuni habari kubwa kuhusu msanii Mbosso wa lebo ya WCB, ilihuus kuwanunulia na kuwajengea nyumba wazazi wake.

Mbosso anasema ilikuwa ndoto yake tangu anasoma kuwa siku moja awanunulie au awajengew nyumba wazazi wake.

Msanii huyu ambaye jina lake halisi ni Yusufu Mbwana, alisainiwa WCB Januari, 2018 anasema maisha yake yalibadilika alipoanza kazi na WCB.

Anasema alianza muziki kitambo, lakini alipojiunga na WCB, maisha yalibadilika na ndiyo akakumbuka wazo lake aliloliacha kiporo.

“Unajua kwa nini nimeamua kupanga na kuwajengea nyumba wazazi wangu?

“Kwa sababu walipata taabu wakati tunakua, tulikuwa watoto wanne, lakini tulilelewa katika vyumba viwili kwenye nyumba ya kupanga pamoja na wazazi wetu.

“Niliyachukia sana maisha hayo ndiyo maana nilijiapiza kimoyo moyo kuwa nikipata fedha jambo la kwanza nitawatafutia makazi yatakayowatosha japo kwa uchache,” anasema.

Mbosso ambaye alisainiwa na lebo ya WCB, ikiwa umepita mwaka mmoja tangu kundi la Yamoto Band lilipovunjika mwaka 2017 ambalo lilikuwa likiundwa na yeye jina la Maromboso, Dogo Aslay, Beka Flevour na Enock Bella, anasema mbali ya nyumba pia amewanunulia gari aina ya Iphad.

“Baba yangu anafanya biashara ya matunda katika Soko la Stereo Temeke, sidhani kama kwa shughuli hiyo angemudu kujenga au kununua gari kutokana na kipato kidogo na majukumu ya familia, hivyo ni faraja yangu kuwapa kile walichokuwa hawakifikirii,” anasema.

Anasema hata yeye binafsi maisha yamebadilika, anaishi nyumba nzuri japo ya kupanga kwa kuwa alitaka kwanza kuwaweka wazazi wake pahala pazuri na pia amebadili gari ya kutembelea kutoka Harrier na kumiliki Prado.

Mbosso mwenye wafuasi wasiopungua milioni mbili katika mtandao wa Instagram anasema kupitia muziki wake ametembelea nchi ambazo hakuwahi kufikiria zikiwamo Oman, Comoro, Uswis na Kenya.

Mbosso licha ya kukubaliwa na mashabiki kama alivyotabiri katika wimbo wake wa kwanza alipojiunga na lebo hiyo ‘Watanikubali’, hajalewa pombe ya skendo kama ilivyo kwa wasanii wengine na hadi sasa mahusiano au mapenzi kwake ni maisha binafsi.

Mbosso anasema kwa sasa hana mwanamke baada ya kutengana na mzazi mwenzake.

“Ana mtoto wangu anaitwa Rukia, ninawahudumia wote wawili lakini siishi naye anaishi kwake nami kwangu.

Hata hivyo anasema alitamani kuoa na kuwa na familia tangu akiwa na miaka 20, lakini kutokana na changamoto anazozipata katika mahusiano na anazoziona kwa wengine ameamua kujisogezea muda hadi afikishe miaka 30 na kuendelea.

Mbosso ambaye kwa sasa ana miaka 24, anasema bado ana mambo mengi ya kujijenga katika maisha yake ikiwemo muziki wake,hivyo asingependa mahusiano yakawa chanzo cha kuharibu ndoto zake.