Mafyatu kumkaribisha Rahis kuzindua kijiwe

Nkwazi Mhango

Baada ya kuona kuwa inawezekana kumfyatua, sorry, kumchengua rahis hadi anazindua mangomangoma ya Hamnazoo, mafyatu tunakula mkakati kumkaribisha kuzindua kijiwe chetu cha ndumuu. Naona yule anatikisa kichwa kuwa rahis na vijiwe vya bangii, sorry, nimesema bangili wapi na wapi? Hamkumuona arap Rooter wa kwa njirani akijinoma na mchekeshaji kwa Joji Kichaka akiwatosa wake.

Ama kweli marahis tunao. Jamaa alikodisha pipa kwa bei mbaya akajaza familia na maswahiba wakaenda zao kutanua majuu kwa kodi za mafyatu. Hamkuona vibinti vyake na vinjukuti majuu? Halafu mnashangaa kwa nini Afrika siku zote haiendelei! Kwa uzwazwa huu?

Kimsingi, baada ya urahis kuwa rahisi hasa usawa huu wanene wanavyohaha na kufyatua maigizo ya kupatia kura ya kula, wanjanja ndo wakati wa kuwatumia kirahisi. Lazima tuwarahisishe japo wamejirahisi wenyewe. Hakumsikia profedheha Muongo aliyekataa msosi hotelini eti ‘kuokoa’ njuluku za mafyatu utadhani alianza unene jana? Tuliokua zama za mzee Nchonga, haya ni makufuru yaliyovunja miiko yote kimaadili. Nakumbuka mzee Ruxa alipomkaribisha Mic Jekson. Wee, tulizoza. Hakurudia.

Turejeee inshu. Nani asiyetaka kura ya kula hata ikibidi kuvunja protokali? Kwani, waziri wa michezo hakutosha kuzindua mangomangoma ya Chingaboy aka Hamnazoo aka kijana wa maza on top of mwana wa pekee wa Arushwa na Abuduli? Wasiojua, maza ni maza wa wanangomangoma mbali na kuwa mpenzi mhifadhi, mfadhili na mchambuzi mahiri wa mambo ya mangomangoma. 

Soon, nitamshauri fyatu mhariri wangu ampe safu ya kuchambua mangomangoma ili mafyatu waelewe uzuri. Mwaka huu tutashuhudia mengi. Wasiojua jiulize kwanini, maza, kwanza, alisema jamaa ni kijana wake? Pili, zile ngomangoma siyo za mafyatu, bali akina maza wa kisasa na kisiasa wasio na visasi wala madenguzi.

Nilipoitisha kikao kumkaribu mheshimika, mtukufu, mpendeka, msikivu, mchapakazi, mwelewa, doktari mwenyewe, mmwaga njuluku, fyatu mmoja alidai ninamdhalilisha. Nilimfukuza kigwenani na kumtangaza adui nambari wani wa kaya. 

Kama Katiba inampa kila uwezo hadi wa kimuungu wa kuweza kuumba na kufuga chawa, nani atamzuia kudhamini na kufungua kijiwe au kucheza nchiriku tena unaomsifia kamwaga njuluku tusizoziona? Kwani yeye siyo binadamu wala fyatu? Ukisikia usikivu na kujishusha­­­­––siyo kujirahisisha––kama mafyatu pingaji wanavyoweza kudhani––ndiko huku.

Huku ndiko kupenda mafyatu kiuchakachuaji japo kwa muda hadi kura ya kula ivunwe. Upendo au usanii? Apples and oranges.

Mbali na hayo, siku hizi, siasa zinahitaji kiwango kikubwa cha usanii. 
Hivyo, si vibaya rahis kuwa msanii awatumiaye wasanii wenzake. 

Mmemsahau Njaa kaya kwenda kubembea kule Jomeika utadhani huku hakuna! Mmesahau? Siku hizi ikuu si kukuu tena bali playground ya wasanii? Kesho, sitashangaa kuwaona wakuu wa nkoa na wilaya wakifungua hata vigenge vya kuuzia ulabu kama siyo mmea sorry, mazao yatokanayo na mimea hata kigodoro. Tumeelewana?

Tulikubaliana kumwalika rahis. Tumepanga tumpongeze kwa kuzindua ngoma nzuri kama hizi. Pili, tutamtungia wimbo wa kumpongeza anavyomwaga njuluku na ni simba jike. Hamnazoo aliimba kuwa wamaza ni ngurumbili na nusu. Sisi tutaimba kuwa mamaza hasa maza mwenyewe, ni ngurumbili mia. Tatu, maza ana roho ya chuma. Nani alijua kuwa anamilki runinga binafsi? Tutamtaka ataje miradi yake yote, ukiwemo ukwasi wake na namna alivyoutengeneza na kuuchuma.

Tutampongeza namna maza anavyowahusudu mafyatu maskini kama vile wauza madafu, mitumba na udohoudoho mwingine hadi wengine wakiruhusiwa kuuzia hata pale ikuli. Nadhani umenielewa. Pia, tutamuomba mafyatu hasa Fyatu Mfyatuzi atutaje siku hiyo kama alivyowataja wasanii.

Mafyatu wamenipa mbinu ya kumvutia maza ili anitaje. Lazima nianze usanii. Nitaanza kuimba mapiano na singeli na kimatress nikieleza anavyovutia kura. Nitamsifia kuwa ni goddess kama wale wa Misri zamani, pia kuwakumbuka wasanii. Tutampa maza outing ya nguvu kuliko dingi anavyompa.

Kabla ya kumaliza, lazima nimshawishi maza, atumie kipaji chake cha kujua mangomangoma na wanamangomangoma kusoma vitabu vya watunzi na waandishi wetu wa vitabu nchini waliododa na kusahaulika huku usanii ukipewa thamani kuliko ilmu. 

Tutamwambia katatizo ka kaya. Inakuwaje wasanii tena waimbao ngonongono watajirike lakini waandishi wa vitabu wafe maskini? 
Je, tatizo ni kaya kupenda na kutukuza mambo haya? Hamjaona orodha ya short time guest houses, vilabu na madanguro vilivyo vingi kuliko mashule hadi tunapeleka vitegemezi kwa majirani walioamua kutopenda mambo haya. 

Hamuoni vijigazeti vya udaku vinavyotajirisha wasanii wengi kuliko vitabu vya kiada? Mie mwenyewe niliwahi kuandika kitabu cha kiada kikauawa kwa sababu ambazo sikuambiwa.

Tutamshauri maza, aanze kuandamana na waandishi wa vitabu badala ya wasanii. Ikishindikana, tubadilishe shule na vyuo vyote kuwa vya sanaa huku wizara yake ikihamishiwa ikuu. Wajanja wanawekeza kwenye ilmu, sie kwenye mipasho! Sijui nani katuroga yarabi? Je, tamasha la Hamnazoo kaandaa yeye au katumwa na maza aanze kampani za kampeni kabla ya kipenga? Hivi, uchaguzi, sorry, uchakachuaji ni lini? Kaeni chonjo. Nshaonya.