Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Boni Yai afichua kilichomuangusha Mbowe Chadema

Muktasari:

  • Katika uchaguzi huo, Tundu Lissu alishinda kwa kura 513 sawa na asilimia 51.5 dhidi ya kura 482 sawa na asilimia 48.3 alizozipata Mbowe ambaye alikubali matokeo hayo kwa mikono miwili na kuhitimisha safari yake ya uenyekiti wa Chadema iliyodumu kwa takribani miaka 20.



Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, Boniface Jacob,  maarufu Boni Yai amebainisha mbinu walizozitumia kuhakikisha mwenyekiti wa zamani, Freeman Mbowe anashinda uenyekiti wa chama hicho, lakini kwa bahati mbaya ‘upepo’ haukuwa upande wao.

Pia, amekanusha madai ya kumsaliti Mbowe baada ya uchaguzi huo, uliofanyika Januari 21, 2025, akisema baada ya kukamilika kwa uchaguzi  hakutakiwa kununa au kuhama chama, bali kuungana na mshindi kukijenga chama.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Boni Yai, ofisini kwake jijini Dar es Salaam, ambapo amezungumzia mambo mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa ndani uliosababisha mgawanyiko, ikiwa umepita mwaka mmoja na miezi mitano tangu uchaguzi huo ulipofanyika.

Katika uchaguzi huo, Tundu Lissu alishinda kwa kura 513 sawa na asilimia 51.5 dhidi ya kura 482 sawa na asilimia 48.3 alizozipata Mbowe ambaye alikubali matokeo hayo kwa mikono miwili na kuhitimisha safari yake ya uenyekiti wa Chadema iliyodumu kwa takribani miaka 20.

Boni Yai ambaye alikuwa mwenyekiti wa timu ya kampeni ya Mbowe, anasema alilitekeleza vizuri jukumu alilopewa na mwenyekiti huyo wa zamani, hata hivyo upande wa timu iliyokuwa ikimuunga mkono Lissu waliwazidi maarifa.

Anasema upepo wa upande wa kambi ya Mbowe haukuwa mzuri kuelekea katika mchakato huo, licha ya mipango kabambe walioipanga kuhakikisha wanashinda.

“Timu ya wenzetu (Lissu) kushinda kwa tofauti ya kura 32 tunahitaji tupongezwe si kunyooshewa kidole. Ndani ya chama Bavicha (Baraza la Vijana la Chadema) yote, yaani Gen Z, walikuwa upande wa Lissu, kwa hiyo sisi tulipokuwa tukinadi sera zetu hawakutuelewa.”

“Nje ya chama, katika mitandao ya kijamii, tuliwaomba watu watusaidie kuposti bango la mgombea, waliona kama tumewapa kazi ya ajabu, tunataka kuwapaka matope, ikafika hatua hata watu wetu wa karibu waliogopa kujitanabaisha wapo na Mbowe,” anaeleza Boni Yai.

Mbali na hilo, Boni Yai anasema ilifika hatua watu wao wanaowaunga mkono kuwaambia wapo tayari kumpigia kura Mbowe, lakini si kujionyesha hadharani kuwa yupo upande fulani. Hatua hiyo ilionyesha upepo haukuwa mzuri kwa Mbowe.


Mbinu, mikakati iliyotumika

Kwa mujibu wa Boni Yai, baada ya kuona timu ya Lissu imewazidi katika kampeni za “public” (umma), walibadili upepo na kuanza kutafuta kura moja kwa moja kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema.

“Usichokijua, katika uchaguzi ule kungekuwa na tuzo ningepata, kwa sababu katika wajumbe 1,101 hadi tunafika ya siku ya uchaguzi, tulishawafikia wajumbe 700 ambao Mbowe alionana nao,” anaeleza.

Boni Yai ambaye alikuwa wakala wa Mbowe, anasema hatua ya kwanza waliyofanya ilikuwa kukodi ukumbi Mbezi ili Mbowe aonane na wajumbe takribani 300, kisha akaonana na wengine 250 hadi 300 maeneo ya Mabibo External huku wengine akionana nao maeneo ya Mwenge, Magomeni na Manzese.

“Nilimtembeza Mbowe katika maeneo yote hayo usiku ili kuonana na wajumbe 700 waliotoka mikoani, niliwapokea na kuwaonyesha mahali pa kufikia. Kwa vyovyote tulijua asubuhi, ushindi ulikuwa upande wetu,” anasimulia.

Meya huyo wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, anafafanua iliibuka hoja kwamba wakati Mbowe anaonana na wajumbe ilikuwa muhimu kuwapatia fedha, hata hivyo aliona jambo hilo halikuwa sawa kwa namna mwenyekiti huyo wa zamani alivyokuwa akituhumiwa kwamba anatumika na watawala.

“Kama nalaumiwa basi naambiwa sikupa fedha wajumbe, nilimkataza mgombea na hakuna mjumbe aliyepewa pesa. Tulifanya hivi kwa sababu upande wa Lissu walitushinda kwa kigezo kuwa Serikali ina mkono kwa Mbowe, sasa ukienda kutoa fedha ni dhahiri unathibitisha kwamba mnatumika.

“Tuliweka msimamo wa kutotoa rushwa hata Sh10,000 bali tuongee nao ili watupigie kura, uchaguzi ni namba, hayo makundi ya wajumbe kutoka kanda 10 za Chadema, tuliyafikia kwa usiku mmoja, lakini hatukutoa fedha,” anasisitiza.


Kilio kilivyotawala

Baada ya kupata matokeo, Januari 22, 2025, akiwa chumba cha kuhesabu kura, Boni Yai anakumbuka alitoka kwenda moja kwa moja kwenye chumba cha watu mashuhuli katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ambako Mbowe na timu yake walikuwa wameketi.

“Nakumbuka mwenyekiti alikuwa na watu takribani wanane akiwemo Kileo (Henry), Daniel Ngogo, nikawapa matokeo kwamba tumepigwa kwa kura kadhaa, wakulia walilia. Chumba kizima chenye watu saba nane, karibu wote waliangua kilio isipokuwa mimi na Mbowe.”

“Wajibu wangu ulikuwa kumtuliza mgombea (Mbowe) na kusimamia ile ahadi aliyoitoa kwamba akishindwa atamkumbatia Lissu. Nashukuru Mbowe alinielewa, baada ya hapo aliandaa ujumbe mfupi na kuweka katika akaunti yake X akikubali ushindi wa Lissu,” anasema Boni Yai.

Ujumbe huo ulikuwa hivi: “Nimepokea kwa mikono miwili uamuzi wa uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama chetu Chadema uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025. Nampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la uongozi wa chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele chama chetu.”


Mgombea ajiondoa

Baada ya kuona upepo sio mzuri, Boni Yai anasema walimshauri Said Issa Mohamed, aliyekuwa akiwagombea nafasi ya makamu mwenyekiti akiwa kambi ya Mbowe, kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho kwa kuwa upepo haukuwa mzuri kwao.

“Issa alijulikana yuko upande wa Mbowe, na mshindani wake Mohamed Mzee yupo kwa Lissu, sasa wagombea wote wa upande wetu wameshindwa, tukamshauri Issa kwa mazingira yaliyokuwepo, sidhani kama atashinda katika uchaguzi wa marudio wa makamu mwenyekiti, hivyo ajiondoe,” anafafanua.

Anasema Issa aliwasikiliza na kujiondoa kwenye uchaguzi huo. Anasema lengo la kufanya hivyo lilikuwa ni kupata muda kwa Mbowe kutoa hotuba ya kuaga kwa wajumbe pamoja na kumkumbatia Mbowe, jambo ambalo anasema lilifanikiwa.


Madai ya usaliti

Boni Yai ambaye pia ni mfanyabiashara na mjasiriamali, anakana madai ya usaliti kwa Mbowe, akieleza alitimiza majukumu yake ipasavyo na alikuwa bega kwa began na Mbowe hadi mwisho na hadi sasa wana uhusiano mzuri.

“Ukisema msaliti maana yake kabla ya matokeo kutangazwa ningehama upande, lakini nilikuwa bega kwa bega na Mbowe hadi mwisho. Kwa utaratibu wa Chadema, matokeo yakitangazwa na mshindi akapatikana, chama kinarudi kuwa kimoja, hivyo usaliti hauwezi kuwepo,” anasema.

Boni Yai anasema alitimiza vema majukumu yake ya kusimamia na kuratibu uchaguzi akiwa kambi ya Mbowe na hatimaye upande wa Lissu kuibuka kidedea.

“Ukiondoa kuratibu na kumsaidia Mbowe, nilikuwa pia wakala wake wa kuhesabu kura, nilishuhudia namna kura moja badala ya moja zilivyohesabiwa, hivyo sikuyumba maana nilishuhudia kila kitu kwa jicho langu,” anaeleza.

Anasema katika uchaguzi huo, walimnadi vizuri mgombea wao (Mbowe) na wajumbe walipiga kura lakini hazikutosheleza kuibuka kidedea na hivyo mchakato wa uchaguzi uliishia palepale ukumbini.

“Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, uchaguzi ukiisha mkionekana mnajipanga katika chaguzi zingine za mbele, hilo ni kosa. Kitendo chochote cha kuendelea na uchaguzi, baada ya mchakato kwisha, huo ni uasi na hujuma dhidi ya chama,” anasema Boni Yai.


Uchaguzi ulikuwa mgumu

Boni Yai anasema tangu kuanzishwa kwa chama hicho miaka ya 90 uchaguzi wa Chadema wa mwaka 2025, ulikuwa mgumu na ndio mchakato uliokuwa ukifuatiliwa na Watanzania wengi waliotaka kujua nani ataibuka kidedea baina ya miamba hiyo miwili Lissu na Mbowe.

“Mchakato ule ulituongezea wafuasi na wanachama wengi, binafsi licha ya Mbowe kushindwa lakini nilipokea pongezi nyingi za ndani na nje ya nchi kwa kuonyesha demokrasia. Sijutii kuhusu ule mchakato na sijisikii vibaya kushindwa kwa sababu kilichoshinda ni chama,” anasema.


Itaendelea kesho...