Tuheshimu tahadhari zitolewazo

Muktasari:

  • Kwa nyakati tofauti, viongozi dini wa makanisa tofauti nchini wametoa tahadhari kwa waumini wao dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa corona ambavyo vinaendelea kuua watu katika mataifa mbalimbali duniani.

Kwa nyakati tofauti, viongozi dini wa makanisa tofauti nchini wametoa tahadhari kwa waumini wao dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa corona ambavyo vinaendelea kuua watu katika mataifa mbalimbali duniani.

Tahadhari hizo zinalenga kuwaamsha waumini kuona umuhimu wa kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo hata kama ugonjwa huo haupo nchini au haujasambaa kiasi cha kutisha.

Tumeshuhudia Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga akitoa waraka wa tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya corona ambavyo vimezishambulia nchi kadhaa.

Pia, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo pamoja na Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, kwa nyakati tofauti wametoa tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Msingi mkuu katika hoja ya viongozi hawa wa dini ni kuwataka waumini wao kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona kwa kuzingatia kanuni bora za afya kama zinavyoelekezwa na wataalamu wa afya.

Hili siyo jambo la kupuuzwa hasa katika maeneo yanayohusisha mkusanyiko wa watu wengi kama vile makanisani. Huwezi kujua mwathirika wa ugonjwa huo ni nani na hata mwenye nao anaweza asijue kama ana maambukizi hayo.

Ni vema tukazingatia tahadhari hizo kwa kufanya mambo yanayoshauriwa na wataalamu wa afya kama vile kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka au kukaa mbali na watu hasa katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Pamoja na tahadhari hizo, tunaweza pia kutumia njia nyingine za kujitibu au kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo, kwa mfano, kupiga nyungu kama anavyohamasisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo.

Yapo majani au viungo vinavyoshauriwa kutumika kama tiba mbadala ya kunywa au kujifukiza ili kukabiliana na maradhi mbalimbali ikiwamo virusi vya corona ambavyo vimesababisha vifo vya watu zaidi ya milioni moja ulimwenguni kote.

Vita ni vita, haichagui silaha. Sisi pia tuko kwenye vita ya corona, hatutakiwi kuchagua silaha ya kutumia katika mapambano haya. Pia, hatutakiwi kupuuza silaha nyingine kwa sababu zinaweza kusaidia vizuri zaidi kuliko hata zile tunazoziamini.

Hapa nina maana kwamba tuchukue tahadhari zote kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka, kujitenga na watu, kupiga nyungu, kumuomba Mungu au kuwahi hospitali mara uonapo dalili za ugonjwa huo.

Tutambue kwamba ugonjwa huu upon a ni wajibu wa kila mmoja wetu kujilinda yeye mwenyewe na kuwalinda wengine kuanzia ndani ya familia, sehemu za kazi na maeneo mengine ya umma.

Tusiupe nafasi ugonjwa huu ukaharibu maisha yetu. Tupigane vita hii kama tulivyopigana na magonjwa ya zamani kama vile surua, pepopunda na ndui na tukayashinda, sasa siyo tishio tena kwa maisha yetu.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kutafuta taarifa sahihi kuhusu ugonjwa wa corona na kuchukua hatua za tahadhari mara moja ili kunusuru maisha yake na Taifa kwa ujumla.