Dundula tishio kwa wageni Afrika Kusini

Rais wa Kundi la Operesheni Dudula, Zandile Dabula. Picha na BBC

Muktasari:

  • Je, nini kitatokea nchini Afrika Kusini baada ya kundi lilinaloeneza chuki dhidi ya raia wa kigeni kusajiliwa kuwa chama cha siasa na kupanga kushiriki uchaguzi mkuu ujao.
  • Ni kundi la Operesheni Dudula lililoanzishwa Soweto miaka miwili iliyopita.

Je, nini kitatokea nchini Afrika Kusini baada ya kundi lilinaloeneza chuki dhidi ya raia wa kigeni kusajiliwa kuwa chama cha siasa na kupanga kushiriki uchaguzi mkuu ujao.

Ni kundi la Operesheni Dudula lililoanzishwa Soweto miaka miwili iliyopita.

Dudula ni neno la Kizulu lenye maana ya "kulazimisha kutoka", kinachofanyika ni kuwalazimisha raia wa kigeni kuondoka nchini mwao.

Umaarufu wa Operesheni Dudula umefifisha umaarufu wa Chama cha African National Congress (ANC) ambacho kinaelezwa umaarufu wake uko chini ya asilimia 50.

Matamanio ya kundi la Operesheni Dudula yamelenga kujaza pengo hilo baada ya kujigeuza kutoka kundi la kupinga wahamiaji na kuwa chama cha kisiasa cha kitaifa, kikieleza malengo yake ya kuwania uchaguzi mkuu wa mwakani.

“Lazima tuwe wakweli hapa kwamba matatizo mengi tuliyonayo yanasababishwa na utitiri wa raia wa kigeni.
Nchi yetu ni balaa." Ni kauli ya mwanadada Zandile Dabula, ambaye ni Rais wa kundi linalojiita Operesheni Dudula.

Kundi la Operesheni Dudula ni miongoni mwa makundi mawili yaliyoanzishwa kuanzisha chuki dhidi ya raia wa kigeni, kundi lingine liliitwa vuguvugu la Alexandra Dudula.

Baada ya Nelson Mandela kuingia madarakani kwenye uchaguzi wa mwaka 1994 na kuwa Rais wa kwanza mweusi kushika uongozi wa nchi hiyo, wananchi wake walianza kufurahia matunda ya jamii ya kidemokrasia inayoheshimu haki za binadamu kwa raia wake.

Pamoja na matunda hayo, raia wa kigeni wameanza kuona uchungu wa kuishi kwenye nchi hiyo kwa kuanza kushambuliwa kwa maneno na vipigo wakilaumiwa kuwa chanzo cha matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo.

Wageni wanalaumiwa kwa madai ya ongezeko la vitendo vya uhalifu, ukosefu wa ajira kwa wazawa na kuenea kwa magonjwa.
Licha ya kutokuwepo kwa ushahidi wa haya, bado raia wa kigeni wameendelea kusumbuliwa na polisi, mashambulizi na kuporwa mali zao.

Rais wa kundi la Operesheni Dudula, Zandile Dabula aliyechaguliwa kuongoza kundi hilo Juni 2023, anasema; “Wageni ndio chanzo cha matatizo ya kiuchumi ya Afrika Kusini.”

Dabula licha ya kuelezwa ni mpole na mwenye haiba anasisitiza: "Nchi yetu ni ya fujo. Raia wa kigeni wanafanyia kazi mpango wa miaka 20 wa kuichukua Afrika Kusini."

Hata hivyo, kiongozi huyo alipoulizwa ushahidi wa mpango huo wa miaka 20, alikiri ni uvumi, lakini akasisitiza anauamini.

Rais wa Kundi la Operesheni Dudula, Zandile Dabula (Katikati) akiwasalimu wafuasi wake wakati akiingia kwenye ukumbi wa mkutano kuendesha moja ya vikao vya kundi hilo. Picha na BBC

"Unaona dawa za kulevya kila mahali na wengi wa waathirika wa dawa za kulevya ni wa Afrika Kusini kuliko raia wa kigeni.
Kwa hiyo, nini kinatokea? Je, wanawalisha ndugu zetu wenyewe ili iwe rahisi kwao kuchukua?" Alidai Dabula.

Si Dabula pekee, mfuasi wa kundi hilo Mandla Lenkosi naye anasema: “Tulikulia katika nyakati za ubaguzi wa rangi, ambapo mambo yalikuwa bora zaidi kuliko ilivyo sasa."

Mwanamke mwenye umri wa miaka 57 raia wa Afrika Kusini ambaye ni mpishi shuleni katika jiji la Johannesburg, Dimakatso Makoena baye anasema;

"Kusema ukweli, ninachukia wageni. Ninatamani wangepakia na kuondoka katika nchi yetu.” Anasema Makoena, huku akiongeza kuwa sababu za kuchukia wageni ni kwa tabia zao za kuuza dawa za kulevya kwa wenyeji na mtoto wake alianza kutumia dawa za kulevya akiwa na umri wa miaka 14.

Wingi wa wageni

Maneno ya chuki dhidi ya wageni yanayotumiwa na baadhi ya viongozi wa umma, wanasiasa na makundi yanayopinga wahamiaji yamechangia kuchochea imani potofu kwamba nchi imejaa wahamiaji.

Hata hivyo, utafiti wa Mtazamo wa Kijamii wa Afrika Kusini wa mwaka 2021 uligundua kuwa karibu nusu ya watu milioni 60 waliamini kuna wahamiaji kati ya 17 milioni na 40 milioni nchini humo.

Hofu ya kundi la Operesheni Dudula ni kwamba wingi wa dawa za kulevya unasababishwa na raia wa kigeni wasio na vibali, hata hivyo, hakuna takwimu sahihi kuthibitisha madai hayo.

Ripoti ya Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS) ikimnukuu Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini inabainisha kuwa idadi ya kesi za dawa za kulevya zinazohusu wahamiaji ni asilimia 8.5 ya kesi zote zilizopatikana mwaka 2019 na asilimia 7.1 nyingine za mwaka 2020.

Pia, ripoti hiyo ya ISS imebainisha kuwa asilimi 2.3 ya wafungwa ambao ni raia wa kigeni wanaofungwa kila mwaka hawana hati za kuwa nchini humo.

Idadi ya wahamiaji
Ripoti ya mwaka 2022 ya ISS imebainisha kuna wahamiaji wapatao milioni 3.95 nchini Afrika Kusini, ambao ni asilimia 6.5 ya watu wote, idadi inayolingana na kanuni za kimataifa.

Idadi hii inajumuisha wahamiaji wote, bila kujali hali ya kisheria au wapi wanatoka.

Kauli ya Rais Ramaphosa

Rais Cyril Ramaphosa amezungumza dhidi ya maandamano ya kuwapinga wahamiaji, na kulaani makundi kama hayo kwa kuwanyanyasa na kuwashambulia wahamiaji.

Kwa mujibu wa Rais Ramaphosa, tabia hiyo ya kupiga wageni haina tofauti na mikakati iliyopitishwa na utawala wa kibaguzi kukandamiza jamii za watu weusi.

Rais Ramaphosa mwaka 2019 alizindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa kupambana na ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni, lakini wanaharakati wanataka serikali kufanya zaidi.

Annie Michaels, mwanaharakati kutoka Jopo la Ushauri la Wahamiaji la Johannesburg, anasema Waafrika Kusini wanalaumu watu wasio sahihi kwa matatizo yao na wanapaswa kuwastahi wahamiaji kutokana na ujuzi wao wa kuishi.

Hata hivyo, sheria za kusajili chama kulingana na sheria ya Afrika Kusini, kusajili chama haimaanishi kuwa kitafuzu moja kwa moja kusimamisha wagombea kwenye uchaguzi. Operesheni Dudula haina ilani au sera yoyote isipokuwa msimamo wake kuhusu wageni, ingawa Dabula anashikilia kuwa kipo katika kila mkoa isipokuwa Cape Kaskazini.

Kinachotokea Afrika Kusini

Utafiti uliofanyika kuhusiana na wageni, ulibaini kuwa uchumi wa Afrika Kusini uko hasa kwenye mashamba, migodi, usalama na sekta ya ujenzi.

Kwa mujibu wa utafiti huo, maeneo yote hayo yanatoa ujira mdogo kwa wafanyakazi na wengi wanaokubali malipo hayo ni raia wa kigeni wasio na nyaraka, wengi wakitoka nchi za Msumbiji, Lesotho, Zimbabwe na Swaziland.

Utafiti huo umebainisha kuwa ujira kwa wahamiaji hao ni wastani wa randi tano au dola moja ya Marekani kwa siku.