Upatikanaji maji hafifu unavyoumiza wanawake

Muktasari:

  • Vuta picha wewe ni mama wa watoto watano wanaotakiwa kwenda shuleni asubuhi.

Vuta picha wewe ni mama wa watoto watano wanaotakiwa kwenda shuleni asubuhi.

Lakini unapoamka alfajiri, kumbe ndani umebakiwa na maji kwenye ndoo ya lita 10; unaumiza kichwa hayo maji ugawe vipi ili watoto wasiende shule bila kuoga na nyumbani ubakiwe na akiba kidogo.

Wakati unawaza hilo ndani kuna nguo chafu, choo hakijapigwa deki, hujapika chai watoto wapate kifungua kinywa na hujui utapata wapi maji kwa ajili ya kuandaa chakula.

Kwa kifupi tangu maji yatoke wiki iliyopita hayajatoka tena na hujui yatatoka lini, huku gharama ya ndoo moja ya maji kwa wenye visima yanauzwa Sh500.

Haya ndiyo maisha yanayozikabili familia nyingi katika kipindi hiki cha ukame ambacho kimesababisha vyanzo vya maji kukauka, huku wanawake wakiwa watu wa kwanza kukumbana na changamoto hiyo.

“Nyumbani kwangu maji ni shida, natumia Sh4,800 kila siku kununua ndoo sita za maji, ndoo moja nanunua kwa Sh800,” anasema Habiba Juma, mkazi wa Sinza.

Habiba ambaye familia yake ina watu sita, anasema ndoo hizo sita za maji kuanzia asubuhi hadi jioni haziwatoshi, lakini kutokana na gharama ya maisha inabidi watumie kidogo kidogo.

“Watu wanataka kufua, kupika, kuoga na kufanya mambo mengine, maji ndio kila kitu kuanzia kukuweka wewe msafi hadi mazingira yanayokuzunguka.

“Yaani nikilala nikishtuka usiku nawaza maji, nasema labda asubuhi yatatoka, lakini hukuti kitu; maji yamekuja kutuongezea gharama za maisha,” anasema Habiba.

“Sasa hiyo Sh4,800 hapo si nimepata maharagwe na unga kwa ajili ya chakula cha familia yangu, lakini pesa hizo nazipeleka kwenye maji, ilhali bili ya maji ya mamlaka husika ikija nitapaswa nilipe.”


Mgawo ulivyotangazwa

Oktoba 25, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala alitangaza mgawo wa maji katika jiji hili lenye wakazi takribani milioni sita linalopata maji ya Mto Ruvu na kuhudumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa).

Ukiachana na idadi kubwa ya watu, Dar es Salaam ndiyo inaongoza kwa shughuli nyingi za uzalishaji mali na kwa kiasi kikubwa maji ni malighafi muhimu viwandani.

Mgawo huu ulitangazwa baada ya kujiridhisha kuwa uzalishaji wa maji umepungua kutoka lita za ujazo 466 milioni hadi kufikia lita 300 milioni kwa siku, sawa na asilimia 64 ya uzalishaji, kwa maana hiyo kuna upungufu wa asilimia 36.

Hali hii imesababisha upungufu wa maji, hivyo wakazi wa Dar es Salaam na Pwani wanalazimika kupata maji kwa kugawana kiasi kidogo kinachozalishwa.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa mgawo, baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam bado yanalalamikia kukosa maji.

“Hii ni wiki ya tatu sasa, hakuna mgawo wa maji, ratiba iliyotolwa awali ilibidi tupate maji kila Jumatano, lakini hamna kitu, ukilala unawaza kesho itakuwaje bila maji,” anasema mama wawili, mkazi wa Ilala.

Wanachosema wanawake

Neema William, mkazi wa Kijitonyama anasema uhaba wa maji unawafanya wananchi wapitie kipindi kigumu kutokana na umuhimu wa rasilimali hiyo.

“Mamlaka husika zinapaswa kuongeza jitihada katika kuhakikisha huduma ya maji inakuwa si miongoni mwa vitu vinavyoadimika. Hii si mara ya kwanza kwa hali hii kutokea jijini Dar es Salaam, nakumbuka mwishoni mwa mwaka jana tulikumbana na hali hii na wote tuliona makali yake, ajabu ni kwamba na mwaka huu imejirudia na makali yake yanaumiza kila kona,” anasema Neema.

“Kupatikana au kukosekana kwa maji kuna athari kwa jamii nzima, lakini kwa uzito zaidi makali ya mgawo wa maji tunakumbana nayo wanawake. Nasema hivi kwa kuwa sisi ndio watumiaji wakubwa wa maji na ndio tunatunza familia, hivyo nyumba isipokuwa na maji anayewajibika wa kwanza ni mama,” anasema Neema.

Akizungumza hilo, mkazi wa Kimara, Leila Jamal anasema kwa hali inavyoendelea upo uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko kwa kuwa watu wanalazimika kutumia maji yasiyo salama.

“Tunafahamu fika maji ni uhai, maji yasipokuwepo mambo mengi hayaendi na kutokana na umuhimu wake unaweza kujikuta unatumia yasiyo salama.

“Hali ikiendelea hivi tusishangae mambo ya kipindupindu na magonjwa mengine yanayotokana na kutotumia majisafi na salama yakaibuka. Tumesikia changamoto iliyopo na tunakubaliana na mgawo, lakini sasa hiyo ratiba izingatiwe ili wote tupate maji,” anasema Leila.


Wanaume wanajua changamoto?

Kuhusu changamoto ya maji kuwadondokea wanawake, hilo pia linaelezwa na Richard Mallya, anayekiri kuwa licha ya kufahamu kuna uhaba wa upatikanaji maji, suala hilo ameliacha mikononi kwa mkewe.

“Sasa mimi nitafute hela ya kula halafu nitafute na maji, hilo jambo haliwezekani, nimeliacha mikononi mwa mama, mke wangu ndiye ana jukumu hilo,” anasema Mallya.

“Mimi ninachotaka pale ninapohitaji maji niyapate, siwezi kutoka nyumbani bila kuoga au kuvaa nguo chafu, ni yeye anajua anatoa wapi maji.”

Hemed Mustafa, baba wa watoto wawili anasema changamoto ya upatikanaji wa maji kuwakabili wanawake imetokana na tamaduni za Kiafrika kuwa, anayepaswa jikoni na kuandaa chakula ni mwanamke.

“Kwa hapo mwanamke ndiye anajua maji yamebaki ndoo ngapi, na yapi ni yakupikia, kufulia au kuoga kwa sababu ndipo yanapotumika kwa kiasi kikubwa, sasa mimi kwa sababu siingii jikoni kupika siwezi kujua, badala yake nikitaka kuoga namwambia mke wangu anaandaa maji,” anasema Mustafa.

Hata hivyo, kauli hizo zinatofautiana na kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Faruq, akisema huwa anahakikisha anajaza maji kwa ajili ya familia yake katika mapipa mawili kila yanapokwisha.

“Unajua kazi nyingi za nyumbani zinafanywa na wanawake, kwa hiyo hilo la maji nimejipa jukumu mimi mwanamume, kila yanapokwisha nahakikisha nakwenda kuchota kisimani na kujaza kwenye mapipa nyumbani,” anasema Faruq.


Vipi kuhusu Serikali

Mara kadhaa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amejitokeza na kuzungumzia suala la mgawo wa maji, akitaka mamlaka husika kuheshimu ratiba ili kuwezesha watu wa maeneo yote kupata maji.

Waziri huyu anasema endapo ratiba ya mgawo itazingatiwa, tatizo haliwezi kuwa kubwa kama ilivyo sasa, ila jambo la muhimu ni watu kutambua kuwa kuna changamoto, hivyo wajenge utamaduni wa kuhifadhi maji.

“Tunapitia kipindi kigumu ila niwaombe wakazi wa Dar es Salaam kuwa wavumilivu, jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika chini ya Serikali kuhakikisha tunakuwa na suluhisho la kudumu la tatizo la maji,” anasema Aweso.

“Tuna mradi wa maji wa Kigamboni umeshaanza kufanya kazi, pia kuna visima 197 vimefufuliwa, navyo vimeanza kutoa maji, kati ya hivyo 162 tayari na vimeingiza kwenye mzunguko lita 28 milioni, imani yetu tatizo litapungua,” anasema Aweso.

Akiwa makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alijiwekea lengo la kumtua mama ndoo kichwani. Hili lililenga kupunguza kwa kiasi kikubwa adha ya maji, changamoto inayowasumbua zaidi wanawake.

Katika kutekeleza hili jitihada mbalimbali zimefanyika na wiki iliyopita Rais Samia alieleza kuwa ametekeleza lengo hilo kwa asilimia kubwa, lakini changamoto iliyopo ni athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame.