Unatamani kuacha kuvuta sigara?

Friday January 01 2021
sigara pic
By Chris Peterson

Nimejaribu kufanya tafiti ndogo ya kuongea na wavutaji mahiri wa sigara, wanakiri kwamba kama wasingethubutu kujiingiza katika tabia hiyo, wangerudisha muda wao nyuma ili wasivute sigara.

Uvutaji wa sigara unachochea mazingira hatarishi ya magonjwa ya moyo, saratani ya mapafu, kifua kikuu, saratani ya damu na pia kupoteza nguvu za jinsia hasa kwa wanaume. Cha kuhuzunisha magonjwa haya yote ni rafiki wa karibu wa wavutaji sigara na tafiti zinaonyesha zaidi ya nusu ya wavutaji wa sigara wanakufa mapema kutokana na kitendo hiki. Kwa umekuwa mtumwa wa kuvuta sigara, hujachelewa kuchukua uamuzi wa kuacha kuvuta sigara na utapata manufaa makubwa kiafya kutokana na kuacha kuvuta sigara ndani ya mwaka wa kwanza.

Kama utakuwa tayari ni mwathirika wa magonjwa yatokanayo na uvutaji wa sigara, kuacha uvutaji wa sigara kutasaidia kuzuia hali ya afya yako kuwa mbaya zaidi.

Kwa kusoma makala haya ni hatua ya mwanzo na tayari umeshaanza kuichukua. Kinachofuata ni kutafuta mtu anayeweza kukusaidia katika kampeni hii binafsi ya kuacha kuvuta sigara.

Siku hizi kuna maelfu ya huduma za kusaidia kuacha uvutaji wa sigara. Wahudumu wa afya pia tupo mstari wa mbele katika hili; tunakupatia tiba na ushauri. Tunaanza kufuatilia hali ya tabia yako ya uvutaji, ndipo tunajua tiba sahihi itakayokufaa lakini baada ya kukufanyia vipimo kujua ni kwa kiasi gani tatizo hili limekuathiri kimwili na kiakili. Uvutaji wa sigara ni vyema ukatambulika kuwa ni uraibu kama vilivyo vilevi vingine na sio rahisi kuacha kutokana na uraibu huo. Hivyo ni vyema kwenda kwenye vituo vya ushauri na matibabu ya dawa za kulevya na hapo utakutana na washauri wa magonjwa ya akili na dawa za kulevya ikiwamo hili la uvutaji wa sigara.

Watakupa ushauri wa kisaikolojia, namna ya kupambana na matamanio ili usivute tena sigara.

Advertisement

Kama nilivyotangulia kusema awali, suala la kuacha uvutaji wa sigara ni gumu. Ni jambo linalopaswa kupatiwa tiba lakini bado msaada wa kisaikolojia unahitajika kutoka kwa watoa huduma za afya. Na msaada huu wa kisaikolojia unahitajika mara kwa mara kwa mwathirika wa sigara. Habari njema ni kwamba siku hizi watoa huduma za dawa hasa wafamasia kwa kushirikiana na madaktari na wanasaikolojia wapo tayari kukusaidia kwa namna yeyote wakati wowote, mahali popote.

Makala haya yameandikwa na daktari wa binadamu

Advertisement