Ndani ya boksi: Njaa inaua vipaji na kuzalisha chawa mjini

Diamond. Hivi sasa anazalisha zaidi chawa kuliko vipaji. Wanamuziki walioondoka pale ‘Usafini’, nafasi zao zimejazwa na machawa. Yaani vipaji vinazibwa na machawa. Kwa nini? Endelea kusoma andiko hili uelewe;

Tumekuwa kama majuha. Ukitaka ubunge, au shavu lolote hapa ‘tauni’, tafuta umaarufu na ili ufikie huko anza uchawa. Jiweke pale ‘Usafini’ au ‘Kondeni’ kisha wasifie asubuhi mpaka usiku. Ukibaniwa huko. Msake Uwoya au Mobetto, jitoe ufahamu kwa kuwasifia kila siku mitandaoni kuanzia kula yao, vaa yao, ongea yao na kila kitu chao. Hapo ni dakika sifuri tu na wewe unakuwa ‘supa staa’.

Sasa chawa ni mchongo kwa vijana. Ni mwendelezo wa mabadiliko ya tabia fursa, tangu enzi za ‘mamisi’ wa wakati ule. Walipoachana na ‘umisi’ badala ya kugeukia uanamitindo wao wakageuka uigizaji? Hii pia ilikuwa ‘fasheni’.

Tafakari kwa kina. Kati ya uigizaji na mitindo ni kipi kilipaswa kuwa rahisi kwa ‘mamisi’? Ni wapi wangeweza kwa urahisi zaidi kama wangeamua? Ajabu ni kwamba wengi waliikataa mitindo na kuingia kwenye uigizaji.

Lilikuwa pepo, tena pepopunda kama siyo pepopundamilia kabisa. Kwani kila ‘Misi’ alitamani kuwa Monalisa, Elizabeth Michael, Johari Chagula. Na hata masela mitaani pia walitamani kuwa Kanumba, Ray au Hemed PhD.

Sio vibaya ‘Misi’ kuigiza. Hata India kuna waigizaji kibao waliowahi kuwa ‘Mamisi’ na wanafanya vizuri. Hapa hakuna tatizo. Ila tatizo lipo kwenye kustahili kuigiza. Urembo tu hautoshi kuwa muigizaji.

Ni kweli wanastahili kuwa waigizaji? Kati ya wote waliovamia uigizaji ni wachache sana walioonyesha kufiti. Ila wengi walileta ‘nuksi na sanaa yao kuyumba jumla. Uigizaji ni sanaa na kazi ngumu tofauti sana na ‘umiss’. Hapa ipo tofauti kati ya mwonekano na uigizaji. Unamkumbuka Kemmy? Yule mke wa Sembe katika mchezo wa ITV enzi zile katika ubora wao. Ni nani kama yeye kwa wale ‘mamiss’ walioamua kuvamia uigizaji?

Nani anafanya hata nusu ya kile alichotuonyesha? Wengi wanabaki kuwa warembo tu wanaoonekana runingani. Lakini vipaji vikiwa mbali na ukweli halisi. Kwa miaka kadhaa fani hii iligeuka ya ‘mamisi’ wastaafu.

Kwa sasa kuna kasi ya wanamuziki kimaendeleo kuliko waigizaji. Lakini sanaa ya uigizaji inafuatiliwa zaidi na Wabongo. Siyo kwa filamu, bali kwa tamthilia. Lakini tazama tamthilia za sasa, waandaaji na waigizaji wengi wao ni wasanii halisi. Wale machizi uigizaji kweli. Huoni mstaafu wa ‘umisi’ au mitindo kwenye kazi za sasa. Kifupi ‘gemu’ limesukwa na wenye nalo.

Kutokana na tamthilia kukusanya wasanii wengi. Lakini ni bora zaidi hivi sasa, kuliko wakati ule ambao fani ilivamiwa na wasio wasanii.

Hata kabla Bongo Movie hawajateka soko wakati ule. Waliwateka kwanza watu kupitia michezo ile ya kuigiza runingani. Kama waandaaji wa tamthilia hizi wataamini katika vipaji. Badala ya kuamini katika sura na jina, ni rahisi kurudi kwenye soko la filamu. Tena kwa kiwango cha juu zaidi kuliko enzi za kina Kanumba. Vipaji halisi ndio msingi wa filamu.

Wengi waliingia siyo kwa kuipenda sanaa ya filamu. Waliingia kwa kiu na njaa ya kutazamwa na wengi. Ni hilo tu. Ndio maana hakukuwa na ubunifu, hawakusonga mbele, zaidi ya fulani katoka na fulani. Wakati flani fani hii ilitia huzuni. Wapo waliokuwa na dhamira njema na vipaji vya kweli. Lakini walizidiwa na kundi la wauza sura lenye kujali mwonekano. Siyo kitu kibaya, ila vipi kuhusu vipaji na weledi? Vipi kuhusu mafunzo kwa jamii ambalo ni moja ya kusudio la sanaa?

Kwa kipindi kifupi tulipoteza vitu vingi. Maigizo ya uhalisia, vipaji vya uhakika. Kaole iliyowatoa Dr Cheni, Sinta, Swebe na kina Nora. Imebaki kuwa kumbukumbu nzuri tu.

Ukifuatilia tamthilia huko Azam na kwingine, bila shaka wadau wa sanaa ya uigizaji wameamua kuacha ujinga na kufanya kazi. Wanaamsha mizuka ya vijana mitaani kutamani kazi ya uigizaji, na wadau kuwekeza zaidi. Hii imekuwa ‘vaisi vesa’ kwa wenzetu wa muziki. Bongofleva kama muziki haukui, hausongi mbele wala kutoa makucha yake. Bongofleva imerudi miaka 20 nyuma. Ni wanamuziki wachache wanaoneemeka kati ya kundi kubwa. Wakati tamthilia wanapata kidogo. Lakini hicho kidogo ni cha wasanii wengi sana. Wale wa muziki wanapata kingi, lakini kinafika kwa wachache sana wanaopata kingi huku kundi kubwa likiishi kwa matumaini.

Wanaosifika kwa pato kubwa sana ni WCB. Lakini Harmonize alikimbia huko kwa sababu ya kulilia kipato. Ndicho kilichotokea kwa Mavoko na sasa Rayvvany. Kwa hiyo WCB kuna pato kubwa kwa mmoja tu? Chawa wanazingua.

Konde Gang ni sehemu ambayo pia huaminishwa kuwa kuna mawe sana. Leo hii Harmonize kabaki na Kajala wake. Vijana wake wote wamejikataa au kusepeshwa. Kwa nini? Mapene, mkwanja, faranga ni tatizo. Kumbe pia mmoja tu ndio ana mawe.

Ndivyo ilivyo kwa Kings Music. Kwa tafsiri ya wazi Alikiba na Kings Music yake ni moja ya maeneo huaminisha hadhira kuwa kuna neema sana. Ila ukiwatazama wasanii wa kando ya Kiba, akiwepo mdogo wake, huoni viashiria vya neema ya pesa. Ina maana Kings Music pia, mwenye neema ni mtu mmoja. Mpaka hapa ni bora waigizaji wengi wenye kidogo, kuliko wanamuziki wachache wenye kingi. Hivi sasa wanamuziki wawili watatu wanatanuka na kuacha pengo kubwa la mafanikio kwa wenzao. Umekuwa muziki wa mtu mmoja kuwa staa pekee kwa mwaka wa saba sasa? Kifupi muziki umekata ringi. Ila watu wachache ndio wako poa.Kuwatazama Dai, Kiba na Konde. Ni kama soka la Bongo kutawaliwa na Simba na Yanga tu. Tunawahitaji kina Mondi wa kutosha kwa ubora na kipato kama ilivyo kwa Wanaijeria. Bongofleva iko vilevile ila wanamuziki ni wachache wenye mafanikio. Kuona mafanikio ya muziki kupitia Mondi. Ni kama mafanikio ya soka letu kuyatazama kwa jina la Mbwana Samatta. Mondi kwenye tuzo nje ya nchi. Korido anapita kushoto yupo Salam, kulia Zuchu. Akipishana na wasanii wa Kinaijeria kama buku. Ndio maendeleo ya muziki hayo au ya Mondi kama Mondi? Matokeo yake ni nini? Ni kuzalisha chawa ambao walikuwa wanamuziki. Mafanikio anapata mmoja mpaka wenzake wanageuka chawa wake. Halafu chawa huyo anatutangazia mafanikio ya muziki wakati yeye anafanya uchawa badala ya muziki. Mafanikio hayo yameleta daraja la wasanii wenye njaa na wenye mafanikio. Na mwisho hutunga mimba ya upambe na matokeo yake ni kuzaa watoto machawa. Kelele za machawa huzalisha viumbe wavivu mitaani. Wanaoamini lolote kupitia kelele za uchawa. Na kutengeneza ukoo wa chuki kubwa. Na mwisho kama majuha Wabongo tunahalalisha uchawa kuwa ajira rasmi. Wanalipwa.