Ndani ya boksi: Wa 'Mondi nijibu nivimbe kitaa' Wanavyotengwa

Bob Marley’. Mtaa ‘ulimmaindi’ baada ya kununua mijengo ushuani Miami huko. Na kusepa ‘uswazi’ ya ‘Kingstone’. Kama vile Diamond na Tandale. Wana walikatika ‘stimu’ na kuona Bob ndio wale wale ‘Babiloni sistimu’. Walimchana Bob kinoma.

Bob naye aliwachana ‘masela lawama’ hao. Kwamba tunatafuta pesa ili tuhame huko. Sasa kama tunazisaka na kuzipata kisha tuendelee kulikita huko uswekeni. Basi hakuna haja ya kuzisaka. Yu noo? Stori ikaishia hapo.

Hii inahamia huku ‘dairekti au inidairekti’. Wanamuziki wengi wanatoka uswahilini. Ni vigumu kuona mwanamuziki mkubwa akitokea Masaki, Oysterbay, Mikocheni au hata Sinza. Wengi wametokea uswekeni haswa.

Watoto wa mtaa ndio wanaojua kufanya muziki na siyo kusikiliza. Wakishua wanajua kusikiliza na siyo kufanya.Wauswekeni ndio walioupeleka muziki ushuani. Toka enzi za Inspekta Harun na Juma Nature.

Pesa zilivyoingia kwa wingi, na hofu ya kuishi katika mazingira yaleyale ikawaingia.

Wakahamia sinzani, mbezini, Mikocheni na maeneo rafiki ya aina hiyo. Maeneo ambayo yana unafuu wa kuendana na zile balloon zao. Wapo waliobakia katika mitaa yao, lakini wengi wao walisepaa. Pesa za muziki ziliwaachanisha na mtaa.

Hawana kosa. Wakati enzi za Mwalimu ulitakiwa usome sana ili uishi Osterbay na kina Jaji Warioba, Daudi Mwakawago na kina Paul Rupia. Leo hii unatakiwa utafute sana pesa ili ukaishi Oysterbay jirani na Haji Manara.

Hata wasio wanamuziki huko uswekeni wanazichanga ili wakaishi ushuani. Ni utaratibu na akili za kawaida kabisa kwa watafutaji. Tunazisaka ili tuishi zaidi ya hivi tulivyo. Ingawa siyo tatizo ukipata na kulikita hukohuko uswekeni kwenu.

Lakini kuna tatizo naliona sijui ni mimi peke yangu au tupo wengi. Wanamuziki wanahama na kila kitu hivi sasa. Hata aina ya watu wa kuwaburudisha kwa shoo wamewahama jumla. Hivi sasa uswekeni wanaishia kusimuliwa tu.

Shoo zao hazipigwi kule uswekeni kwao. Wamehama jumlajumla. Hata Marioo naye kaamua kukiwasha ‘Mlimani Site’ kama kaka zake. Shoo za kule Mbagala na Goms hazipo tena. Kuna daraja la watu wetu linawatenganisha.

Tunafahamu aina ya watu wa ‘Mlimani Site’. Tunajua sampuli ya watu wa kutoa elfu hamsini. Siyo wale ‘wanaokomenti’ na kutupambania mitandaoni dhidi ya adui zetu. Siyo wale wanaohaha kutupigia kura kazi zetu mitandaoni.

Wanaojaa ‘Mlimani Site’ ni watu ambao wamekuta tu Mario ni maarufu. Ni wale waliomjua Mondi baada ya kudeti na Zari au ‘kolabo’ yake na Davido. Wamemjua Konde baada ya kusifiwa na Anko Magu. Hawana wanalojua kabla.

Wanaojaa ‘Mlimani Site’ ni wanaotaka kuwa zaidi ya Mondi. Wale wanataka Mondi awe juu zaidi. Abebe tuzo kila mwaka, huwezi kukutana nao ‘Mlimani Site’. Waliomnyanyua Dai au Konde Boy, ni wa shoo za buku tano au bure.

Wanaojaa ‘Mlimani Site’ ni watu wao wa ‘komplimentari’. Ambao ‘wakikomenti’ kwenye ‘peji’ ya staa yeyote wanajibiwa. Lakini waliowafikisha walipo, ni wale ‘wakikomenti’ husema ‘Mondi nijibu leo nivimbe mtaani’. Na hawajibiwi.

Wa ‘Mlimani Site’ hawawezi kuacha kazi zao. Wakampambania ‘YuTubu’ ili Konde Boy afikishe ‘vyuzi’ milioni moja kwa siku moja. Lakini ndio wanaopewa burudani zaidi kwa sasa. Kule uswekeni ni kama siyo hadhi yao tena.

Muziki una gharama sana, hasa sasa unahitaji pesa nyingi ili uwekeze vya kutosha. Ni lazima wasanii wapate faida kwa gharama wanazowekeza. Lakini hatufiki pale bila uwepo wa wale watu wetu wanaopiga ngoma zetu kwenye bodaboda na bajaji. Wale wanaoziimba nyimbo zetu siku hiyohiyo baada tu ya kuzitupia mjini ‘yutyubu’. Kwa sababu waliingia ‘yutyubu’ na kuutazama wimbo mara nyingi na kuukariri.

Wale ambao wanaweka bando la jero ili watupigie kura. Nao wanataka watuone ‘laivu’ kama walivyotuona Dar Live kule Mbagala na kutupenda. Kama walivyotuona Fiesta na kutuhusudu jumla jumla. Wanatuhitaji sasa tuwepo.

Tukiendelea na shoo za elfu hamsini hizi, ni dhahiri tumeamua kutengana na watu wetu. Ambao kimsingi ndio wenye huu muziki. Nao watafutiwe ‘lokesheno’ ya ‘kiloko’. Yenye gharama ndogo ili kuwapa burudani ‘laivu’.

Labda tusema tu ukweli. Misiba ya watu maarufu wanavyojaa siyo kwamba ndio wanatupenda sana. Ni wale mashabiki wanaojua hapo ndio sehemu pekee ya kuwaona ‘laivu’ Mbosso na Kiba wake. Kama siyo Bwakila. Tuendelee kupiga pesa za ‘mabishoo’ na ‘masista duu’ wa ‘Mlimani Site’. Wakati tunawaza pesa nyingi kulingana na nafasi zetu za kisanii. Pia tuwaze kuwa hatupo hapa tulipo kwa sababu ya wingi wa ndugu na ndevu. Tupo hapa juu kwa sababu ya watu wetu wa uswekeni huko. Wanahitaji faraja ya vipenzi vyao. Mchele shida, mafuta shida, maharagwe shida, nauli shida, pango shida, vikoba shida. Jamani hata kumuona msanii iwe shida? Wanamuziki acheni undezi wenu huo kawapeni faraja watu wa uswekeni hata mara moja kwa mwaka.

Muziki ni kwa ajili ya watu maskini, matajiri. Muziki ni kwa ajili ya wagonjwa na wendawazimu. Muziki ni kwa wafungwa na watawala. Muziki ni kila kitu na kwa kila mtu. Tuishi humo!