Prime
Aliyekatwa Chadema kukata rufaa, wenyewe wasema anatapatapa
Dar es Salaam. Sakata la aliyekuwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Said Issa Mohammed, kuvuliwa uanachama wake limechukua sura mpya baada ya kutangaza kuwa atakata rufaa kwa Kamati Kuu ya chama hicho kupinga uamuzi huo.
Mbali na hilo, Said ametishia kuchukua hatua zaidi kwenda chombo cha juu yake iwapo rufaa yake haitazingatiwa kwa haki, ingawa hakutaka kuweka wazi ni chombo gani hicho cha juu atakachokwenda.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, amemjibu maneno anayozungumza ni kutapatapa hali ambayo huwa inawakuta wengi wakikumbana na kadhia, lakini akili ikiwarejea wanajua wametimuliwa na kubaini walichokifanya si kizuri.
“Maneno anayozungumza ni ‘stress’ na kutapatapa hali ambayo huwa inawakuta wengi wakikumbana na kadhia hiyo, lakini baadaye akili ikiwarejea wanajua wametimuliwa kwa sababu walichokifanya si kizuri,” amesema.
Amesema wanaheshimu hatua za kinidhamu ambazo mamlaka za chama wamechukua dhidi ya Saidi Issa, kama kuna rufaa au malalamiko yatakwenda kwenye ngazi husika, hadi kutufikia huku juu itahitaji kupitia kwanza ngazi zote huko chini.
Said Issa aliyevuliwa rasmi uanachama Juni 6, 2026, amesema hakuna kikao halali kilichofanyika kabla ya kufikiwa kwa uamuzi huo, wala hajawahi kupewa wito au barua ya kutakiwa kujieleza kuhusu tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Taarifa ya kufutwa kwa uanachama wake ilitolewa Juni 7, 2026, kufuatia uamuzi wa Kamati tendaji ya Kanda ya Pemba uliopitishwa katika kikao cha dharura kilichofanyika Chake Chake, Pemba, Juni 6, 2026.
Kwa mujibu wa chama, Said alifutwa uanachama baada ya kushindwa kujitetea dhidi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili ndani ya siku 14 alizopewa.
Hatua hiyo ilitokana na ushiriki wake katika kufungua Shauri la Madai Na. 8323 la mwaka 2025 dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Katibu Mkuu wa chama.
Katika shauri hilo, yeye pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu (marehemu kwa sasa), walidai kuwapo kwa mgawanyo usio sawa wa mali na rasilimali za chama kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Hata hivyo, Mei 28, 2026, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitupilia mbali kesi hiyo baada ya kubaini kasoro za kisheria katika hati ya madai, ikiwamo kushindwa kuainisha tarehe ya kuanza kwa ukiukwaji uliodaiwa. Uamuzi huo ulitolewa na Jaji David Ngunyale wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi kutoka Zanzibar, Said amesema hajawahi kupewa barua yoyote ya kujieleza na ameitaka Chadema kuweka wazi kumbukumbu za vikao vinavyodaiwa kufanyika iwapo inaamini ilifuata taratibu zote.
“Mimi Said sijapokea barua yoyote ya kuniita wala ya kutaka nijieleze. Kwa kuwa sheria hazikuzingatiwa, nitakata rufaa kwa Kamati Kuu kupinga uamuzi huo. Kama mwanachama nina haki zangu, na chama kina haki zake,” amesema.
Amesema hafahamu kikao kilichofikia uamuzi wa kumvua uanachama na ameeleza kushangazwa na hatua hiyo kutoka kwa Chadema, chama ambacho kwa muda mrefu kimekuwa mstari wa mbele kupigania haki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pemba, Omar Nassor, amesema kikao cha Mei 23, 2026 pamoja na kile cha Juni 6, 2026, vilikuwa halali na kwamba uamuzi uliotolewa ulizingatia katiba ya chama.
“Tulimpa barua ya kutakiwa kutoa maelezo ndani ya siku 14, lakini hakuwasilisha majibu yoyote katika kipindi hicho. Ndipo tukafikia uamuzi wa kumfuta uanachama,” amesema Omar.
Katika hatua nyingine, Said amesema si kila uamuzi unaotolewa na kikao huwa halali, bali uhalali wake hutegemea taratibu zilizofuatwa na watu walioshiriki katika kufanya uamuzi huo kwa mujibu wa Katiba ya chama.
“Ndiyo maana chama kimeweka mfumo wa rufaa kwa yeyote ambaye haridhiki na uamuzi uliotolewa. Nitakata rufaa kwa Kamati Kuu kwa sababu sikubaliani na uamuzi wa Kanda,” amesema.
Amesema iwapo Kamati Kuu itashindwa kumtendea haki, atachukua hatua nyingine za kisheria au za kiutaratibu, ingawa hakutaka kuzitaja kwa sasa.
“Sitaki kueleza kwa sasa nitakwenda wapi. Nitatoa taarifa nitakapofikia hatua ya kukata rufaa. Kwa sasa nashauriana na wanasheria wangu na kupitia Katiba pamoja na kanuni za chama ili kubaini ni kifungu gani kimekiukwa,” amesema Said.
Said amesema madai yake makuu ni kuhakikisha Zanzibar inanufaika kwa haki katika mgawanyo wa rasilimali za chama.
“Chadema hupokea ruzuku. Kama walikuwa wanapokea Sh559 milioni, ni muhimu kuonyesha Zanzibar inapata asilimia ngapi ya fedha hizo,” amesema.
Amedai kuwa licha ya chama kuwa na zaidi ya magari 43, Zanzibar haina hata gari moja tangu kuanzishwa kwa chama hicho.
“Nasikitika kuona nafutwa uanachama kwa madai ya usaliti wa chama ilhali ninachodai ni haki ya Zanzibar katika mgawanyo wa rasilimali,” amesema.
Amesema anashangazwa na viongozi wa chama Zanzibar kwa kile alichodai kuwa hakuna usaliti wowote alioufanya, bali amekuwa akidai haki kama mwanachama wa kawaida mwenye kadi ya daraja la gold.
Hata hivyo, Omar amesema kitendo cha kukipeleka chama mahakamani tayari kinatosha kuhesabika kuwa usaliti kwa mujibu wa katiba ya Chadema.
Katika hatua nyingine Golugwa amesema hatua za kinidhamu zinahitaji kumpa taarifa muhusika juu ya tuhuma zake, ajibu na kuitwa mbele ya kikao.
“Sasa kuna hali ya kiburi watu huweka hasa pale anapokuwa sikio la kufa, halisikii dawa. Mamlaka za chama wamechukua hatua, Saidi Issa amefukuzwa uanachama. Kwa hatua iliyochukuliwa kwa sasa atakuwa na stress hivyo apewe muda atazoea na ataelewa kuwa ameshafukuzwa uanachama na kuwa hatakiwi tena aende hukohuko kwa waliomtuma,” amesema.
Amesema hali hiyo ngumu ya kutapatapa inawatokea wengi lakini atazoea tu kuwa hatakiwi ndani ya chama hicho kwani ameshafukuzwa na uamuzi huo unafurahiwa na Wazanzibar.
“Mamlaka za chama huko Pemba wamechukua hatua na wao wenyewe ni kama wanasema wametua mzigo wa misumari, maana wanasema huyu bwana alikuwa kama amewatia unajisi Wanzanzibar kwa kukitaabisha chama nchi nzima na kupelekea kuzuiwa shughuli za siasa kwa siku 309,” amesema.