Wiki ya sheria yamalizwa na kilio cha Katiba Mpya

Juzi, Tanzania iliadhimishwa Siku ya Sheria wakati kukiwa na malalamiko mengi ya wadau mbalimbali kuhusu utawala wa sheria katika Taifa hili ambalo kwa miaka mingi limejipambanua kwa siasa zake za demokrasia inayokuwa.

Muktasari:

  • Juzi, Tanzania iliadhimishwa Siku ya Sheria wakati kukiwa na malalamiko mengi ya wadau mbalimbali kuhusu utawala wa sheria katika Taifa hili ambalo kwa miaka mingi limejipambanua kwa siasa zake za demokrasia inayokuwa.

Juzi, Tanzania iliadhimishwa Siku ya Sheria wakati kukiwa na malalamiko mengi ya wadau mbalimbali kuhusu utawala wa sheria katika Taifa hili ambalo kwa miaka mingi limejipambanua kwa siasa zake za demokrasia inayokuwa.

Pia, madai ya Katiba mpya yamechukua nafasi katika maadhimisho ya wiki ya sheria ambapo, wanasiasa na wanaharakati mbalimbali wamezungumzia nafasi ya Katiba mpya katika utawala bora unaozingatia sheria.

Nchi hii kama zilivyo nchi nyingine duniani, inayo Katiba yake ambayo ndiyo sheria mama inayoongoza na kuweka misingi ya utawala na jinsi Watanzania watakavyoendesha maisha yao katika nchi yao bila kuingiliwa na mataifa mengine.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeweka mgawanyo wa majukumu kwa viongozi wa kitaifa pamoja na mihimili mitatu ambayo kila mmoja unapaswa kufanya kazi kwa kujitegemea.

Licha ya shinikizo la mabadiliko ya Katiba kutoka kwa wanaharakati na wanasiasa mbalimbali nchini, bado Katiba hiyo ya mwaka 1977 ndiyo inatumika huku ikiwa inafanyiwa mabadiliko madogo mara kadhaa.

Hata hivyo, changamoto kubwa imekuwa kwenye utekelezaji wa matakwa ya Katiba hiyo pamoja na sheria mbalimbali zilizopo, jambo ambalo limekuwa likisababisha sintofahamu na kuacha pengo na vilio kwa wananchi katika upatikanaji wa haki zao za kisheria.

Licha ya kuwa wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya sheria, wengi wao hujliuta wakipoteza haki zao kwa sababu hawajui namna ya kufuatilia haki hizo kwenye vyombo husika.

Wiki iliyopita, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma aliwahimiza wananchi kutembelea mabanda ya Mahakama katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria ili kujifunza kwa kiasi gani Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki kwa ufanisi kwa matumizi ya Tehama.

Jaji Mkuu alisema katika mabanda hayo inatolewa elimu ya taratibu za ufunguaji wa mashauri, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri ya ndoa na talaka, utekelezaji wa hukumu, sheria za watoto na taratibu za mashauri ya mirathi.

Licha ya jitihada zinazofanywa na Mahakama kuelimisha wananchi kupitia wiki ya sheria, wanasiasa nao wamekuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa sheria zilizopo, jambo ambalo linawanyima haki wananchi.

Pia, mchakato wa kupata Katiba mpya ulikwamishwa na wanasiasa kutokana na sababu mbalimbali, hata hivyo, wadau wanasema bado kuna umuhimu wa kupata Katiba mpya ili kuleta haki, usawa na uwajibikaji.

Wakizungumzia katika Siku ya Sheria, wadau mbalimbali wanasema umefika wakati sasa kwa nchi kurejesha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya ambao ulikwama.

Wanasema hilo litasaidia kumaliza changamoto zingine zinazojitokeza kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alimkumbusha Rais John Magufuli kutimiza ahadi yake ya kumalizia mchakato wa Katiba mpya aliyoitoa wakati wa hotuba yake ya kufungua Bunge, Novemba 2015.

Profesa Lipumba aliyasema hayo juzi Februari Mosi jijini Dodoma baada ya kupewa nafasi na Rais Magufuli kuzungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama ya Tanzania.

Mwanasiasa huyo mkongwe alisema katika hotuba aliyoitoa, Rais Magufuli alisema amelipokea suala la Katiba mpya na kwamba atalitekeleza kabla hajamaliza muda wake wa uongozi ili Watanzania wapate Katiba yao.

Alimweleza Rais Magufuli kwamba amezungukwa na watu ambao walikuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na akihitaji vitendea kazi, vipo vya kutosha kabisa.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala anasema kuna madai ya muda mrefu ya Katiba mpya. Madai hayo yanalenga kuwa Katiba hiyo ije iendane na mfumo wa vyama vingi uliopo sasa hapa nchini.

Anasema Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alianzisha mchakato wa Katiba mpya lakini haukufanikiwa kwa sababu rasimu bora iliyopatikana, haikupitishwa katika Bunge Maalumu la Katiba (BMK).

“Wiki hii itukumbushe kuwa bado tunahitaji Katiba mpya ambayo ndiyo sheria mama. Tuendelee kudai Katiba mpya kwa sababu ndiyo maisha yetu ya kila siku,” anasema Profesa Mpangala.

Mwanazuoni huyo anasema sheria nyingine pia ziangaliwe kwa sababu zipo ambazo ni kandamizi na zinawanyima watu haki zao za kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Anatoa angalizo kwamba uhuru wa Mahakama nao uangaliwe ili wananchi wawe na imani na mhimili huo.

“Kila muhimili unatakiwa utekeleze majukumu yake. Wiki hii ya sheria wadau walitafakari kwa kiasi gani mihimili hasa Mahakama na Bunge iko huru,” anasema Profesa Mpangala.

Mchambuzi wa siasa, Andrew Bomani anasema nafasi ya Katiba imepuuzwa hapa nchini ndiyo maana kila mtu anafanya mambo bila kufuata matakwa ya Katiba ya nchi ambayo ndiyo msingi wa sheria zote.

“Kila siku tunafikiria sheria tu lakini tunasahau sheria mama, Katiba. Nchi hii lazima tuamue kwamba Katiba mpya ni kipaumbele, hakuna haja ya watu kukwepa hilo suala,” anasema Bomani.

Bomani ambaye pia ni kada wa chama cha UDP, anasema vyama vya siasa pia vinatakiwa kusimamiwa kwa mujibu wa sheria ili visijiendeshe kama Taasisi za watu binafsi bali kama Taasisi za umma. Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea, Rashid Twaha anasema changamoto iliyopo nchini ni utungaji wa sheria ambazo zinaangalia maslahi ya watawala, hivyo, utekelezaji wa sheria hizo unasababisha maumivu kwa wananchi.

Anasema suala la utawala bora na utawala wa sheria unategemea kwa kiasi kikubwa utashi wa kisiasa wa watawala wa nchi yoyote.

Bila watawala kuwa na utashi huo, ni vigumu kupata sheria bora na utawala wa sheria.

“Watawala ndiyo wanaanzisha miswada ya sheria, wao ndiyo wanaitetea mpaka inapita na wao ndiyo wanakwenda kuitekeleza.

Wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko katika eneo hili,” anasema mwanasheria huyo.

Pia, anasema Katiba mpya nayo inahitaji kufanyiwa mabadiliko kwa sababu wananchi wanahitaji.

Anasisitiza kwamba Katiba mpya inahitaji maridhiano kama Taifa na siyo jambo la mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu kukaa na kutoa uamuzi.