Chadema wanguruma Tunduma, vurugu zazuka

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema ili Watanzania wafanikiwe azma ya kupata uongozi unaotakiwa ni lazima waungane na chama hicho kwa kujiandikisha kupata viongozi kuanzia serikali za mitaa, kata, wilayani hadi mikoani.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka wanachama wa chama hicho kuungana kuiondoa CCM madarakani kwa kujiandikisha uanachama ili katika chaguzi zinazokuja wawachague viongozi wakuwatumikia.

Akizungumza leo Oktoba 21 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Tunduma mkoani Songwe, akifungua mikutano Kanda ya Nyasa, Mbowe alikosoa mfumo wa uchaguzi akisema nchi inashindwa kupiga hatua kwa sababu inaongozwa na viongozi ambao hawajachaguliwa na wananchi.

“Tuna tatizo la nchi ambalo ni Katiba inayotoa mamlaka makubwa kwa viongozi waliopo madarakani akiwamo Rais. Taifa linaoongozwa na watu wasiochaguliwa na wananchi matokeo yake linashindwa kupiga hatua,” amesema.

Amesema ili Watanzania wafanikiwe azma ya kupata uongozi unaotakiwa ni lazima waungane na chama hicho kwa kujiandikisha kupata viongozi kuanzia serikali za mitaa, kata, wilayani hadi mikoani.

“Kufanya hivyo tutakuwa tumejenga msingi mzuri katika maeneo yote kwa kuwasimika viongozi na katika kuwahamasisha Watanzania tutazunguka bila kulala hadi kumaliza chaguzi zote.

“Tunataka tuijenge nchi yote cha msingi kila mmoja ajisajili tukimaliza Nyasa tunakwenda Ruvuma, Lindi na Mtwara; tukimaliza tunaenda Kilimanjaro, Manyara, Arusha na Tanga kisha tutakwenda Morogoro, Dodoma na Singida tunamalizia Pwani, Dar es Salaam, Pemba na Unguja,” amesema.

Amesema wanataka wananchi wabadilike kwa kuchukua hatua za kulikomboa Taifa kiuchumi akidai kila uchwao maisha yameendelea kuwa magumu kwa kuwa viongozi waliopo hawana uchungu.

“Watanzania wana maisha magumu siyo kwamba Mungu anapenda ni sababu mmeamua kukaa kimya na kuruhusu watu msiowachagua kuendelea kuwaongoza, tunageuzwa kama chapati,” alisema.

Alisema maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu kutokana na mfumuko wa bei unaochangiwa na Serikali kushindwa kudhibiti bei, mathalani kwenye bidhaa ya nishati, huku akieza kodi, tozo zinaongezeka.

“Kila mwananchi akitoka hapa anapaswa kutafakari Chadema tunayakubali mabomu ya machozi, tunazikubali Mahakama, jela, tunakubali mateso yote haya kuwaamsha tuibadilishe nchi hii,” alisema

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salim Mwalimu alisema chama hicho kinataka wanachama waliojisajili na kupatiwa kadi ya kisasa kabla ya kuwapata viongozi watakao kuwa na uwezo wa kufuata dira waliyojiwekea.

“Operesheni hii inaenda sambamba na uongozi wa ndani, vijana, kina mama, wazee jitokezeni kuomba nafasi za uongozi ngazi mbalimbali kupata watu wa kuvusha salama chaguzi zilizo mbeleni,” amesema.

Alisema wana siku 30 ndani ya kanda hiyo kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi na kuhakikisha wanajindikisha sawa na walivyofanya shughuli hiyo kwenye kanda zingine ikiwamo ya Magharibi.

Naye, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa amesema viongozi ni tatizo kubwa lililopo nchini na ziara zinazofanywa na chama hicho mikoa mbalimbali zinalenga kuwaeleza wananchi cha kufanya.

“Kanda ya Nyasa ni kapu linalowalisha Watanzania hadi tunazungumza wakulima wameuza mahindi yao lakini hadi sasa fedha zao hawajapata hata wakulima za zao la kahawa wanadai ni mambo yanayohitaji viongozi wa kuwasaidia,” amesema.

Vurugu zazuka

Awali, mkutano huo ulioanza kwa maandamano ya wanachama waliokuwa na pikipiki na magari ulifika katika viwanja vya shule ya sekondari Mwalimu Nyerere.

Hata hivyo, baada ya msafara wa Mbowe kufika uwanjani, kulizuka tafrani baada ya walinzi wa chama hicho kudai kuwapo mbinu za watu wasiojulikana kumwaga pilipili kwenye eneo la jukwaa kuu.

"Mambo gani haya yanatokea wakati Polisi mpo hebu fanyeni kazi yenu la sivyo muondoke tutajilinda wenyewe," amesikika akisema Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu.

Kutokana na kauli hiyo, polisi walisogea haraka na kudhibiti ghasia kwa kupiga mabomu mawili ya machozi kisha kuwakamata vijana kadhaa waliokuwa wakishambuliwa na wanachama wa Chadema na kuondoka nao.

Akizungumzia vurugu hizo, wakati wa hotuba yake Mbowe amesema hayo ni mapambano na mahasimu wao, akiwataka wananchi kuwaondoa madarakani kwa sanduku la kura.

"Tumefanyiwa vitimbi vingi ili mkutano wetu usifanyike, lakini nawaambia wana Chadema tutakuwa na mikutano 117 katika Kanda hii,” amesema.