CCM Chunya yawaonya wanafunzi wasioripoti shule

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Noel Chiwanga akitoa vyeti vya pongezi kwa mdau wa maendeleo, Mbwiga Maganga katika maadhimisho ya miaka 46 ya chama hicho. Picha na Mary Mwaisenye.

What you need to know:

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Noel Chiwanga amewataka wazazi ambao bado hawajawapeleka watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wawapeleke ili kuepuka kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.


Chunya. Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Noel Chiwanga amewataka wazazi ambao bado hawajawapeleka watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wawapeleke ili kuepuka kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Chiwanga ametoka kauli hiyo leo Februari 4, 2023 katika maadhimisho ya chama hicho, ambayo hufanyika kila Februari 5 ya kila mwaka, ambapo kwa wilaya ya Chunya imefanyika katika Kata ya Sangambi.

Amesema chama hicho kinachoisimamia Serikali iliyopo madarakani kwa sasa kikiwa kinaadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwake kinajivunia maendeleo yanayoonekana kama ujenzi wa zahanati kwenye vijiji, vituo vya afya, miradi ya maji, barabara na madarasa.

"Naomba wazazi wapelekeni watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule walizopangiwa hata kama hawana sare za shule waende hivyo hivyo.

“Serikali yetu imejenga madarasa mazuri kwenye shule zetu hatuna changamoto ya upungufu wa madarasa, amesema Chiwanga,” amesema.

Ameendelea kusisitiza kuwa uwepo wa majengo mazuri ya kujifunzia bila wanafunzi haina maana yeyote ni lazima viongozi wa kata na vijiji mfanye msako kuhakikisha watoto wanakwenda shule bila kukwamishwa na kitu chochote.

Aidha amewaomba viongozi wa Serikali kujenga ushirikiano na chama hicho, kwani kwa sasa ilani inayotekelezwa ni ya chama hicho. 

Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya hiyo, Charles Jokery amewaagiza viongozi wa matawi, vijiji na kata kuhakikisha wanaboresha na na kujenga ofisi ambako hakuna ofisi ili kukipa hadhi chama.

Katibu wa azazi Wilaya Maendeleo Nyamka amesema, wao kama wasimamizi wa elimu na malezi watahakikisha wanasimamia ipasavyo kuhakikisha watoto ambao bado hawajaripoti shule wanaripoti.

Naye Mwenyekiti wa Halmshauri Wilaya ya Chunya, Bosco Mwanginde amewakumbusha wanachama wa CCM kuhakikisha wanalinda heshima ya chama kwa kuhakikisha wanayaeleza yale yaliyofanywa na Serikali.

"Kpindi hiki tutashuhudia kila aina ya maneno ambayo yatakuwa yakisemwa na vyama vya upinzani, ni lazima tutambue kuwa wao hawawezi kutusifia hivyo kwenye maeneo yetu tuitishe mikutano na kueleza yale tuliyafanya kipindi hiki”, amesema Mwanginde.

Awali, Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Chunya, Tamimu Kambona amesema katika katika Kata ya Sangambi wamejenga kituo cha afya kupitia mapato ya ndani, wamejenga shule ya sekondari Sangambi na kuna mradi wa maji uliogharimu zaidi ya Sh500 milioni.

“Maeneo mengine ya Luaraje ambako tumejenga sekondari, kituo cha afya, Kambikatoto tumejenga shule za msingi na sekondari, hivyo hatuna changamoto ya madarasa na sasa tunaelekeza nguvu kwenye kujenga mabweni ili kupunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu.