CCM yapitisha mabadiliko idadi ya wajumbe NEC

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan akisalimia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho alipokuwa akiwasili katika ukumbi kwa ajili ya kuongoza mkutano huo jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbali na idadi ya wajumbe wa NEC, CCM imefanya mabadiliko madogo ya Katiba yao, ambapo sasa nafasi uenezi wa mkoa itakuwa ya kuajiriwa badala ya kuteuliwa ili kuleta ufanisi katika chama hicho.

Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepitisha marekebisho yaliyofanyika katika Katiba ya chama hicho ikiwemo idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), ambapo sasa zitakuwa Tanzania Bara 20 na Zanzibar 20 badala ya 15 kila upande.


Pia, nafasi za uteuzi kwa wajumbe wa NEC zinaongezeka kutoka sita hadi 10, huku nafasi ya ukatibu wa siasa na uenezi wa mikoa kuwa ya ajira badala ya kuteuliwa.


Wajumbe hao wamepitisha marekebisho hayo leo Jumatano Disemba 7, 2022 katika mkutano mkuu wa 10 wa CCM unaondelea Jijini Dodoma. Walikubaliana na mchakato huo baada ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan kuwahoji.

Kabla ya hatua hiyo, mwenyekiti huyo ameeleza sababu mbalimbali za mabadiliko hayo ya katiba hasa nafasi ya uenezi ndani ya CCM kuwa ya kuajiriwa akisema aina ya waliokuwa wakichaguliwa walikuwa wakishughulika na kuimba katika mikutano badala ya kueneza siasa ya CCM.

“Inawezekana kuna sababu nyingi labda uwezo au nyingine, tumeona ili chama kisimewe vizuri kuanzia ngazi ya mkoa nafasi ya uenezi iwe ya ajira.

“Hatua hii itafanya awajibike vizuri kukisemea chama, kwa sababu ni nafasi ya ajira itakuwa ina vipimo kwamba unafanya vizuri utaendelea au unafanya vibaya mkataba utasitishwa ili awekwe mwingine atakayekuwa na sifa ya kukisemea chama.”


Amesema kwa sasa CCM inafanya mambo mengi pamoja na Serikali hakuna anayeyasemea badala yake wenezi wamejipa kazi ya kuimba kwenye mikutano.

Pia amesema CCM imeamua katika ngazi ya mikoa makatibu wenezi wapatikana kwa mfumo wa ajira, akisema kwa namna chama hicho kitakavyokuwa kinapata uwezo basi mchakato huo utashuka hadi ngazi ya chini.

Rais Samia amesema wenezi walioko katika mikoa hivi sasa wameongezewa muda hadi miezi mitatu kutumikia nafasi hiyo wakati mchakato wa kuwapata wengine ukiendelea watakaoshika nafasi hizo.

Pia amesema wameongeza kazi na majukumu ya wa- NEC katika mikoa yao.

“Kilikuwa kilio kikubwa, kwamba hawaingii, hawatumiki na wanajiona hawashirikishwi, sasa tumeamua wapangaiwe majukumu maalumu,” amesema Rais Samia.