WanaCCM wanaoutamani urais 2025 wamesahau desturi?

Muktasari:

  • MNEC adai watanawa lakini hawatakula

Historia, utamaduni na asili ya CCM ni Rais na Mwenyekiti aliye madarakani mwenye nia ya kugombea kupewa nafasi hiyo bila kupingwa; kama kuna wana CCM watajitokeza kuchuana na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2025 tutawakumbusha historia, utamaduni na asili hiyo. Kifupi naweza kusema watanawa lakini hawatakula.”

Hiyo ni kauli ya mjumbe wa NEC ya CCM Mkoa wa Mwanza, Jamal Babu alipozungumza na Mwananchi kuhusu taarifa za kuwepo wana CCM wanaofikiria kuchukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho tawala kuwania urais uchaguzi mkuu ujao mwaka 2025.

“Wahenga walitufundisha kuwa mwacha asili ni mtumwa; asili yetu CCM ni Rais na Mwenyekiti aliye madarakani anayeruhusiwa kugombea kikatiba kutopingwa iwapo akionyesha nia ya kufanya hivyo. “Kamwe CCM hatuwezi kukubali kuwa watumwa kwa kuacha asili yetu. Muda ukifika sote tutakumbushana asili yetu hiyo kwa kumpa fursa Rais Samia,” alisema Babu.

Mjumbe huyo wa NEC aliwashauri mawaziri na viongozi wa CCM kutumia muda na nafasi zao kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na ahadi za CCM mwaka 2020 badala ya kufikiria nafasi ya urais mwaka 2025.

“Ilani na ahadi za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 tayari imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 95 ndani ya kipindi cha miaka miwili, ni vema wana CCM wote tuelekeze nguvu na kujikita kwenye utekelezaji wa Ilani na ahadi zetu kwa wananchi, ili kurahisisha kampeni uchaguzi ujao,” alisema.

Kauli ya MNEC huyo imetokana na joto la uchaguzi wa mwaka 2025 unaoendelea kupanda ndani ya Serikali na CCM kutokana na taarifa za kuwepo viongozi na wanachama wanaoendesha kampeni na harakati za chinichini kujiimarisha kwa kinyang’anyiro cha kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika nafasi ya urais katika uchaguzi huo.

Joto hilo limeendelea kupanda licha ya viongozi wa kitaifa wa Serikali na chama, akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka kuutangazia umma hadharani kuwa Rais Samia ndiye mgombea wa CCM mwaka 2025.

Ipo video ya hivi karibuni iliyosambaa kupitia mitandao ya kijamii ikimkariri Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila kuwa wapo baadhi ya vigogo, wakiwemo mawaziri wanatamani kiti cha urais mwaka 2025.


Kujiua kisiasa

Akizungumzia madai ya baadhi ya wanasiasa ndani ya CCM kuutamani urais mwaka 2025, Mdhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo alisema vyovyote iwavyo, ni kujitafutia ‘kifo’ kisiasa kufikiria kukabiliana na Rais na Mwenyekiti aliye madarakani.

“Ni political suicide (kujiua kisiasa) kufikiria kupambana na Rais na Mwenyekiti wa chama aliye madarakani mwenye nia ya kugombea; kiuhalisia hakuna fursa kama hiyo kwa mujibu wa utamaduni ndani ya CCM,” alisema Profesa Kinyondo ambaye ni mchumi mbobevu.

Alisema yawezekana baadhi ya vigogo ndani ya CCM kudaiwa kujipanga kuwania kuomba ridhaa ya kugombea urais mwaka 2025 ni mbinu za kupima kina cha maji kuona iwapo Rais Samia bado yupo au ataondoka mwaka 2025, huku akionya kuwa majaribio ya aina hiyo ni hatari iwapo aliye madarakani ana nia ya kugombea.

“Hizi zinaweza kuwa ni chokochoko za kupima kina cha maji… zina hatari ya kifo cha kisiasa iwapo watatumia miguu yote miwili kujaribu kina cha maji,” alisema Profesa Kinyondo.

Aliongeza; “Japo ni kawaida kisiasa kupima iwapo Rais Samia bado yupo au ataondoka mwaka 2025; ni hatari kisiasa wanaopima kina cha maji kuendeleza harakati zao hata baada ya Rais aliye madarakani kuonyesha au kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo.”


Awamu mbili

“Wanaosema Rais Samia amemaliza muda wake wa awamu mbili kwa sababu ameshiriki uongozi wa juu kwa kuwa Makamu wa Rais tangu mwaka 2015 na baadaye Rais kuanzia Machi mwaka 2021 wanakosea sana, kwa sababu yeye ni Rais anayemalizia muda wa mtangulizi wake. Rais Samia hajagombea urais; alikuwa mgombea mwenza,” alisema Profesa Kinyondo.

Akitoa mfano wa nchi ya Zambia, mwanazuoni huyo alisema; “akitumia hoja za aliyekuwa Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu aliyeingia madarakani baada ya kifo cha mtangulizi wake, Michael Satta, Rais Samia anaweza kudai kuwa mwaka 2025 ndio awamu yake ya kwanza kugombea na hivyo kuwania tena nafasi hiyo mwaka 2030.”

Mhadhiri wa zamani wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Onesmo Kyauke alisema haoni namna yoyote ya CCM kukiuka utamaduni wake wa Rais na Mwenyekiti aliye madarakani kupewa fursa ya kugombea bila kupingwa.


Mawaziri kumkabili Rais

“Ni kukosa nidhamu iwapo kweli wapo mawaziri ndani ya Serikali wanaotamani urais na kufikiria kufanya kampeni kutaka nafasi ya aliyewateua; hii haikubaliki na ikithibitika kwa ushahidi hakuna namna nyingine zaidi ya kumwondoa mhusika kutoka ndani ya Serikali,” alisema Dk Kyauke.


Wana CCM kumpigania Rais Samia

Akizungumza kwa tahadhari na kuchagua maneno, Dk Maua Daftari ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe waliowahi kushika ndhifa mbalimbali ndani ya chama na Serikali, alisema ni haki kwa mwanachama yeyote kutamani kugombea urais, lakini wana CCM watatumia nafasi yao kidemokrasia kumpigania Rais Samia iwapo ataomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama.

“Kama wapo wana CCM wanaofikiria wanafaa kugombea urais ni ruksa waje; lakini sisi tunaomwamini Rais Samia ambaye kwa kipindi kifupi alichoongoza amefanya mengi ya kupigiwa mfano, tuna wajibu wa kumpigania kuhakikisha anapata fursa ya kupeperusha bendera ya CCM iwapo ataonyesha nia 2025,” alisema Dk Daftari.


Mshangao ndani na nje ya CCM

Anna Abdallah, mwanasiasa mkongwe, waziri na mjumbe wa zamani wa Kamati Kuu ya CCM alisema iwapo kuna wana CCM watajitokeza kutamani na kuomba ridhaa ya kugombea Urais uchaguzi mkuu ujao, watashangaza si tu ndani ya chama hicho tawala, bali hata nje ya chama kwa sababu si utamaduni, desturi na mila ya CCM Rais na Mwenyekiti aliye madarakani kupingwa.

“Kikatiba ni haki ya kila mwana CCM kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama; lakini hatuna utamaduni wa kushindana na Rais na Mwenyekiti aliye madarakani iwapo ataonyesha nia ya kugombea. Wakijitokeza wana CCM kugombea urais 2025 watashangaza watu ndani na nje ya CCM,” alisema Mama Anna Abdallah.

Mkongwe huyo alisema hata wakijitokeza na kuchukua fomu, watu hao hawatafua dafu mbele ya Rais Samia kutokana na historia yake ya uongozi na mambo aliyoyafanya kwa kipindi chake tangu Machi 19, 2021.

“Nimekuwa waziri kwa vipindi tofauti, hatukuwahi kupata fedha za maendeleo na kujiendesha kwa kiwango cha sasa chini ya uongozi wa Rais Samia. Kwa maoni yangu (Rais Samia) anatosha na katiba inamruhusu kugombea. Kama wapo wenye nia ya kugombea naye watashangaza hata wasiokuwa wana CCM,” alisema Mama Anna Abdallah.