CCM Zanzibar bado inaamini katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Bakari Machumu (kushoto) akimwelezea jambo Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis wakati alipotembelea ofisi za MCL Tabata jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliundwa baada ya kufanyika kwa maridhiano baina ya vyama vikuu vya siasa visiwani humo kwa lengo la kumaliza mzozo wa kisiasa ambao umekuwa ukisababisha machafuko hasa wakati wa uchaguzi.

Dar es Salaam. Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis amesema CCM inaamini kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ndiyo suluhisho la siasa za Zanzibar na kwamba wapinzani wajielekeze kuwaambia walipokosea

Khamis amebainisha hayo leo Machi 13, 2023 jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) ambayo ni mchapishaji wa Magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina yao.

Amesema licha ya kukosolewa na vyama vya upinzani kikiwemo chama cha ACT Wazalendo ambacho ni mshirika kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, bado wanaamini kwamba serikali hiyo ni suluhu la siasa visiwani humo.

SUK iliundwa baada ya kufanyika kwa maridhiano baina ya vyama vikuu vya siasa visiwani humo kwa lengo la kumaliza mzozo wa kisiasa ambao umekuwa ukisababisha machafuko visiwani Zanzibar hasa wakati wa uchaguzi.

“Sisi tunaamini kwenye maridhiano, nchi hii siyo ya wanaCCM peke yao, nchi hii ni ya Watanzania sisi sote, tuna haki. Rais Samia Suluhu Hassan alipofungua mikutano ya hadhara, wenzetu wawe kama kioo, watuambie hapa umekosea, lakini wao hawatwambii.

“Sisi tunaamini Serikali ya Umoja wa Kitaifa ndiyo suluhisho ya siasa za Zanzibar,” amesema Khamis na kusisitiza kwamba msimamo wa chama chake kuhusu muundo wa muungano ni Serikali mbili.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu alimkaribisha Khamis pamoja na maofisa wengine alioambatana nao katika ofisi za MCL na kumweleza shughuli ambazo kampuni hiyo inazifanya katika kufuikisha taarifa kwa umma pamoja na kuibua mijadala.

Machumu amesema MCL inachapisha magazeti ya Mwananchi, MwanaSpoti na The Citizen na kwamba inaendesha mitandao ya kijamii, tovuti na chaneli ya YouTube ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maudhui kwa njia za kidigitali.

“Tumeanza kutumia mitandao ya kijamii kuendesha mijadala inayoibuka katika jamii. Mijadala hii inayoendeshwa kupitia Mwananchi Twitter Space inawaleta pamoja wadau tofauti ambao wanakutaka na kutoa maoni yao,” amesema Machumu.

Mkurugenzi huyo ameeleza pia kwamba MCL inatoa mafunzo tofauti ya ndani na nje kwa wafanyakazi wake kwa lengo la kuwajengea uwezo na kwamba hivi karibuni wameanza kutoa mafunzo ya uandishi wa data kwa maofisa habari wa Serikali.