Kambaya akanwa na wenzake

Abdul Kambaya
Muktasari:
- Ni wanachama 10 tu kati ya 604 waliojiunga na Chadema kutokea CUF, ndiyo walioungana na Abdul Kambaya huku wengine wakisisitiza hawang'oki.
Dar es Salaam. Siku mbili baada ya Abdul Kambaya kutangaza uamuzi wa kujiondoa uanachama wa Chadema, wenzake 594 wamemkana wakiahidi kusalia ndani ya chama hicho.
Kambaya na wenzake 603 walijiunga na chama hicho siku 54 zilizopita baada ya kujivua uanachama wa CUF walikokuwepo kwa nafasi mbalimbali.
Alipotangaza uamuzi huo Mei 2, 2023 Kambaya alisema: "Tulijiunga CHADEMA wanachama wengi na tulikubaliana vitu vingi lakini tunaona wenzetu wanakiuka makubaliano, kuna suala la kuachiwa majimbo kugombea kwenye uchaguzi ujao."
"Lakini wale tuliowakuta tunaona wameshaanza kujijengea mizizi lakini pia ada ya kujiunga kidijitali tunaona ni kubwa sana sasa tumeamua kuwaachia chama chao kwa nia njema," alisema.
Leo Jumatatu ya Mei 5, 2023 mmoja wa wanachama hao aliyejiunga Chadema pamoja na Kambaya, Shahada Issa amesema hakubaliani na uamuzi wa mwanasiasa huyo.
"Mimi binafsi sikubaliani na yeye (Kambaya) ukiangalia hakuna sababu za msingi amezitoa za kumuondoa Chadema.
"Ameondoka na watu tisa hadi 10 hawatozidi hapo na bahati nzuri watu tulioshirikiana nao bado wapo ndani ya Chadema," amesema.
Hata hivyo, amesema hakuna makubaliano wala ahadi yoyote waliyopeana wakati wanaamua kujiunga na Chadema.
"Kwenye mchakato wa kujiunga na Chadema hatukuwa na makubaliano yoyote badala yake tulizungumza kwamba tunaingia kwenye chama kwa ajili ya kufanya kazi za chama.
"Mambo ya uongozi yatakuja baada ya shughuli zitakazofanywa ndani ya chama," amesema.
Mwanachama mwingine, Ally Mohamed amesema kuondoka kwa Kambaya hakutaathiri chochote ndani ya Chadema.
"Yeye anasema ameleta wanachama 600 wapo walioleta zaidi ya hao kina Mzee Slaa (Wilbroad) na wakaondoka wameiacha Chadema ipo pale pale," ameeleza.
Hata hivyo, ametaka Watanzania wasitafsiri uwamuzi wao wa kujiunga Chadema umelenga kusaka vyeo.
Ameutafsiri uamuzi wa Kambaya kuondoka ndani ya Chadema ni ishara ya kukosa sifa hata ya uongozi.
"Kama changamoto ndogo ndani ya chama anasema zimemshinda, sasa ataweza huo ubunge anaousema maana nao una changamoto kibao," amesema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje, John Mrema amesema: "Hata kama aliahidiwa ubunge uchaguzi unafanyika lini ujue kuna vitu vingine basi bwana."
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Kambaya amejibu: “Sina tatizo ya viongozi wa Chadema wala sitaki kuingia kwenye tatizo hilo wala kujibu maelezo ya Mrema (John) kwa sababu ni kiongozi wa juu.
Kuhusu kilichozungumzwa na Shahda amesema: “Itoshe kusema hivi tujipe muda kesho linaweza kutokea lolote, tusubirie.”