Makalla: No Reforms, No Election haipingwi na watawala, ni Chadema wenyewe

Muktasari:
- Leo Ijumaa, Mei 23, 2025, katika ufunguzi wa kikao cha Kamati Kuu ya Chadema, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema watawala wanatumia mifumo kutaka kutengeneza vyama mbadala, ili kuziba pengo la Chadema kama chama kikuu cha upinzani, jambo ambalo limepingwa na CCM.
Shinyanga. Hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kueleza ajenda yake ya No Reforms No Election, inavyodaiwa kupingwa na watawala, imekiibua Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimesema upinzani dhidi ya ajenda hiyo upo ndani ya Chadema yenyewe.
CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla, amefafanua hilo akilirejea kundi la watia nia wa ubunge linalounda G55 kutoka ndani ya Chadema, ambalo liliipinga hadharani ajenda hiyo.
Mapema leo Ijumaa, Mei 23, 2025, katika ufunguzi wa kikao cha Kamati Kuu ya Chadema, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema watawala wanatumia mifumo kutengeneza vyama mbadala, ili kuziba pengo la Chadema kama chama kikuu cha upinzani.

Mnyika alienda mbali akisema licha ya vita, Chadema kitashinda. Akasema, "Haya yote ni mapigano ambayo watawala wanayapigana yakilenga No Reforms, No Election, lakini imani yangu chini ya uongozi wenu, vita hii tutaishinda na mapigano yote tutayashinda," amesema Mnyika.
Akichambua hoja hiyo mbele ya mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Town, mkoani Shinyanga, Makalla amesema kuwa amemsikia Mnyika aliyedai kuwa No Reforms, No Election inapingwa na watawala, jambo ambalo mwenezi huyo amelikana.
Makalla, ambaye ameanza ziara mkoani Shinyanga, amesema, “Namwambia Mnyika aache uongo. Kauli mbiu ya No Reforms No Election imepingwa na imekataliwa na wana-Chadema wenyewe, wakianza na kundi la G55. Kundi la pili lililopinga ni baadhi ya vyama vya siasa ambavyo vinashiriki uchaguzi.
“Kundi la tatu ni baadhi ya wananchi wanaojitambua wanaotaka kushiriki uchaguzi, hivyo wamekataa No Reforms, No Election. Wasisingizie dola, No Reforms, No Election imepingwa ndani ya Chadema,” amedai Makalla.
Pia, katika kikao hicho cha Kamati Kuu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche, amesema chama hicho hakijapasuka, na wanaoondoka ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wajumbe wa vyombo vya uamuzi vya chama.
“Kamati Kuu ina wajumbe wengi, aliyeondoka ni mmoja sawa na asilimia mbili. Baraza Kuu lina wajumbe 456, waliondoka 20 pekee, huku Mkutano Mkuu ukiwa na wajumbe 1,194, waliondoka wakiwa ni 34, sawa na asilimia nne,” amesema Heche.
Akichambua hoja hiyo tena, Makalla amesema uimara wa chama haupimwi na viongozi bali wanachama, akiwataka Chadema kuacha kujipa matumaini, akisistiza kuwa kila kukicha watu wanakihama.