Bendera yatajwa sababu vurugu Chadema, UVCCM
Muktasari:
- Polisi Mkoa wa Tanga yasema uchunguzi unafanyika kubaini mhusika wa vurugu hizo ili hatua zichukuliwe.
Dar es Salaam. Ushindani wa kupeperusha bendera mtini, unatajwa kuchochea ugomvi uliomsababishia kipigo na hatimaye majeraha kiongozi wa Chadema Wilaya ya Tanga, Hussein Ally kutoka kwa vijana wanaodaiwa kuwa wa CCM.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya vijana wa CCM kushusha bendera ya Chadema iliyokuwapo kwa takriban miaka mitatu katika mti uliopo kwenye kituo cha bodaboda cha Mgandini mkoani humo na baadaye kuibuka vurugu za kila upande kutaka bendera yake ipepee.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema uchunguzi unafanyika kubaini mhusika wa vurugu hizo ili hatua zichukuliwe.
Ilivyokuwa
Inaelezwa ugomvi ulizuka baada ya madereva bodaboda wa Kituo cha Soko la Mgandini ambao ni wafuasi wa Chadema kutaka bendera ya chama hicho ipandishwe kwenye mti uliokuwepo eneo hilo kama inavyosimuliwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe.
Kwa mujibu wa Jumbe, bendera ya Chadema ilikuwepo eneo hilo kwa takriban miaka mitatu lakini Septemba 5 vijana wa CCM walifika na kuishusha.
Hatua ya kushushwa kwa bendera hiyo ilitokana na kilichoelezwa na Jumbe kuwa, vijana wa CCM waliipandisha ya kwao wakidai kunafanyika shughuli za chama hicho tawala na hivyo ya Chadema ishushwe wakimaliza itapandishwa.
Ametaja shughuli iliyokuwa ikifanywa na CCM ni uzinduzi wa shina lililojengwa karibu na eneo hilo, ambalo pia lilikuwa na vijana wa bodaboda waliogawanyika kutoka walewale wa Mgandini na wakawa wafuasi wa CCM.
Uzinduzi huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM na Serikali, Jumbe anasema ulifanyika huku bendera iliyokuwa ikipepea ni ya chama hicho na hapakuwa na ugomvi.
Anasema katika uzinduzi huo, kiongozi mmoja wa CCM alitoa Sh2 milioni kwa vijana wa bodaboda waliokuwa kwenye kijiwe hicho cha chama tawala na wengine waliahidi kutoa Jumatatu Septemba 11, hivyo kuwa na jumla ya Sh4 milioni.
Amesema vijana wa bodaboda wa CCM walikuwa takribani 50.
Anaeleza shida iliibuka kwenye mgawo wa fedha Sh2 milioni baada ya wengine kudai kupunjwa hivyo uliibuka mgogoro wa wao kwa wao.
Hatua hiyo anasema ilisababisha baadhi ya vijana hasa waliopunjwa kurudi kwenye kituo cha bodaboda walipo wafuasi wa Chadema wakisema wanarudi kwenye chama chao na wakataka bendera ipandishwe.
“Waliposema lazima ipande yule kiongozi ndiyo akaona amepata washirika na wakaanza kupandisha. Wale vijana wa CCM walipiga simu akaja Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa (Ramadhani Omari) na kundi lake wakampiga sana kiongozi wetu wakampakia mshikaki wakaondoka naye,” anasema.
Baada ya kupokea taarifa hizo, anasema alikwenda vituo mbalimbali vya polisi bila kumpata Ally, hadi saa 10 alasiri alipopigiwa simu kutoka Hospitali ya Mombo akaelezwa kuna ndugu yao anahitaji kupatiwa huduma.
“Nilikwenda nikamkuta ameumizwa hakuwa anajiweza tukalipa akaanza kupatiwa huduma,” anasema.
UVCCM yajibu
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mwenyekiti wa UVCCM Tanga, Ramadhani Omari amesema licha ya uwepo wa tukio hilo, lakini uhalisia wake ni tofauti na linavyoelezwa.
Amesema tukio hilo linakuzwa ilhali halikuwa kubwa na yaliyotendeka si makubwa kama inavyosimuliwa.
Alipoulizwa uhalisia ukoje, amejibu asingeweza kuelezea zaidi kwa sasa, lakini itakapolazimu atatoa tamko.
“Kwa sasa siwezi nikalielezea lakini itakapolazimu tutatoa tamko. Kikubwa uhalisia hauko hivyo,” amejibu.
Kamanda Mchunguzi amethibitisha tukio hilo akisema limetokea katika Kata ya Msambweni, likihusisha kushambuliwa kwa mtu anayedaiwa kuwa ni kiongozi wa Chadema na tayari uchunguzi umeanza ili kubaini wahusika.
“Suala hilo lipo katika hatua za kiuchunguzi, limetokea jana (Septemba 5, 2024), uchunguzi unaendelea kubaini undani wake,” amesema.
Kuhusu mhusika wa shambulio hilo amesema atajulikana pale uchunguzi utakapokamilika na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.