Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waandishi ni madaktari au wafinyanzi?

> Wanahabari wakiwa kazini .Kundi hili lisipokuwa makini linaweza kuharibu jamii.Picha na maktaba.

Muktasari:

Kama ni kuwachambua wengine, utaandika kwa haraka na wakati mwingine kwa maneno mazito.

Ni kazi kubwa kufanya uchambuzi juu ya kitu kinachokugusa au kazi unayoifanya wewe mwenyewe.

Kama ni kuwachambua wengine, utaandika kwa haraka na wakati mwingine kwa maneno mazito.

Hata hivyo, mambo yakigeuka ukalazimika kujichambua wewe mwenyewe, kigugumizi kinaishika mikono!

Najaribu kuifanya kazi hii kwa manufaa yetu sote, maana kazi ya kulijenga Taifa letu ni yetu sote. Tutafanikiwa kulijenga, tukianza kujigeukia sisi wenyewe na kujihoji.

Wanasiasa, viongozi, wataalamu, wasomi na viongozi wetu wa dini wajihoji. Kwa namna hii tunaweza kupiga hatua kuelekea maendeleo ya kweli. Mimi ni mwandishi, hivyo nitageukia uandishi!

Waandishi wa habari

Tunaandika na kuchambua masuala mengi katika jamii yetu. Tunaandika juu ya siasa na wanasiasa; tunawapamba wanasiasa na kuwatukuza, tunawapamba hata majambazi, wazembe, mafisadi; tunawasafisha kwa kalamu zetu.

Tunazitumia kalamu zetu kuandika mema na mabaya. Bila kutilia maanani kwamba kalamu zetu zinaweza kulijenga Taifa au kulibomoa. Tunapoelekea Uchaguzi Mkuu, watu wanajiandaa kutengeneza fedha kwa kalamu zao. Wanajiandaa kuandika ukweli na uongo, ili kuwatukuza viongozi wanaotamani kuingia madarakani.

Kalamu inaweza kuisambaratisha siasa na hasa kama ni siasa mbaya, lakini pia kalamu inaweza kuijenga na kuiimarisha siasa iwe mbaya au nzuri. Kalamu ni silaha ya hatari.

Bila kuitumia kwa hekima na busara, inaweza kuleta maafa makubwa katika jamii yoyote ile. Na kwa upande wetu Tanzania, bila kuzitumia kalamu zetu vizuri, kuna hatari ya hapo baadaye kulia na kusaga meno.

Wengine wanasema kilichoandikwa kimeandikwa! Hivyo mwandishi kabla ya kuandika ni lazima awe makini. Ni lazima kufanya utafiti na kuhakikisha anaandika ukweli, maana kilichoandikwa kitasomwa vizazi na vizazi.

Maandishi mengine yanaweza kuleta mwanga katika jamii na kuwasaidia walio wengi, lakini maandishi mengine yanaweza kuleta giza na kuwachanganya watu.

Waandishi wa habari, waandishi wa vitabu na wachambuzi wa masuala mbalimbali katika jamii, lazima wawe makini wanaposhika kalamu na kuandika au wanapotumia vyombo vya kisasa kuandika.

Waandishi wengine na hasa waandishi wa vitabu ni vigumu kuwaelewa haraka, wengine wanatumia mafumbo au wanaficha ujumbe wao kwenye majina ya wahusika, au maneno ambayo ni lazima kufikiri na kuyatafakari ili mtu aupate ujumbe husika.

Siku za nyuma nilipokuwa nikisoma vitabu vya Ngugi wa Thiong’o, daima nilihisi maana au ujumbe mzito kwenye majina ya wahusika wakuu katika vitabu hivyo. Inawezekana pia ni kwa vile Ngugi, daima anaanza kuandika kwa Kikuyu na baadaye ndipo maandishi yake yanatafsiriwa kwenye lugha nyingine.

Kuna wakati nilitamani kujifunza lugha ya Kikuyu, ili niweze kupata ujumbe mzima kwenye vitabu vya mwandishi huyu maarufu duniani. Kwa mfano, Ngugi anapenda kutumia majina kama Muriuki, Guthera na mti wa Miiguno.

Mwaka 1989, nilipata bahati ya kukutana na Ngugi jijini Dar es Salaam. Swali langu la kwanza kwake nilitaka kujua maana ya majina anayopenda kutumia mara kwa mara, katika vitabu vyake. Bahati mbaya hatukuwa na muda wa kutosha. Aliweza kunielezea maana ya jina moja tu; Matigari na Njiruungi.

Wakati huo Matigari kikiwa kitabu chake kipya. Ilikuwa shida kukipata kitabu hicho katika nchi zetu za Afrika wakati ule, kutokana na maelezo ya Ngugi mwenyewe, Matigari (kitabu) na Matigari (mhusika mkuu kwenye kitabu) na mwandishi wa kitabu hicho, walikuwa wakiishi uhamishoni, wakimbizi wa kisiasa.

Kwa ufundi wa kuandika alionao Ngugi, mhusika mkuu wa kitabu chake alitokea kuwa mtu anayeishi na askari wa Kenya, wakaamini mtu huyu yupo na alikuwa akizunguka nchi yote ya Kenya.

Waliamua kumtafuta kila kona ya Kenya na kuishia kuvikusanya vitabu vyote vya Matigari na kuvichoma moto! Baadaye nilibahatika kukipata kitabu cha Matigari mwaka 1990 mjini Amsterdam. Nikakisoma na kukutana na Matigari na Njiruungi.

Ngugi anaeleza maana ya jina Matigari na Njiruungi, kwamba ni wale waliopigana wakati wa vita ya kumfukuza mkoloni, ni wazalendo, mashujaa wa vita waliopigana kufa na kupona kumfukuza mkoloni; lakini pia ni wale wasiofurahishwa na jinsi mambo yalivyoendeshwa baada ya uhuru, rushwa, kupora mali, upendeleo, uonevu, kuiga maisha ya mkoloni, ubepari, ukabila, kuuza nchi, chuki na ukabila.

Matigari na Njiruungi, ni wale wanaoutafuta ukweli na haki katika nchi huru za Afrika. Kadri wanavyohoji juu ya haki na ukweli, ndivyo wanavyofungwa na kuishi uhamishoni na pengine kuyapoteza maisha yao.

Waandishi wote wana namna ya kutumia vitu mbalimbali kutoa ujumbe katika jamii, wengine wanatumia majina yanayobeba ujumbe mzito. Wengine wanatumia mifano mbalimbali, mara nyingi inategemea ujumbe unakwenda kwa jamii ipi.

Daktari na mfinyanzi

Mwaka 1984, kule Munchen, nchini Ujerumani nilipata bahati ya kuhudhuria mhadhara wa mwandishi maarufu wa nchi hiyo, Gunter Grass. Huyu alikuwa akitoa ujumbe kwa Wajerumani wenzake kwa kutumia hadithi fupi ya daktari na mfinyanzi.

Daktari na mfinyanzi ni watu wawili wenye kazi zinazotofautiana. Gunter alieleza kwamba siku moja daktari alifanya mkataba na mfinyanzi, alitaka mfinyanzi amtengenezee (kufinyanga) sanamu ya marehemu mke wake.

Baada ya maelezo na bei, walipatana kwamba kazi hiyo ingechukua miezi mitatu. Baada ya miezi mitatu, daktari alikwenda kwa mfinyanzi kudai sanamu yake. Lakini kwa mshangao mkubwa mfinyanzi ndiyo kwanza alikuwa anaianza kazi hiyo.

Kazi ya miezi mitatu ikachukua mwaka na zaidi. Baadaye daktari alichukia na kutishia kukatisha mkataba. Mfinyanzi hakukasirika, bali alimjibu daktari kwa upole:

“Daktari! Kazi zetu zinatofautiana, wewe ni daktari, unawatibu watu, wengine wanapona na wengine wanakufa. Wewe ukifanya kosa wakati wa upasuaji, tena kosa la uzembe, mtu anakufa. Na mtu akifa, kaburi linayaficha makosa yako!

Hakuna mtu atakayejitokeza baada ya miaka miwili au mitatu na kukuhukumu juu ya kosa lako. Kaburi linakulinda daima. Lakini mimi nikifanya kosa la ufundi, kosa la kutokuwa makini, nikatengeneza sanamu mbaya, kumbuka sanamu inadumu vizazi hadi vizazi, hivyo nitahukumiwa kwa kosa la kutokuwa makini wakati wa kutengeneza sanamu. Hivyo ni lazima kazi yangu ya ufinyanzi niifanye polepole na kwa umakini zaidi”.

Baada ya hadithi hii fupi, umati wote ulimshangilia Gunter. Ninasikia baadaye alipata nishani ya juu kwa hadithi hii fupi. Waafrika tuliokuwepo kwenye mhadhara huo, hatukuguswa na mfano huo, lakini baada ya kuelezwa kwa undani, tulijikuta tukiiunga mkono.

Kazi ya kuijenga jamii, kulijenga Taifa ni lazima kufanywa polepole na kwa umakini kama vile mfinyanzi anavyotengeneza sanamu. Sanamu inabaki vizazi hadi vizazi.

Hakuna kaburi la kuficha maovu ya jamii yoyote ile, jamii iliyopita, iliyopo sasa na ile ijayo, sanamu inabaki vizazi hadi vizazi. Jamii, kama sanamu, ni muhimu kuifinyanga kwa umakini mkubwa. Ni sharti kuijenga jamii kwa umakini mkubwa.

Tuna imani kwamba lengo la waandishi ni kulijenga Taifa. Hivyo ni muhimu kuifanya kazi yao kwa uangalifu kama ule wa mfinyanzi. Maana maandishi yanabaki milele kama sanamu. Hakuna kaburi la kuficha makosa ya mwandishi.

Tunawaandika wengine, tunawachambua wengine, lakini ni muhimu pia kujigeukia sisi wenyewe. Pia, tukikumbuka kwamba uandishi wetu ni sehemu ya ujenzi wa Taifa letu.

Tujipime, sisi ni kama madaktari ambao endapo wakifanya kosa, kaburi linaficha siri zao au tuko kama mfinyanzi ambaye kama hajafanya kazi vizuri, sanamu yake itamshitaki vizazi hadi vizazi?