NANI NI NANI SERIKALI YA JPM?- Dk Phillip Mpango – Waziri wa Fedha na Mipango

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango     

Muktasari:

Mpango ni mzaliwa wa Kigoma, baba yake ni marehemu Isidori Nzabhayanga Mpango, ambaye alizaliwa Kijiji cha Kasumo, Wilaya ya Kasulu. Dk Mpango alizaliwa hapohapo Kasumo na ni kaka mdogo wa Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanganyika Magharibi – Kasulu mkoani Kigoma, Dk Gerard Mpango.

Historia na elimu

Dk Philip Mpango ni Waziri wa Fedha na Mipango katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli. Ni mbunge wa kuteuliwa.

Mpango ni mzaliwa wa Kigoma, baba yake ni marehemu Isidori Nzabhayanga Mpango, ambaye alizaliwa Kijiji cha Kasumo, Wilaya ya Kasulu. Dk Mpango alizaliwa hapohapo Kasumo na ni kaka mdogo wa Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanganyika Magharibi – Kasulu mkoani Kigoma, Dk Gerard Mpango.

Dk Mpango ni mchumi mwenye shahada ya uzamivu ya uchumi. Hata hivyo, hadi sasa taarifa zake za elimu ya msingi, sekondari na shahada za awali za chuo kikuu hazijapatikana naye amekuwa vikaoni Dodoma muda mrefu na alishindwa kuzitoa kwa wakati.

Kuanzia miaka ya 1990 hadi 2000, alifanya kazi akiwa mhadhiri mwandamizi wa uchumi katika kitivo cha Biashara (sasa Shule ya Biashara) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Alikuwa akifundisha “Microeconomics”, “Macroeconomics” (kwa mwaka wa pili) na “Public Finance” kwa mwaka wa tatu na kozi za uzamili. (Kwa tafsiri yangu, Uchumi mdogo, Uchumi mkubwa na masuala ya Fedha za umma.)

Amewahi kuwa Mchumi Mwandamizi wa Benki ya Dunia, Mkuu wa Kamati ya kumshauri Rais Jakaya Kikwete wakati huo kuhusu masuala ya uchumi, Katibu binafsi wa Rais anayeshughulikia masuala ya uchumi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, kabla ya kuhamishiwa Tume ya Mipango, Ofisi ya Rais. Nyadhifa hizi zote amezishika wakati wa utawala wa Kikwete.

JPM alipoingia madarakani alimteua kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baada ya siku chache akateuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Nguvu

Kwanza, Dk Mpango ni kiongozi mwenye msimamo thabiti. Baadhi ya watendaji ambao wamewahi kufanya kazi chini yake kwenye ofisi ya Rais wanamuelezea kama mtu anayetaka waliomzunguka wazungumze kwa takwimu na ushahidi hasa katika masuala ya uchumi. Msimamo huo pia aliuonyesha alipokuwa mtaalamu wa Benki ya Dunia. Hakuwa mwoga kuieleza ukweli Serikali pale ambako ilikuwa haifanyi vizuri.

Mathalan, wakati wasomi wengi wa uchumi wakiwa wanapiga kelele za kuisifia Serikali juu ya ukuaji wa uchumi miaka ya mwanzoni ya 2000, Dk Mpango alieleza wazi kuwa lengo hilo la kukuza uchumi kwa asilimia 5.9 haliwezi kufikiwa kwa sababu katika miaka minne iliyopita, Serikali ilishindwa kulifikia.

Alisema: “Angalia kwa miaka minne hadi mitano iliyopita ambayo tulikuwa na sera nzuri za kibajeti, hakuna mwaka ambao ukuaji huo ulifikiwa, hizo ni dalili tosha kwamba hali hiyohiyo ndiyo itajitokeza mwaka huu.”

Misimamo ya namna hii ni nadra kwa wasomi wa ngazi yake walio wengi, ambao hubakia kusifia kila kinachotendwa na Serikali ilimradi kwa kutegemea siku moja watateuliwa kushikilia nyadhifa kubwa. Ushahidi wa msimamo wa Dk Mpango pia umeelezwa na baadhi ya wanafunzi wake aliowafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wengine ni wahadhiri katika chuo hicho hivi sasa. Mwanafunzi wake amenieleza kuwa kama kuna mwalimu ambaye wanafunzi wa uchumi walikuwa wanampenda na kumheshimu ni daktari huyu. Pia anasema kama kuna mwalimu ambaye walikuwa wanamuogopa kwa misimamo yake ni huyu.

Nimeambiwa wakati wote alitaka wanafunzi wake waenende na miiko ya kitaaluma na hakuchelewa kuwa rafiki wa yeyote pale anapofanya vizuri.

Pili, ni kiongozi mwenye dira na maono mapana, ni mtendaji anayeweza kusimamia jambo alilokabidhiwa na likafanikiwa. Alipoteuliwa kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, ndani ya mwezi mmoja ukusanyaji wa mapato wa taasisi hiyo ulivunja rekodi. Kwa mara ya kwanza TRA ilikusanya zaidi ya Sh1.4 trilioni kwa mkupuo. Rais JPM alijitokeza na kumpongeza kwa hatua hiyo na muda mfupi baadaye akamkabidhi Wizara ya Fedha.

Bila shaka hapa tunaweza kupata jambo la nne linalomuongezea nguvu, suala la kujua vyanzo vya umaskini wa Taifa na wapi linafanya makosa kwenye uchumi, ukusanyaji wa mapato na uongezaji wa vyanzo vya mapato. Haya, hajayaokota tu barabarani, ameyaishi tokea akiwa mwalimu wa chuo kikuu na baadaye kufanya kazi kubwa Benki ya Dunia kabla ya kuajiriwa kusaidia mambo ya kiuchumi akifanya kazi kwenye Ofisi ya Rais.

Katika moja ya andiko lake kwenye kitabu cha mwaka 2008 kilichoshirikisha wataalamu wa Benki ya Dunia na ile ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kiitwacho “Sustaining and Sharing Economic Growth in Tanzania” (Ukuaji wa Uchumi Endelevu na Shirikishi Tanzania – kwa tafsiri yangu) na kuhaririwa na Robert J. Utz, Dk Mpango amefafanua ukuaji wa uchumi kwa mujibu wa tofauti za kikanda hapa Tanzania akionyesha tofauti ya vipato katika mikoa na kanda za Tanzania, namna ambavyo rasilimali za Taifa zinagawanywa bila usawa katika kanda na mikoa, akieleza vikwazo vikuu vya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu na kupendekeza hatua za kimikoa na kikanda zinazopaswa kuchukuliwa ili kuufanya uchumi wa Tanzania upae.

Ukilisoma andiko hilo, unaweza kugundua kuwa nchi inao wataalamu na wasomi waliobobea na wenye uwezo mkubwa wa kuyajua matatizo ya uchumi na njia za kuyatatua lakini unaweza kujisikia vibaya kwamba wamekuwa hawasikilizwi na Serikali haina muda na maandiko kama haya ambayo yanatumiwa na nchi nyingine kujikwamua kiuchumi. Ubobezi na ujuzi wake kwa uchumi wa chini na juu wa wananchi na kujua matatizo na hatua za kuchukua ni kigezo tosha kitakachomsaidia daktari huyu kuchukua hatua za kiuchumi za kulivusha Taifa, ikiwa atapewa nafasi hiyo na siasa zikawekwa kando.

Udhaifu

Mahali kote alikopita amechukuliwa kama mtendaji hodari, mweledi na anayejitambua katika majukumu yake. Ni vigumu kupekua na kutambua nini udhaifu wake hadi atakapoanza utendaji. Jambo moja ambalo kwa sasa ni kitisho kwake ni uzoefu wa masuala ya siasa. Watu wake wa karibu wameniambia kuwa kiongozi huyu hata siku moja hakuwahi kuwa na ndoto za kuwa mwanasiasa wala hakuwahi kutamani na kufikiria nyadhifa za kisiasa.

Kuteuliwa kwake kuwa mbunge na baadaye waziri (nafasi ya kisiasa) kuna maana ya kumuweka kwenye wakati mgumu na huenda akachelewa kuenenda na siasa za Bunge na serikalini. Kama hilo likitokea, atapita kwenye wakati mgumu kiutendaji kwani hivi sasa yeye ni mwamuzi na mhimizaji wa mipango na sera na ndiye msimamizi wa jumla na mtu atakayewajibika kwa lolote lile nchi ikiendelea kwenda kombo kiuchumi. Anayo kazi ya kufanya kujigeuza kisaikolojia na kiakili kukubaliana na hali ya sasa kwamba yeye ni mwanasiasa lakini akabaki katika misingi yake ya taaluma na kusimamia.

Matarajio

Tarajio kubwa kutoka kwake ni kuweka matamanio yake mengi ya ukuaji wa uchumi kwenye vitendo. Bila shaka wapo wachumi nguli wengi kama yeye ambao siku zote wamekuwa wakitamani kuibadilisha nchi lakini wanaishia kuwa watendaji na washauri na siyo waamuzi wa mwisho. Dk Mpango leo amekabidhiwa fursa nzito ya kuwa mtu wa mwisho wa uamuzi wa uchumi wa nchi na fedha za nchi.

Wadau wa uchumi wana matumaini makubwa naye. Wengi wanasema amekwishaonyesha njia katika nyadhifa alizopitia na siyo mtu unayeweza kuhoji uwezo wake. Kati ya uteuzi ambao hata kwenye mitandao ya kijamii uliungwa mkono ni pamoja na huu wa kwake, wananchi wana matumaini makubwa naye na matarajio yao ni kuona kero kuu za kiuchumi zinapungua au kumalizwa kwa kiasi kinachoridhisha.

Changamoto

Serikali yoyote mpya inaweza kupambana na umaskini kwa kukuza uchumi wa nchi yake. Tangu miaka 10 iliyopita, nchi yetu imekuwa ikikuza Pato la Taifa kwa wastani wa asilimia 5.9 kwa mwaka ikiwa ni nchi ya 14 kwa ukuaji wa pato hilo Afrika na hadi mwaka huu 2015, imeweka rekodi ya kawaida ya kuwa na Pato la Taifa lifikialo dola za Marekani bilioni 49.

Takwimu hizi ambazo zinaweza kutofahamika vizuri kwa mwananchi wa kawaida kwani haziakisi hali halisi ya mwenendo wa fedha wanazomiliki mifukoni mwao. Hali ya maisha katika Taifa ni ngumu, mfumuko wa bei unakua kwa kasi, deni la Taifa limeongezeka na kufika zaidi ya trilioni 40 na kuna uwezekano mkubwa kuwa hata Rais Magufuli amekabidhiwa nchi ikiwa ina upungufu mkubwa wa fedha.

Dk Mpango amekwishavuka changamoto ya kwanza ambayo hutaka uchumi wa nchi na masuala ya fedha kufanywa na watu wenye weledi mkubwa na waliobobea katika fani hizo kwa muda mrefu, lakini watu hao wanapaswa kusimama kidete dhidi ya hila na maelekezo ya wanasiasa wa ngazi za juu ambao mara nyingi hutaka kushauri njia za uhuishaji wa uchumi bila kuwa wataalamu wa uchumi. Tabia hiyo ya wanasiasa ni tatizo kubwa na ni changamoto ambayo Dk Mpango anapaswa aiwekee msimamo wa kudumu dhidi ya mtu yeyote ambaye atataka kulazimisha siasa ziingizwe kwenye uchumi.

Katika kitabu cha “from Goatherd to Governor,” mwandishi Edwin Mtei ambaye aliwahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania enzi za Mwalimu Nyerere na baadaye Waziri wa Fedha, anaeleza kuwa baada ya Tanzania kukausha hazina kutokana na Vita ya Uganda na nchi kuelekea kufilisika, Mtei alitumwa na Mwalimu kwenda Mataifa ya Magharibi na vyombo vya fedha vya kimataifa ili kuomba misaada ya kukwamua uchumi wetu, alipotoka huko alikuja na hoja za kiuchumi zilizotolewa na mashirika ya fedha duniani ambazo yeye akiwa mchumi alikuwa akiziunga mkono, mojawapo ilikuwa ni ile ya Tanzania kutakiwa kupunguza thamani ya shilingi pamoja na kufanya marekebisho makubwa kwenye mashirika makubwa ya umma ambayo yalikuwa yakijiendesha vibaya na kwa hasara.

Mwalimu Nyerere alimjibu Mtei “…you will devalue our shilling over my dead body” (mtaishusha thamani ya shilingi yetu nikiwa nimeshakufa). Nyerere alikuwa mkuu wa nchi na hakuwa mchumi na hakuwahi kufanya kazi za kichumi lakini hakupokea ushauri wa wana uchumi wa kimataifa na hata Gavana wake. Baada ya ushauri wake kukataliwa, Mtei aliandika barua na kujiuzulu uwaziri.

Changamoto hii inabidi ipigwe vita na Dk Mpango kwani ilishazigharimu Serikali zilizopita ikiwamo ya Kikwete na hata ya Mkapa. Ndiyo maana wakati nilipofanya uchambuzi juu ya namna wizara za JPM zinavyoweza kuundwa (kabla hajajitangaza) nilisema: “Rais ateue waziri wa fedha ambaye anaweza kufanya kazi kwa uhuru na kwa kufuata taratibu alizopangiwa, tusiwe na waziri ambaye atakuwa anaongoza huku anawaogopa wanasiasa waliomzunguka, wakiwamo waliomteua”. Natumaini Dk Mpango na Dk Magufuli mwenyewe wanalitambua jambo hili kwa uhakika.

Ni wazi kuwa kwa namna Dk Magufuli alivyosisitiza suala la kubana matumizi ya Serikali na kwa kuzingatia kuwa ina hali mbaya kifedha, wizara hii sasa itakuwa na jukumu kubwa la kumsaidia ipasavyo kubana matumizi na kusimamia uchumi. Bila shaka changamoto itakayomkabili Dk Mpango na wenzake ni namna ya kuongeza ukusanyaji wa mapato na kupanua vyanzo vya mapato. Wakifuzu kwenye eneo hilo kisha wakaambukiza morali hiyo kwa ngazi za halmashauri na manispaa ili nazo ziwe na fomula moja ya kukusanya mapato na kuongeza vyanzo vya mapato, hatutakuwa na msamiati wa kueleza jambo hili zaidi ya “kuona Tanzania ikipaa kiuchumi”. Lakini kama nilivyosisitiza msingi wa yote haya ni changamoto ya kwanza, ya wataalamu wa fedha kufanya kazi pasi na mashinikizo ya kisiasa kutoka upande wowote. Changamoto hii ikitafutiwa ufumbuzi wa kudumu, itajibu tatizo la bajeti tegemezi moja kwa moja na kwa asilimia 100.

Kwa hatua ya sasa, tunaweza pia kukumbusha hali na thamani ya shilingi yetu pamoja na upandaji holela wa bei za bidhaa za ndani. Sote tunakubaliana kuwa moja ya sababu za thamani ya fedha ya nchi yoyote kushuka ni kukosekana kwa uzalishaji wa bidhaa za ndani na kuifanya nchi kila mara itumie akiba ya fedha za kigeni kununua bidhaa ambazo hazipatikani ndani lakini zingeliweza kuzalishwa ndani ya nchi kama tungeliamua. Mathalan, kwa nini Tanzania itumie aina nyingi ya mafuta ya kujipaka mwilini lakini yakitengenezwa kwa wingi Kenya ambako malighafi zinazotumiwa ni zilezile zinazopatikana Tanzania. Kwa nini Tanzania isiwe na viwanda vyake ikatumia malighafi zake katika viwanda vyake yenyewe. Pia, tunaweza kujiuliza kwa nini nchi yetu inaagiza hata “stick” za kutolea mabaki ya chakula kinywani kutoka China wakati hapa Tanzania tunazalisha mamilioni ya tani za magogo kila mwaka. Haya ni mambo ambayo lazima wizara hii ipambane nayo ili kutusaidia kuongeza uzalishaji wa ndani ya nchi na kupunguza ununuzi wa bidhaa nje ya nchi na hivyo kuifanya fedha yetu iwe na thamani kubwa.

Mwisho kumekuwa na vitendo vya rushwa na ufisadi vilivyopitiliza katika sekta ya uchumi na fedha. Mathalan, benki zetu zimekuwa zikifanya vitendo ambavyo wachumi wa kimataifa wakisikia wanaweza kushangaa. Kuna benki zimewahi kutuhumiwa kutoa mabilioni ya fedha kwa njia ya fedha taslimu kinyume kabisa na masharti ya masuala ya fedha katika nchi karibu zote duniani. Baadhi ya watendaji wa Wizara ya Fedha vipindi vilivyopita wamewahi kutuhumiwa kula njama na benki za kawaida ili kuzinusuru na mibinyo na wajibu wa benki hizo kisheria. Dk Mpango ana kibarua kigumu kutatua changamoto hii.

Hitimisho

Dk Mpango ni mmoja kati ya wasomi na wabobezi mashuhuri kwenye sekta ya uchumi. Kwa miaka mitano ijayo hana cha kujifunza, bali anayo mambo ya kufanya na kila mmoja anasubiri kuona yanafanikiwa. Rais wake mara kadhaa ameshatamka, anataka uchumi wa nchi ukue “seriously”, hizo ni dalili muhimu kwamba Dk Mpango anaweza kuachiwa uhuru wa kutosha wa kupanga mipango ya kiuchumi bila kuingiliwa na masilahi ya wanasiasa. Lengo moja kubwa ambalo lazima alikumbuke ni kwamba ifikie wakati sekta yetu ya uchumi na fedha ndiyo iendeshe siasa, kamwe siasa zisiendelee kutuamulia aina ya uchumi tunaoutaka. Wakati wa kufanya haya ni sasa na mimi namtakia kila la heri.

*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi*

Kuhusu mchambuzi

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com, Email; [email protected]).