CCM yaweka kiporo uteuzi sekretarieti

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Shaka Hamdu Shaka

Muktasari:

CCM imesogeza mbele mchakato wa kuunda sekretarieti mpya baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho uliofanyika Jijini Dodoma leo.

Dar es Salaam.Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesogeza mbele mchakato wa uteuzi na uchaguzi wa wajumbe wa kamati kuu na sekretarieti ya chama hicho, hadi kitakapotangaza tena.

Awali ilitarajiwa kuwa baada ya kufungwa kwa mkutano mkuu na kikao cha kwanza cha wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), kungekuwa na taarifa ya kuundwa kwa sekretarieti mpya.

Hata hivyo, akitoa taarifa ya kwa wanahabari leo Desemba 8, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka amesema mchakato huo umeahirishwa hadi utakapotangazwa wakati mwingine.

“Uteuzi na uchaguzi wa wajumbe wa sekretarieti na kamati kuu umesogezwa mbele, hadi baadaye kitakapoitwa kikao kingine kitakachokamilisha hizo nafasi. Hizi nafasi bado tumetoa muda kidogo, tutakutana kwa ajili ya kukamilisha ungwe iliyobakia,” amesema Shaka.

Mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho uliofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, umemchagua kwa mara nyingine Rais Samia Suluhu kuwa mwenyekiti wa chama hicho tawala.