ACT Wazalendo wamkumbusha Rais Samia kutoa ratiba Katiba Mpya

Mwenyekiti wa Taifa wa Ngome ya Wazee Yassin Gumsani

Muktasari:

  • ACT Wazalendo yamkumbusha Rais Samia kuweka wazi ratiba ya kuanza mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimetoa msisitizo kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuweka wazi ratiba ya mchakato wa Katiba mpya na upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam, leo Machi 23, 2023 na Ngome ya Wazee ya chama hicho, huku ikieleza Rais huyo haitoshi kila siku kuendelea kuwapa matumaini Watanzania kwamba mchakato utaanza, bila kueleza lini utaanza.

"Tunaendelea kutoa msisitizo Rais aweke wazi ratiba ya mchakato wa kupatikana Katiba mpya na upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi, kwani haitoshi kuendelea kutupa matumaini ya kwamba mchakato utaanza," amesema Mwenyekiti wa Taifa wa Ngome ya Wazee Yassin Gumsani.

Gumsani amesema wanatamani kujua ratiba nzima hadi ukomo wake utakuwa lini huku wakieleza wanatamani mchakato huo unakamilishwa kabla ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Gumsani amesema Rais Samia amekuwa akirejea kauli hiyo mara Kwa mara huku akitolea mfano hotuba aliyoitoa Machi 19,2 023 kwenye Uwaja wa Uhuru, kukumbushia ahadi yake ya kuanza mchakato huo.

Naye Ally Mtumweni ambaye ni Katibu Mwenezi Taifa Ngome hiyo, amesema katika kuunga mkono masuala ya kitaifa wamekusudia kuunganisha wazee wa vyama mbalimbali nchi nzima ili kutengeneza umoja wa wazee wa vyama vya siasa kuwa na sauti moja ya kudai maslahi ya kitaifa.

"Tutafanya ziara kutembelea wazee wenzetu katika vyama mbalimbali ili kuchukua maoni na mapendekezo yetu ya uundwaji wa umoja wa wazee wa vyama katika nchi yetu," amesema.

Ameeleza nafasi ya uongozi wa umoja huo itakuwa inahuduma kwa mwaka mmoja mmoja ambapo vyama vitakuwa vinashika nafasi hiyo kwa awamu.