Ndani ya boksi: Mama Dangote + menejimenti + akili ya Mondi = utajiri
Ngumu sana kuelewa nguvu ya Bi Sandra, katika michongo ya Diamond. Huyu ni kiungo mchezeshaji. Ambaye toka siku ya kwanza aliamua kutoa ‘asisti’ za mipunga kwa mtoto wake. Akili na moyo wa Bi Sanura, hupatikana katika vichwa vichache sana vya wazazi.
Msione ‘Mondi’ kama kadata kila kitu kuacha chini ya huyu mama. Ni kwa sababu ndio binadamu wa kwanza kuamini kuwa koo na akili ya Nasibu vitabadilisha maisha yake. Ujasiri wa huyu mama hauhitaji elimu kubwa wala upeo wa juu. Ni imani tu.
Wakati lundo la wazazi wakiwasusa watoto. Wakiwachapa na kuwafokea kila uchwao. Kwa kosa la kuendekeza ujinga wa muziki badala ya masomo. Sandra akawa wa kwanza kulihamasisha toto lake lifanye muziki. Akili hizi zipo kwa wazazi wa Marekani Kusini na soka. Mpaka leo huwezi kujua ni yupi kati yao aliyemshika mkono mwenzake ili litokee hili linaloendelea. Unapoona Mondi kila jambo anataka Bi Mkubwa aamue ama ajue, siyo bahati mbaya. Kwa sababu maisha yake ya sasa huyo Bi mdashi ndiye mchonga barabara toka wakiwa gizani.
Wakati watu wengi wakitamani uwepo wa kina Diamond wengi nchini. Binafsi natamani uwepo wa kina Bi Sandra wengi zaidi, kwani ndio wanaweza kutuletea kina Diamond wengi zaidi. Kuliko Diamond kutuletea kina Diamond wengine. Niamini!
Wapo wazazi wengi walioamini katika vipaji vya watoto wao. Kama mama yake Sugu, mama yake Profesa Jay, mama yake Dully Sykes hata mama wa Zuchu. Lakini Bi Sandra ni mfano wa wazi zaidi. Katenda haya katika dunia ya wazi zaidi kupitia mitandaoni na vyombo pendwa vya habari. Kuna mambo aliyavumilia kwa kuyaishi ili mradi mwanaye afanikiwe. Hasa udaku na habari za mjini. Kuna wakati watu walimuona kama kichaa. Au mzazi wa ovyo, pale alipoamua kufumbia macho ‘upuuzi’ wa mwanaye. Lakini yote aliyaacha ili sela la Tandale lipige bao.
Pengine ‘spiriti’ na kujitoa kwake kwa toto lake Mondi. Ndo kuliongeza chachu kwenye akili ya Bi Khadija kwa mwanaye Zuhura. Akaacha elimu aliyopata India ibaki katika stoo za ubongo. Ili atimize ndoto za kuwa staa wa muziki kama yeye kupitia WCB.
Bi Sandra alikuwa mjasiriamali tu, lakini akaamini katika muziki ikibidi hata kwa kuuza cheni ili arekodi.
Unaijua thamani ya cheni ya dhahabu. Tena ikiwa katika shingo ya mama wa Kiswahili? Lakini kwa Bi Sandra akaamini kipaji cha mtoto wake kitaleta cheni nyingi zaidi katika shingo lake. Ewaaaaaa.
Mtazame leo, ana cheni nyingi shingoni na kwenye droo zake pale Madale. Kuliko idadi ya ndevu katika shavu za Sallam SK na Don Vumbwe. Mama aliuza cheni ya thamani katikati ya dhiki kubwa, ili mtoto akarekodi muziki ambao aliamini utaleta neema ndani ya nyumba yake.
Kabla ya kumuwaza Diamond Platinumz, ni vyema ukawaza uwepo wa kina mama sampuli ya Sandra. Ambao watatuletea vichwa vingi zaidi kitaa sampuli ya huyu Mondi Bin Laden.
Unayeshangaa Bi Sandra leo, kuacha mapichapicha ya Mondi kwa zile pisi. Wapo walioshangaa alipofunga safari kutoka mtaa mmoja mpaka wa saba. Akimsindikiza mtoto wake ili akaombe sapoti ya Papa Misifa. Michoreshano ya Mondi na pisi, wazazi wenzake magazetini, mitandaoni. Ilikuwa kitu kidogo sana kwa Bi Sandra, kwani kabla kulikuwa na michoreshano ya kuishi ‘rumu’ moja na mtoto. Huku chumba akipangisha ili apate ada ya dogo. Kwa aliyeishi ‘tauni’ hapa kimazabezabe bila mchongo, anaelewa msala ulivyo ili kulea mtoto, haijalishi hata kama kuna mjengo wa urithi. Sandra aliruka sarakasi zote ili dogo atoboe siku kwa siku, kisha mwaka kwa mwaka mpaka akiwa tayari mkaka. Leo akipanda ndege tulizeni ‘vipapatio’. Unapoona lundo la watu wenye ajira pale WCB. Nyuma yake kuna jasho jingi na akili ya huyu mama.
Hii siyo dunia ya miujiza, manabii na mitume. Hiyo dunia haipo tena sasa ni neema, akili, bidii na imani tu. Bila vitu vyote hivyo tusingeona haya yanayoendelea kupitia Diamond. Kuanzia muziki mzuri mpaka ajira kwa washikaji kibao. Bi Sandra anahusika kwa asilimia 100. Kila kitu kilichopo nyuma ya mtu kuna jasho, akili, bidii na imani ya mtu. Ndio kilichopo kwa Sanura na WCB, hivi vitu siyo bahati, ni bidii na imani.
Mondi mwenyewe ana talanta ya kusimamia mambo ndiyo maana rahisi sana kujua watu sahihi wa kusimamia mambo yake. Kipaji ni moja, usimamizi mzuri wa kipaji ni jambo mtambuka.
Ndio maana tunashuhudia vipaji vikubwa vikitoweka duniani bila kitu. Lakini kuna vipaji vya kawaida vinaacha utajiri kama wote. Kuna wakati binafsi nashindwa kujua kitu kipi ana ‘kimasta’ zaidi Mondi. Uwezo wa kimuziki au kusimamia ‘ishu’ zake. Kote anaua!
Said Fella, Babu Tale na Sallam SK, wote ni wasimamizi wa mambo yake. Na kila mmoja anajua mipaka ya majukumu yake, kwa sababu nao wanasimamiwa vizuri na Diamond mwenyewe. Umeelewa?
Ubora wa Mama Dangote, menejimenti na Mondi mwenyewe katika kusimamia mambo, ndiyo unaoleta utulivu pale WCB licha ya mipunga kuingia kwa wingi kila uchwao. Pesa hazijawapa kiburi, ujinga wala uzembe. Bado wapo imara katika kusimamia, kuzitunza na kuzisaka zaidi. Kimsingi Mama Dangote anatufundisha kupambania, kujitoa kafara, kuziishi ndoto za watoto wetu na nyendo za utafutaji wao na kusimama nyuma yao kwa kila kitu. Yes! Hii dunia siyo ya muujiza, ni ya bidii na akili. Muziki wa Diamond Platnumz unavutia sana. Lakini mapambano ya mama mtu ndani ya mapambano ya mtoto mtu, ndio yanavutia zaidi. Sanura hajakutana na pesa za mtoto wake kwa bahati mbaya. Bali wengi wao wanaokutana naye kwa bahati mbaya na kumchukulia poa.
Bi Sandra kaweka alama flani ya juu sana kwa wazazi wengi kwenye huu muziki. Muziki ulipofikia kwa sasa, kuna kivuli kikubwa sana cha Bi Sandra. Kwani hakuna Diamond bila yeye. Aliyemleta Nasseb, ndiye yuleyule aliyemleta Diamond. Imani yake ileile akiwa kiumbe tumboni akitaka kutoka kuja duniani, ndiyo aliyokuwa nayo alipotaka kutoka kimuziki.
Mama aliamini na imani imemponya na njaanjaa za kidwanzi.