Ado Shaibu: ACT tumeamua kuzibeba kero za wananchi

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema chama hicho kimedhamilia kuweka  utaratibu utakaowezesha kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu uwajibikaji wa Serikali katika majimbo mbalimbali nchini.


Tunduru. Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema chama hicho kimedhamilia kuweka utaratibu utakaowezesha kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu uwajibikaji wa Serikali katika majimbo mbalimbali nchini.

Amesema lengo ni kuhakikisha Serikali inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa kuwaletea maendeleo Watanzania, akisema utaratibu huo utawahusisha viongozi wa kitaifa na waliokuwa wagombea ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu 2020.

Ado ambaye leo Jumatano Oktoba 5, 2022 ameingia siku ya sita ya ziara yake, ametoa kauli hiyo,  akizungumza na wanachama na wafuasi ACT Wazalendo katika kata ya Ligunga, Jimbo la Tunduru Kaskazini mkoani Ruvuma.

"Nikianza na Tunduru sitowaacha mimi na viongozi wenzangu tutasimamia ajenda zenu za maendeleo kwa kuhakikisha Serikali inawajibika. Nafahamu baadhi ya waliochaguliwa hawatekelezi majukumu yao kwa ufanisi wa kusimamia kero zenu.

"ACT Wazalendo tumeamua kuzibeba kero zenu sio Tunduru bali majimbo mengine tutahakikisha nchi nzima tunazisemea changamoto zenu ili zipate ufumbuzi.Nikielekea ukingoni mwa ziara ya nimebaini kero mbalimbali ikiwemo maji, barabara na korosho mashamba kuvamia na tembo zinazopaswa kufuatiliwa kwa ukaribu," amesema.

Ado aliyegombea ubunge wa Tunduru Kaskazini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 lakini hakufanikiwa baada ya Hassan Zidadu wa CCM kuibuka kidedea,  amesema licha ya ACT Wazalendo kuwa na wasemaji kisekta bado haitoshi hivyo wamedhamilia kuweka wasemaji ngazi ya chini ili kuwa sauti ya wananchi.

"Ukishuka ngazi ya chini utakutana na madiwani na wabunge waliokosa nafasi, tunataka hawa ndio wawe sauti ya wananchi nje ya Bunge na mabaraza ya madiwani.

"Mimi na Mtutura (Abdallah, aliyekuwa  mgombea jimbo la Tunduru Kusini) tutakuwa wabunge wa nje ya Bunge. Tutapaza sauti dhidi changamoto za stakabadhi ghalani, uingizwaji holela wa ng'ombe na kupigania huduma nzuri za kijamii kwa wanatunduru," amesema Ado.

Amesema hali hiyo itakuwa katika  majimbo mengine ya mikoa mbalimbali ya Mtwara, Lindi, Pwani, Shinyanga  Kigoma, Tabora, Shinyanga bila kusahau Pemba na Unguja. Amesisitiza lengo ni kuwa sauti mbadala yenye uhakika wa kufikisha kero za wananchi ili Serilali itafute ufumbuzi.

Katibu wa Mkoa wa kichama wa Selous, Abdallah Mtutura amesema utaribu huo uliolezwa Ado utalenga kufikisha kwa wakati kero zao za wananchi hasa wa maeneo ya vijijini.

Mtutura amesema yeye ameshaanza kuutekeleza utaratibu huo katika jimbo hilo.

"Kwa kutumia nafasi yangu ya waziri kivuli wa kilimo, nimekuwa nikipokea kero mbalimbali za wananchi wa wilaya ya Tunduru ikiwemo suala mgogoro wa wakulima na wafugaji.

Pia, changamoto ya wanyama pori wanaovamia na kufyeka mashamba ya wakulima," amesema Mtutura.

Aliyekuwa mgombea wa udiwani wa Ligunga katika jimbo la Tunduru Kaskazini, Said Kazembe amesema kazi ya vyama vya upinzani ni kuhakikisha vinakuwa sauti mbadala ya kufikisha changamoto za wananchi kwa Serikali na kupatiwa ufumbuzi.