Kikwete ampigia debe Samia urais 2025

Mwenyekiti wa CCM mstaafu, Jakaya Kikwete akizungumza alipohudhuria mkutano mkuu wa 10 wa chama hicho, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete amesema hajaona mwanachama mwingine atakayeweza kuwania urais ndani ya chama hicho na kumshindana na Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam.  Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema kwa sasa haoni mwanachama mwingine ndani ya CCM atakayewania urais mwaka 2025 zaidi ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kikwete ametoa kauli leo Alhamisi Disemba 8, 2022 katika mkutano mkuu wa 10 wa CCM uliiongia siku ya pili ukifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

“Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan), usisikilize porojo za watu kwamba sijui kuna kijana gani au mzee gani atagombea ni upuuzi mtupu, sio kwamba nawazuia, lakini simuoni mwana CCM mwaka 2025 atakayechukua fomu kukupinga labda mambo yaharibike sasa hadi wakati huo.

“Lakini siombei iwe hivyo si mila yetu, lakini niseme ukweli hapa Tanzania leo kuna mwanasiasa maarufu kumshinda Samia? Hayuo ndani ya CCM wala nje ya chama hiki, usibabaishwe na maneno haya,” amesema Kikwete.

Kikwete ambaye pia mwenyekiti mstaafu wa CCM, amemtaka Rais Samia kutobabaishwa na maneno yanayozungumza bila kuwa na ushahidi.  

 “Uongo mtupu, ninacho waombeni ndugu zangu acheni uongo, katika kipindi cha kuelekea uchaguzi huu ukisoma mitandao maneno ni ovyo ovyoo… ambayo yote ya kutunga.

“Mara fulani sijui yupo hivi, anaungwa mkono na mzee huyu ni upuuzi mtupu, tuache hii tabia inakigawa chama chetu bila sababu,” amesema.

Kikwete amemshauri wanaCCM wanaosema maneno hayo kuitwa katika kamati ya maadili na kuelezwa kwamba, amesikika akisema kuna mawaziri wamepewa vyeo na sasa wanatafuta cheo cha uraisi, anapaswa amtaje kama hamjui aambiwe aache uongo na akome.

 “Hii ndio njia pekee itakayoondoa uchonganishi au kuchimbachimba watu, chama chetu kikubwa sana, hakistahili kuvumilia upuuzi kama huu, mkiuvumilia chama hiki kitagawanyika kwa maslahi ya watu wapuuzi na waongo wenye kazi ya kukaa katika mitandao kila siku na kuandika,” amesema.

Ameongeza kuwa Rais Samia na Rais wa Zanzibar wanafanya kazi nzuri na zinazoonekana, akiwataka viongozi wa CCM kuwasaidia wakuu hao kupata utulivu ambao kutozua uongo.