Viongozi wa dunia walaani mapinduzi ya kijeshi Myanmar

Muktasari:

  • Zama za jeshi kushika hatamu za uongozi zimejirudia tena katika nchi ya Myanmar, na sasa jeshi la nchi hiyo juzi liliiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia katika mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji wa damu huku likimtaka kiongozi aliyechaguliwa, Aung San Suu Kyi kuachia madaraka huku likitangaza hali ya dharura kwa mwaka mmoja.

Zama za jeshi kushika hatamu za uongozi zimejirudia tena katika nchi ya Myanmar, na sasa jeshi la nchi hiyo juzi liliiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia katika mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji wa damu huku likimtaka kiongozi aliyechaguliwa, Aung San Suu Kyi kuachia madaraka huku likitangaza hali ya dharura kwa mwaka mmoja.

Mapinduzi hayo yamesitisha miaka kumi ya utawala wa kiraia, huku jeshi likihalalisha kitendo chake kwa kutuhumu kuwa uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba ambao chama cha Suu Kyi cha National League for Democracy (NLD) kilipata ushindi mkubwa, ulijaa wizi na udanganyifu.

Hatua hiyo ya jeshi imesababisha jumuiya ya kimataifa kulaani kitendo hicho, huku Marekani ikitoa wito kutaka demokrasia irejeshwe haraka.

Suu Kyi na Rais Win Myint walikamatwa wakiwa mji mkuu wa nchi hiyo wa Naypyidaw juzi jioni, msemaji wa chama chao, Myo Nyunt aliiambia AFP saa chache kabla ya Bunge kuitishwa kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu ufanyike.

Jeshi lilifunga barabara kuzunguka mji mkuu wa Naypyidaw kwa kuweka wanajeshi, malori na magari yenye silaha. Pia, helikopta za jeshi zilikuwa zikizunguka anga la jiji hilo kufanya doria na kudhibiti aina yoyote ya ghasia za wananchi.

Hata hivyo, haijafahamika wazi hatua hiyo ya jeshi itachukua muda gani huku shinikizo la jumuiya ya kimataifa likizidi kuongezeka kwa kulitaka jeshi hilo kurejesha utawala wa kiraia uliochaguliwa na wananchi.

Umoja wa Mataifa (UN), Marekani na mataifa mbalimbali ulimwenguni yamelaani mapinduzi hayo ya kijeshi nchini Myanmar, huku yakitoa wito wa kurejeshwa kwa utawala wa kidemokrasia na kuachiwa huru kwa Suu Kyi na wanasiasa wenzake.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres naye amelaani vikali kushikiliwa kwenye mahabusu za kijeshi kwa Aung San Suu Kyi, Rais Win Myint na viongozi wengine wa kiraia kufuatia mapinduzi hayo ya kijeshi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la DW, msemaji wa Katibu Mkuu huyo, Stephane Dujarric alisema matukio haya “yanaashiria pigo kubwa kwa mageuzi ya kidemokrasia” nchini Myanmar.

Msemaji wa Ikulu ya White House, Jan Psaki alisema kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari na umma wa nchi hiyo kwamba Marekani itachukuwa hatua kali dhidi ya wale waliohusika na mapinduzi hayo endapo hawataurejesha haraka utawala wa kiraia.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, Marekani haikubaliani na jaribio lolote la kuyapindua matokeo ya uchaguzi wa Novemba ambao ulikipa chama cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi ushindi mkubwa kabisa, lakini ukakumbwa na tuhuma za wizi wa kura.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken naye pia alitoa tamko rasmi kulitaka jeshi la Myanmar kuwaachia huru maofisa wote wa serikali na asasi za kiraia waliowakamatwa pamoja na kuheshimu matakwa ya watu wa Myanmar kupitia uchaguzi wa Novemba 8.

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen naye alilaani mapinduzi hayo ya kijeshi na pia kutoa wito wa kuachiliwa kwa watu wote wanaoshikiliwa.

“Serikali halali ya kiraia inapaswa kurejeshwa kwa kuzingatia katiba ya nchi na uchaguzi wa Novemba,” aliandika Rais huyo wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kabla ya mapinduzi hayo ya Januari 29, Marekani pamoja na mataifa mengine ya Magharibi yalitoa tamko la pamoja kulitaka jeshi kuheshimu utamaduni wa kidemokrasia, kufuatia kitisho kilichotolewa na mkuu wa majeshi ya Myanmar kwamba angelisitisha kutumika kwa katiba ya nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amelaani mapinduzi hayo na kushikiliwa kwa Aung San Suu Kyi. Kupitia ujumbe wake wa Twitter alisema: “Kura ya wananchi lazima iheshimiwe na viongozi wa kiraia waachiliwe.” China ambayo kawaida hupinga uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar, imetaka pande zote kutatuwa mkwamo uliopo.

“China ni jirani na rafiki wa Mnyanmar na tunarajia pande mbalimbali zinazohusika na mgogoro huu kuutatuwa kwa kufuata Katiba na sheria za nchi yao ili kulinda utulivu wa kisiasa na kijamii,” alisema msemaji wake wa mambo wa kigeni, Wang Wenbin, kwenye taarifa yake ambapo kauli kama hiyo imetolewa pia na Japan, Uturuki, Canada, Singapore na Norway.

Hadi kufikia jana, hakukuwa na taarifa za majaliwa ya Aung San Suu Kyi na wenzake walioshikiliwa, kuachiwa huru.