Hakimu auawa kwa kipigo Mbeya

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Dk Vicent Anney amesema watu wawili wameuawa  akiwemo hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Handeni, Joachim Mwakyoma baada ya kupigwa na  wananchi wenye hasira.


Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Dk Vicent Anney amesema watu wawili wameuawa akiwemo hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Handeni, Joachim Mwakyoma baada ya kupigwa na  wananchi wenye hasira.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Januari 22, 2023,  Dk Anney amesema tukio hilo limetolea katika kijiji cha kibole halmashauri ya Busokelo.

Amesema hakimu huyo alikuwa ameambatana na wenzake wawili kwenda kwenye shamba lenye mgogoro na wanakijiji walishinda kesi katika  Mahakamani Kuu  Desemba mwaka 2022  baada ya kesi hiyo kusikilizwa mahakamani kwa miaka zaidi ya 10.

Dk Anney amesema taarifa za awali zinaeleza kuwa kitendo cha hakimu na wenzake kuingia katika shamba hilo kiliwashtua wananchi waliowafuata na kuwahoji na yakaibuka malumbano.

Amesema  katika tukio hilo wananchi wawili walipigwa risasi  na mmoja wa watu waliokuwa wameambata na hakimu na  walikimbizwa  katika hosptali ya Itete kwa matibabu zaidi na hali zao zinaendelea vizuri  .

Dk Anney marehemu  licha ya kuja kijiji hapo  kwa ajili ya mapumziko,  pia alikuwa kwenye taratibu za kukata rufaa mahakamani kupinga hukumu.

“Kwa sasa tumeliachia Jeshi la Polisi kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo  kuwasaka watu waliohusika na  mauaji. Wilaya hii imekithiri  matukio ya mauaji yanayohusiana na migogoro ya ardhi, ”amesema.

Akigusia tabia isiyofaa ya wananchi kujichukulia sheria mkononi Dk Anney amesema, "tunaendelea kushughulikia matukio hayo ikiwepo kushirikisha na  viongozi wa dini, kamati za amani wilaya kuona wanakemea  na kutoa elimu kwa jamii kuachana na tabia ya kuchukia sheria mkononi."

Diwani wa Busokelo ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri, Anyosisye Njobelo amesema, "ndio tukio hilo limetokea kwenye kijiji kilicho katika kata yangu ila kwa sasa mimi sio mzungumzaji tuviachie  vyombo vya dola vifanye kazi yake."

Mmoja wa wananchi wa kata ya Kiwila Wilaya ya Rungwe ambaye aliomba jina lake lisitajwe amesema  changamoto  kubwa ni mienendo ya kesi za migogoro ya ardhi zinavyoendeshwa kwenye vyombo vya maamuzi .

“Tukisema kwa Tanzania,  Rungwe kuna migogoro mingi sana ya ardhi, mauaji  lakini tushukuru Mungu ujio wa Mkuu huyu wa Wilaya, Dk Vincent Anney ameweza kudhibiti kwa wananchi wanaohusika kukamatwa na kuchukuliwa hatua kidogo imesaidia,” amesema.