Chadema yaja na mkakati mpya kudai Katiba

Ikungi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuanzia mwezi ujao kitaanza kutoa elimu ya uraia nchi nzima.

Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Ikungi mkoani Singida.

Mbali na elimu hiyo, Mbowe alizungumzia mapungufu yaliyomo kwenye Katiba aliyosema inampa mamlaka makubwa Rais jambo ambalo Chadema kinataka yapunguzwe na viongozi wote wa kisiasa wachaguliwe na wananchi badala ya kuteuliwa na Rais.

Akizungumzia mikutano hiyo ya kutoa elimu ya uraia kwa Watanzania kwa ngazi zote za kijiji, mtaa, kata hadi kitongoji, alisema wataanza na kanda tatu watakakojielekeza kuimarisha chama chao.

Mbowe alizitaja kanda hizo kuwa ni Victoria yenye majimbo 25 ya uchaguzi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera, kanda ya magharibi yenye majimbo 24 katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi na kanda ya Serengeti yenye majimbo 25 ikijumuisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara.

“Tumeanzisha mikakati ya kukijenga chama kwa kwenda kuwaeleza wananchi umuhimu wa Chadema, kuwahamasisha wakate kadi za uanachama za kielekroniki na kutoa elimu ya uraia. Hakuna kulala, nimewaeleza viongozi wangu hakuna ruhusa ya mtu kubaki ofisini makao makuu. Natangaza hapa Ikungi tutakwenda kukiimarisha chama, kukipanga na kukisimamia,” alisema Mbowe.

Kwa miaka saba iliyopita, alisema hawakuruhusiwa kufanya mikutano. “Fimbo tumepigwa za kutosha kama ni magareza...tumeenda chuo cha mafunzo,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti huyo alisema mkakati wa kukijenga chama unalenga kujiimarisha na kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimedumu madarakani tangu Tanzania ipate uhuru miaka 62 iliyopita kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

“Ninawaomba Watanzania wote vijijini, kwenye vitongoji, mitaa muandae watu watakaowafaa kuwa viongozi wa vyama ili tutakapopita mjiunge kwenye chama na muwachague viongozi wenu,” alisema.

Kwenye mkutano huo, Mbowe pia aliwaeleza wananchi waifanye siasa ni maisha yao kwa kuwa kujitenga nayo kunawafanya watawaliwe na viongozi wabovu.

“Ukijiweka mbali na siasa ukatapa viongozi wabovu...kupanda kwa bei ya vyakula kutakuhusu, kuongezeka kwa tozo kunakuhusu na vikokotoo kinakuhusu,” alisema.


Katiba Mpya

Akizungumzia umuhimu wa Katiba Mpya, Mbowe alisema hoja kubwa ni kubadili mfumo wa utawala kwani kwa Katiba iliyopo Rais ana mamlaka makubwa sawa na mfalme.

“Wanawaletea viongozi kama wakuu wa mikoa wanaofanya kazi kwa masilahi ya aliyewateua. Kwanza hamumjui na hafamu mazingira ya kwenu, mnateuliwa wakuu wa wilaya msiowajua na wengine wanateua jamaa zao. Sera ya Chadema kwenye Katiba Mpya viongozi wote wakiwamo wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya watachaguliwa na wananchi. Kama Rais wa Chadema atatumia madaraka yake vibaya atashughulikiwa kama wezi wengine,” alisema Mbowe.

Katiba wanayoitaka Chadema, alisema ni ile ambayo kiongozi akifanya makosa akiwa madarakani atakapoondoka ataweza kushtakiwa ili abebe msalaba wake.

Sera za Chadema alisema mikoa yenye rasilimali kama dhahabu itanufaisha kwanza na itachukuliwa kidogo kupelekwa Serikali Kuu kusaidia maeneo mengine yasiyo na rasilimali kama hiyo.

Aliwataka Watanzania kusimamia haki wakiwamo askari polisi kwamba kama Chadema itaingia madarakani polisi watakuwa upande wa Chadema.

“Leo tuna polisi hapa hawana mabomu, hawana silaha za kutisha, hawana makofia yanayotisha. Simamieni haki, polisi ni wetu sote, tukiingia madarakani tutatetea haki zenu na kuboresha masilahi yenu,” alisema Mbowe.

Mbowe pia alisema ardhi imekuwa ikagawanywa hovyo kwa wageni na Serikali za vijiji kinyume na sheria inayowaruhusu kutoa chini ya ekari 50 lakini baadhi vinazidisha.


Lissu asimulia alivyokamatwa

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu aliyeishi uhamishoni nchini Ubelgiji kwa zaidi ya miaka mitano alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kulikuwa na njama za kumkamata.

Akitangaza kurudi rasmi nyumbani na kusindikizwa na uongozi wa juu wa Chadema, Lissu alisema alilazimika kujificha.

“Wakati natafakari naenda wapi, nikaangalia namba zangu za simu, ya kwanza ilikuwa ya balozi wa Ujerumani nchini.Nikamwomba niende kwake akasema sawa. Nilipofika getini nasubiri kuingia, yakaja magari matatu yakaziba njia wakanifuata na kuniambia ‘mheshimiwa Lissu tunakuomba twende kituoni kwa maohojiano.”

“Wakati nabishana nao wakanimbia tutakwenda na wewe hata kwa nguvu. Kwenye zile purukshani ghafla akatoka balozi mdogo akawauliza mnampeleka wapi nao wakasema wanaenda kuzungumza na mimi. Akawauliza kama nao wanaweza kwenda, wakamkubalia. Tumefika polisi balozi akawauliza mtakaa naye kwa muda gani wakajibu kama dakika 20, akasema ananisubiri.”

“Kule ndani wakaniambia kwa nini nimepeleka wazungu, baadaye waliniachia na yule balozi akasema nimeona hapa hakuna usalama utaenda kukaa kwangu. Nikakaa kule kwa kama siku nane, wakanitafutia pasi ya kusafiria na alinisindikiza hadi ndani ya ndege,” alisema Lissu.

Lissu aliwaeleza wananchi wa Ikungi kwamba kama si balozi yule hajui hali yake ingekuwaje kwani alikuwa anasakwa kwa udi na uvumba.

Aliwaleza wananchi hao kwamba yote hayo yaliwekezana kutokana na Katiba mbovu inayompa madaraka makubwa Rais na aliwataka wananchi kuungana nao katika kudai mabadiliko kwa lengo la kuodokana na kadhia hizo.

Lissu alizungumzia malalamiko ya vikokotoo kwamba wastaafu wanapunjwa mafao yao ambayo walikuwa wapate asilimia 50 lakini sasa wanapata chini ya hapo.

Lissu alisema wananchi wa Wilaya ya Ikungi wanaporwa ardhi yao inayotolewa kwa wawekezaji kwa kutumia Katiba iliyopo.

Makamu huyo mwenyekiti pia alizingumzia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwamba wazee wa Ikungi waliotakiwa kupewa msaada huo wanafanyishwa kwanza kazi ya kulima barabara na kuchimba mabawa jambo lisilokubalika.