Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT- Wazalendo kutumia msemo wa 'Ubaya ubwela' uchaguzi wagombea

Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Dorothy Semu akizungumza na wananchi wa Kwa Mkonga wilayani Handeni mkoani Tanga katika mwendelezo wa ziara ya chama hicho.

Muktasari:

  • Chama cha ACT- Wazalendo, kimesema wagombea watakaoteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera katika uchaguzi wa serikali za mitaa watakuwa ni viongozi wanaojali maslahi ya Watanzania.

Dar es Salaam. Kiongozi wa  ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amesema chama hicho kitawateua wagombea makini na wasikivu watakaowania mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, akiwaomba Watanzania kuwaunga mkono muda utakapofika.

Semu ameeleza hayo leo Alhamisi Septemba 12, 2024 akihutubia wananchi wa  Kwa Mkonga wilayani Handeni mkoani Tanga katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika wilayani humo kwa lengo kusikiliza kero na  kufanya maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongaoji utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Viongozi wakuu wa ACT- Wazalendo, wakiongozwa na Semu wameingia siku ya pili ya ziara ya  awamu pili ya siku 21 ya  kutembelea mikoa 22 ikiwemo ya Dar es Salaam, Manyara, Dodoma, Pwani, Geita, Mwanza, Kilimanjaro na Pwani, Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Songwe na Rukwa.

Amewahakikishia wananchi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla kwamba ACT - Wazalendo kitateua wagombea watakaokuwa sauti ya watu na watakaotoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Tupeni ushirikiano, tutawaletea viongozi watakaokuwa tayari kukosolewa, pasipo kujali itikadi za vyama vya siasa sambamba na kusoma mapato na matumizi," amesema Semu.

Mbali na hilo, Semu amesema ACT- Wazalendo, itaendelea kuwa sauti za wananchi katika kuhakikisha wanazisemea shida zao ili zipate ufumbuzi na kuondokana na umasikini na kujiletea maendeleo.

"Niwahakikishe chama chetu kitakuwa mstari wa mbele kuikumbusha Serikali kutekeleza majukumu yao ya kutatua changamoto za Watanzania," amesema.

Mwenyekiti wa Ngome ya Wananake wa ACT- Wazalendo, Janeth Rithe amesema chama hicho, kipo katika ziara ya kutengeneza mfumo wa uongozi katika Taifa kwa kuwaandaa Watanzania kufanya uamuzi sahihi katika Uchaguzi Mkuu mwakani 2025.

"Wananchi wa Handeni msidanganyike, chagueni ACT - Wazalendo au upinzani mpate maendeleo, achaneni na porojo za kwamba usipochagua chama tawala hupati maendeleo.

"Niwape mfano mwaka 2015 ACT ilishinda Jimbo la Kigoma Mjini pamoja na Manispaa ya Ujiji mbona maendeleo yalipatikana, msidanganyike na porojo hizo," amesema Rithe.

Ado Shaibu

Akizungumza na wananchi wa Mtwara, Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amesema imebaki miezi miwili kwenda katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, akisema chama hicho kitakwenda katika uchaguzi huo kwa kaulimbiu ya klabu ya Simba ya 'Ubaya Ubwela.'

" Tunataka atakayeshinda basi atangazwe sio kiongozi mmoja atoe kauli ya aliyeshindwa ndiye atangazwe, hii hapana hatutakubali tunataka haki itendeke ili uamuzi wa wananchi uheshimiwe," amesema Ado.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti viongozi wa CCM  wakiongozwa na katibu wa itikadi, uenezi na mafunzo wa chama hicho, wameweka wazi kwamba chaguzi zijazo ukiwemo wa serikali za mitaa utakuwa huru, haki, na atakayeshinda atatangazwa.

Pia, Ado amewataka wananchi wa mikoa ya kusini kuwa mstari wa mbele kuwafichua watu wanaodaiwa kuwanyonya katika mazao yao ya ufuta, korosho na mbaazi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa.

"Msiwe wanyonge, tupeni ushirikiano wa kuwafichua wanaowanyonya au kuwadhulumu haki zenu, nipo tayari acheni uoga tuambie ili tuwaweke hadharani na hatua zichukuliwe," amesema Ado.